
Babati. Mkazi wa Kijiji cha Kiru Six wilayani Babati mkoani Manyara, Sokoya Aako (60) amefariki dunia kwa kudaiwa kujinyonga kwa kutumia shati kutokana na mgogoro wa kifamilia.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Ahmed Makarani akizungumza Juni 17, 2026 amesema tukio hilo limetokea kwenye Kijiji cha Mawemairo wilayani Babati.
Kamanda Makarani amesema polisi walipewa taarifa kuwa kuna mtu kakutwa amejinyonga juu ya mti kwa kutumia shati na walifika eneo la tukio na kukuta mwili huo.
Amesema polisi wanaendelea na uchunguzi juu ya sababu ya kifo hicho ila uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa chanzo cha kifo hicho ni ugomvi wa familia.
Mmoja kati ya watoto wa marehemu huyo, Samwel Gabriel amesema kabla ya tukio hilo baba yao alitoka kwenye mkutano wa kijiji na kuzozana na familia yake.
Amesema baada ya mzozo huo baba yao aliondoka kwa hasira nyumbani kwake na baada ya siku mbili wakapata taarifa kuwa amejinyonga kwenye kijiji kingine.
Gabriel ameeleza kuwa walipata taarifa kuwa baba yao alikutwa amefariki dunia kwa kujinyonga kwenye mti kwa kutumia shati lake na baiskeli yake ikiwa pembeni yake.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Manyala, Queen Sendiga akizungumzia tukio hilo amesema wanaume hukutana na changamoto nyingi wanapokuwa nje ya familia, hivyo wanahitaji kupata utulivu wanaporejea nyumbani.
“Wakina mama tuwasaidie wanaume zetu jamani, huko nje wanakutana na mengi, vichwa vinaenda ‘resi’, nyumbani tuwape pumziko la mioyo yao, ukute huyu hata hakujua kama anajiua, hasira za kuona mtoto wake hana nidhamu, ghafla kafa kweli,” amesema.