Shinyanga. Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, amewapa watumishi wa Serikali katika Wilaya ya Shinyanga Vijijini siku 14 kukamilisha uchunguzi na kuwasilisha taarifa za kina pamoja na mapendekezo ya utatuzi wa kero zote zilizowasilishwa na wananchi katika Tarafa za Samuye na Nindo.

Akizungumza leo Juni 16, 2026, Mtatiro amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha changamoto za wananchi zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu, na kuondoa tabia ya malalamiko yale yale kujirudia kila anapofanya mikutano ya kusikiliza na kutatua kero katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.

Akizungumza leo Juni 16, 2026, wakati wa ziara yake katika Wilaya ya Shinyanga Vijijini, Mkuu huyo wa Wilaya amesema ameunda timu maalumu itakayoshughulikia kero zote zilizobainishwa na wananchi na kuwasilisha mapendekezo ya suluhu ndani ya muda uliopangwa.

“Kwa kero zote zilizowasilishwa katika mikutano niliyofanya Samuye na Nindo, nimeunda timu na kuiagiza ndani ya siku 14 iwe imefika katika maeneo husika, kuzungumza na wahusika pamoja na wananchi na kuniletea taarifa kamili ya suluhu mezani kwangu. Hii itasaidia kuhakikisha changamoto hizo hazijirudii kila ninapokutana na wananchi,” amesema Mtatiro.

Sambamba na hilo, amewataka watumishi wa Serikali kuhakikisha wanashughulikia migogoro ya ardhi kwa kutumia mifumo ya kiutawala iliyopo kabla ya kufikia hatua ya kupeleka kesi katika mabaraza ya usuluhishi wa ardhi.

Amesema baadhi ya migogoro inayofikishwa kwenye mabaraza hayo inaweza kutatuliwa katika ngazi za utawala wa wilaya endapo viongozi na watendaji watachukua hatua kwa wakati.

“Migogoro ya ardhi ndiyo inaonekana kuongoza kwa wingi katika malalamiko ya wananchi. Nawakumbusha watumishi kutowapa wananchi barua za kwenda kwenye mabaraza ya usuluhishi kabla suala halijafikishwa ofisini kwangu. Kuna migogoro mingi ambayo ipo ndani ya uwezo wetu kuitatua bila kufika katika hatua hizo,” amesema.

Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) Wilaya ya Shinyanga, Emmanuel Mkopi, amewatahadharisha wananchi kuhusu mabadiliko ya gharama za huduma ya maji yatakayoanza kutumika kuanzia Julai 1, 2026.

Amesema bili ya maji itaongezeka kwa Sh100 na wananchi watakapobaini tofauti katika ankara zao wanapaswa kufahamu kuwa ni matokeo ya marekebisho hayo ya bei.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Andrew Mitumba, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.

Ziara ya Mkuu wa Wilaya inaendelea katika maeneo mbalimbali ya Shinyanga Vijijini ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kusikiliza na kutatua kero za wananchi kwa karibu, huku ikisisitiza uwajibikaji wa watendaji katika ngazi zote za utawala.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *