DA ES SALAAM: Taasisi ya Al Ameen Foundation (AIF) imetoa msaada wa vyakula kwa kituo cha watoto yatima cha Upendo Orphane Center, kilichopo Buguruni Ghana, Dar es Salaam leo Juni 17, 2026 ikiwa ni hatua muhimu inayolenga kuboresha ustawi wa watoto wanaolelewa katika kituo hicho.

Msaada huo ni juhudi za taasisi hiyo za kushirikiana na jamii katika kusaidia makundi yenye uhitaji maalumu, hususan watoto yatima wanaohitaji malezi bora, lishe na mazingira salama ya kuishi.

Mwenyekiti wa AIF, Sheikh Ghalib Monero amesema taasisi hiyo imeamua kutoa msaada huo kama sehemu ya kusherehekea mwaka mpya wa Kiislamu kwa vitendo vya kijamii vinavyogusa maisha ya watu wenye uhitaji, hususan watoto yatima.

“Maadhimisho ya mwaka mpya wa Kiislamu huyafanya kwa utaratibu huu kununua vyakula kisha kuleta katika kituo cha watoto yatima, tulikuwa tuna uwezo wa kununua chakula, nyama tukapika, lakini tukaona tufanye hivi,” amesema Sheikh Monero.

Akizungumzia umuhimu wa kutoa msaada kwa watoto yatima, Mwanachuoni Sheikh Yusuph Machelenga amesema suala la kutoa limeelekezwa kwenye Dini ya Kiislamu, hivyo kila mwislamu mwenye uwezo wa kutoa anapaswa kufanya hivyo.

“Jamii hii imesahaulika, yatima wanaowakumbuka ni wachache sana, hivyo tunatoa wito kwa waislamu kwamba hili jambo lina thamani, bora na wasijisahau kuwapa yatima,” amesema Sheikh Yusuph.

Misaada iliyotolewa ni mchele, unga, mafuta ya kula, sabuni na mahitaji mengine mengi ambayo yawatasaidia watoto hao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *