MOROGORO: WANANCHI wa Kata ya Kinole, Tarafa ya Mkuyuni, Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro wameipongeza Serikali kwa ujenzi wa Kituo cha Afya Kinole kitakachotoa huduma bora za afya.
Wametoa pongezi hizo kwa nyakati tofauti baada ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Mwang’onda kuweka Jiwe la Msingi la mradi wa ujenzi wa kituo hicho.
Mkazi wa kata hiyo, Rukia Mkangainda amesema changamoto ya huduma za afya kwenye Kinole ilikuwa kubwa na wakati mwingine kulazimika kutumia gharama kubwa za usafiri kufuata huduma kituo cha afya kilichopo mbali.

“Tunashukuru kwa kupata kituo hiki kituo cha afya ambacho kitatusaidia, isipo kuwa tunaomba pia serikali ilete wahudumu wa kutosha wenye upendo na huruma ili wananchi wanufaike kikamilifu,” amesisitiza Rukia.
Mkazi mwingine wa kata hiyo, Mohamed Isa Mohamed amesema wananchi wako tayari kushirikiana na Serikali kuhakikisha kituo hicho cha afya kinakamilika na kuanza kutoa huduma kwa wakati.
“Sisi wananchi tuko bega kwa bega na serikali kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa asilimia mia moja ili tuanze kunufaika na huduma za afya zilizokaribu yetu,” amesema Mohamed.

Naye, Mganga Mkuu Mfawidhi wa kituo hicho, Dk Deus Nestory akisoma taarifa ya mradi huo amesema ujenzi umegharimu Sh milioni 250 zilizotolewa na Serikali Kuu kwa lengo la kuboresha na kuongeza upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wa kata hiyo na maeneo jirani.
Dk Nestory amesema ujenzi huo umehusisha jengo la wagonjwa wa nje (OPD), vyoo matundu matano pamoja na kichomea taka na kwamba umekamilika kwa awamu ya kwanza na unaendelea katika awamu ya mwisho ya umaliziaji ili kuanza kutoa huduma.
Kwa upande wake Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Mwang’onda, amesema kuwa kituo hicho ambacho kipo hatua za mwisho za ukamilishaji na ili kuanza kutoa huduma, ni sehemu ya juhudi za serikali za kuboresha na kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.

“Napenda kumshukuru Rais kwa kuleta fedha zilizowezesha kusogeza huduma za afya karibu na wananchi ,sasa ninawaomba wananchi kutunza miundombinu hii ili iweze kutunufaisha sisi na vizazi vijavyo,” amesema Mwang’onda.