Dar es Salaam. Tanzania imejipanga kujenga uhuru wa nchi kupitia teknolojia ya akili unde (AI) na siyo kuwa na akili unde inayotengeneza utegemezi.

Hivyo, katika kuhakikisha hilo vijana wamatakiwa kuwa wabunifu kwa kuja na mifumo ya AI itakayotumika kusaidia biashara, ujasiriamali na fursa mbalimbali za ndani na nje ya nchi.

Hayo yamebainishwa leo Jumanne, Juni 16, 2026 wakati wa Mkutano wa Afrika wa Ubunifu na Teknolojia 2026 wenye kaulimbiu ya “Kuimarisha Utawala wa Kidijitali kwa Kuunganisha Usimamizi wa Intaneti, Data, Usalama wa Mtandao na Sera za Teknolojia”, ambapo imezinduliwa ripoti ya uchumi wa kidijitali Tanzania.

Mkutano huo umeandaliwa na Shirika la Tech & Media Convergency (TMC), ambapo wataalamu 45 wamekutana kujadili eneo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na mustakabali mzima wa sekta hiyo.

Kijana Steven Sebastian kutoka Dar es Salaam amesema ni kweli AI ni fursa ambayo ikitumika vyema na chanzo cha ajira ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

“AI inatakiwa itumiwe hata na bodaboda kujua atapata vipi faida na kundi kama mama lishe kifupi ni ya kila mmoja na si kampuni kubwa pekee,” amesema.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama Tanzania, Dk Nkundwe Mwasaga amesema Tanzania imeendelea kujiimarisha katika safari ya kujenga uchumi wa kidijitali, huku Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ikilenga kuinua uchumi huo kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa, AI na uwekezaji katika sekta ya mawasiliano.

“Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi yatakayochochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali kwa kuimarisha matumizi ya intaneti, usalama wa mitandao, ulinzi wa taarifa binafsi na matumizi ya teknolojia bunifu katika sekta mbalimbali za maendeleo,” amesema.

Amesema matumizi ya AI yanafungua fursa mpya za kuongeza tija, ubunifu na ujasiriamali, huku yakichangia kuibuka kwa ajira mpya na kuongeza mchango wa sekta ya kidijitali katika pato la taifa.

“Tunajenga msingi imara wa uchumi wa kidijitali kwa kuhakikisha wananchi wanapata ujuzi wa kidijitali, wanatumia teknolojia kwa usalama na wanashiriki kikamilifu katika fursa zinazotokana na maendeleo ya teknolojia,” amesema.

Aidha, Serikali imejipanga kuweka mifumo ya kupima mchango wa uchumi wa kidijitali katika pato la taifa ili kuhakikisha sekta hiyo inakuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya kiuchumi nchini.

Dk Mwasaga amesema utafiti uliozinduliwa katika mkutano huo utasaidia kutoa mapendekezo yatakayoboresha sera za kidijitali, utawala wa intaneti, usimamizi wa data na matumizi ya teknolojia kwa manufaa ya wananchi na uchumi wa taifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TMC, Asha Abinallah, amesema mkutano huo umewakutanisha wadau kutoka sekta za umma na binafsi pamoja na wataalamu wa Tehama kujadili mustakabali wa uchumi wa kidijitali na namna ya kutumia teknolojia kuleta maendeleo endelevu.

Alisema wataalamu hao wanajadili matokeo ya utafiti uliofanyika kwa kipindi cha miezi 14 kwa ushirikiano na taasisi moja kutoka Marekani, ukiangazia uchumi wa kidijitali, matumizi ya intaneti na ulinzi wa taarifa binafsi.

“Matokeo ya utafiti huo yanatarajiwa kusaidia kuboresha mazingira ya sera na uwekezaji katika sekta ya mawasiliano, huku yakifungua fursa zaidi za ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *