Arusha. Serikali imeanza hatua mpya ya kuimarisha usimamizi wa miradi ya maendeleo nchini baada ya kutangaza kuwa kuanzia Julai 1, mwaka huu, miradi yote itasajiliwa, kufuatiliwa na kutathminiwa kupitia mfumo wa kidijitali wa e-Delivery.

Mfumo huo ulioandaliwa na Tume ya Taifa ya Mipango unalenga kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, sambamba na kusaidia kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akizungumza jijini Arusha wakati wa mafunzo ya awamu ya kwanza kwa watendaji wa serikali, Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Tume hiyo, Salome Kingdom, amesema mfumo huo utatumika kusajili na kufuatilia miradi yote kuanzia hatua ya uibukaji hadi kukamilika kwake.

Amesema e-Delivery utakuwa chombo kikuu cha serikali katika kufuatilia mwenendo wa miradi kwa wakati, hatua itakayowezesha maamuzi kufanyika kwa kutumia taarifa sahihi na za uhakika.

“Miradi yote ya maendeleo itakuwa kwenye mfumo mmoja. Hii itaiwezesha serikali kuona hatua za utekelezaji wa kila mradi na kufanya maamuzi kwa msingi wa taarifa sahihi,” amesema.

Ameongeza kuwa utekelezaji wa mfumo huo unakwenda sambamba na maandalizi ya utekelezaji wa Dira ya 2050, ambapo taarifa za miradi zitasaidia serikali kupanga na kusimamia rasilimali kwa ufanisi zaidi.

“Natoa wito kwa wizara, taasisi, halmashauri na wadau wote kuhakikisha taarifa za miradi zinaingizwa kwenye mfumo. Huu ni mfumo muhimu utakaosaidia serikali kufuatilia matumizi ya fedha kulingana na maendeleo halisi ya mradi,” amesema.

Kwa upande wake, Meneja wa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Tanzania Electric Supply Company Limited (Tanesco), Josephat Odondo, alisema mfumo huo utaleta mageuzi makubwa katika usimamizi wa miradi kwa kuhamisha shughuli nyingi za ufuatiliaji na tathmini kwenye jukwaa la kidijitali.

Amesema utasaidia kubaini changamoto za utekelezaji mapema, kuongeza uwazi na kuhakikisha miradi ya kimkakati inakamilika kwa wakati na kuleta matokeo yaliyokusudiwa kwa wananchi.

Kwa upande wake, Ofisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, Joshua Lukonge, alisema mfumo huo utaimarisha upatikanaji wa taarifa sahihi za miradi na kusaidia serikali kufanya maamuzi yenye tija katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Amesema matumizi ya teknolojia za kidijitali ni nguzo muhimu katika kufanikisha malengo ya Dira ya 2050, ikiwemo kuongeza ufanisi wa matumizi ya rasilimali na kuimarisha ustawi wa wananchi kupitia miradi inayotekelezwa kwa wakati na kwa viwango vilivyokusudiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *