DAR ES SALAAM: ABSA Dar City Marathon imetoa msaada wa vifaa tiba kwa Hospitali ya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha huduma za afya, hususan kwa wajawazito, mama na watoto.

Makabidhiano ya vifaa hivyo yamefanyika leo, Juni 16, 2026, kufuatia mafanikio ya mbio za Absa Dar City Marathon 2026 zilizofanyika Mei 17, 2026 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, pamoja na kampeni ya uchangiaji damu iliyoandaliwa na The Runners Club kwa kushirikiana na wadhamini, washirika, watoa huduma na wananchi mbalimbali.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mnazi Mmoja, Dk Mingole Said, Mratibu wa Magonjwa Yasiyoambukiza (NCDs) wa Manispaa ya Ilala, Dk Milka Mathania, viongozi na wanachama wa The Runners Club, pamoja na wawakilishi wa mdhamini mkuu wa mbio hizo, Absa Bank Tanzania, wadhamini wengine, washirika, watoa huduma na wanahabari.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Dk Mingole Said ameishukuru Absa Dar City Marathon kwa kuichagua Hospitali ya Mnazi Mmoja kuwa mnufaika wa msaada huo kwa mwaka wa tatu mfululizo, huku akisema mchango huo unaendelea kusaidia kuboresha huduma za afya zinazotolewa hospitalini hapo, huku akitoa wito kwa waandaaji wa mbio hizo kuendelea kuiunga mkono hospitali katika matukio yajayo.

Aidha, ameipongeza The Runners Club kwa kuendesha kampeni ya uchangiaji damu, akibainisha kuwa upungufu wa damu salama ni moja ya changamoto kubwa zinazoikabili hospitali hiyo. Alieleza kuwa hospitali hupokea zaidi ya wajawazito 200 katika wodi ya wazazi na kuhudumia zaidi ya watoto 400 kila siku kupitia kliniki ya afya ya uzazi na mtoto.

Kwa upande wake, Mratibu wa Magonjwa Yasiyoambukiza wa Manispaa ya Ilala, Dk. Milka Mathania, amesema magonjwa yasiyoambukiza yanaendelea kuwa changamoto kubwa ya afya ya umma katika Jiji la Dar es Salaam. Alisema programu kama Absa Dar City Marathon zina mchango mkubwa katika kuhamasisha mazoezi ya mwili na kuendeleza mtindo bora wa maisha unaosaidia kupunguza hatari ya magonjwa hayo.

Akizungumza kwa niaba ya The Runners Club, msemaji wa klabu hiyo, Godphrey Mwangungulu, amesema toleo la sita la Absa Dar City Marathon lililofanyika Mei 17, 2026 lilivutia zaidi ya washiriki 4,000 walioshiriki katika mbio za kilomita 21.1, kilomita 10 na kilomita 5 kwa wanaume na wanawake.

Amesema kaulimbiu ya mbio hizo iliakisi dhamira ya klabu ya kuhamasisha maisha yenye afya na kuzuia magonjwa yasiyoambukiza kupitia mazoezi ya kukimbia. Aliongeza kuwa utoaji wa vifaa tiba kwa Kliniki ya Wazazi ya Hospitali ya Mnazi Mmoja ni sehemu ya kutekeleza maono hayo na kurudisha manufaa kwa jamii.

Naye mwakilishi wa Absa Bank Tanzania, Abigail Mutta, amesema benki hiyo imeendelea kuwa mdhamini mkuu wa mbio hizo kutokana na kuamini katika maono ya The Runners Club ya kuhamasisha afya bora kupitia mazoezi ya mwili.

Amesema pamoja na kudhamini mashindano hayo, Absa imekuwa ikiunga mkono shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo utoaji wa vifaa tiba kwa taasisi za afya. Kwa mujibu wake, benki hiyo pia huwahamasisha wafanyakazi na wateja wake kuzingatia afya zao kupitia programu ya Absa Health Club.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *