BAADA ya Kagera Sugar kujihakikishia kucheza Ligi Kuu Bara msimu wa 2026-2027, timu hiyo imeanza kumfuatilia mshambuliaji wa Fortune Sacco FC, Mkenya Collins Maina baada ya kikosi hicho cha Wanankurukumbi kuvutiwa na kipaji chake.

Nyota huyo alionyesha kiwango kizuri akiwa na Fortune Sacco FC, msimu wa 2025-2026 alimaliza kinara wa ufungaji baada ya kufunga mabao 25 kwenye michuano ya National Super League na kuvutia timu mbalimbali.

Chanzo kutoka ndani ya uongozi wa Kagera Sugar, kililiambia Mwanaspoti, Collins ni miongoni mwa wachezaji wanaofuatiliwa kwa ukaribu kwa ajili ya kujiunga na timu hiyo msimu ujao, ingawa hakuna makubaliano yaliyofikiwa kati ya pande mbili.

“Hakuna makubaliano rasmi tuliyokubaliana kati yetu na menejimenti ya mchezaji mwenyewe, japo ni kweli ni miongoni mwa washambuliaji tunaowaangalia kwa ajili ya kuongeza nguvu, tutaweka wazi hilo muda utakapofika,” kilisema chanzo hicho.

Katika mahojiano ya hivi karibuni na Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Juma Kaseja aliyekirejesha kikosi hicho Ligi Kuu baada ya kushuka daraja msimu wa 2024-2025, alisema malengo ya timu hiyo yameshakamilika, ila suala la usajili bado ni mapema.

“Malengo yetu mama kwa maana ya kuipandisha timu daraja kutoka Championship hadi Ligi Kuu tumeyakamilisha, ila suala la usajili bado ni mapema kulizungumzia kwa sababu tutafanya tathimini na kuangalia maeneo ya kuyaboresha,” alisema Kaseja.

Wakati Ligi ya Championship ikibakisha mzunguko mmoja kukamilisha msimu huu, Kagera iko nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo ikikusanya pointi 71 baada ya kushinda mechi 22, sare tano na kupoteza mbili, ikiwa nyuma ya vinara, Geita Gold inayoongoza na pointi 74, ikishinda mechi 23, sare tano na kupoteza mmoja. Timu hizo mbili zimepanda daraja moja kwa moja.

Kaseja aliyekuwa nyota wa Simba, Yanga na Taifa Stars, akiitumikia pia Kagera akiwa mchezaji na kocha wa makipa, amekirejesha kikosi hicho Ligi Kuu Bara, baada ya kujihakikishia kumaliza nafasi mbili za juu, ikiungana na Geita Gold.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *