GEITA: MKUU wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela ameagiza watendaji wa serikali kusimamia na kuhakikisha shule za umma zinafikiwa na nishati ya umeme kupitia mradi wa umeme vijijini.
Shigela alitoa maagizo hayo juzi akiwa ziarani wilayani Mbogwe mkoani humo ambapo alipata fursa ya kukagua ujenzi wa miundombinu katika shule ya sekondari Bunigozi na shule zingine.
Alisema kupitia mradi unaotekelezwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) kwenye vitongoji 528 mkoani Geita kwa thamani ya sh bilioni 61, viongozi wahakikishe shule za umma zinanufaika.
Alisema huduma ya umeme shuleni itachochea mazingira rafiki ya wanafunzi kujisomea wakati wa usiku, matumizi ya teknolojia katika maabara na kuimarisha usalama kwenye mabweni.
Alisema serikali ya awamu ya sita inatamani kuona huduma ya umeme inamfikia kila mtanzania ikiwemo wanafunzi, wajasiriamali, wawekezaji na wananchi wa kawaida kwenye maeneo yao.

Shigela aliahidi kufanya mawasiliano na viongozi wa REA kufanikisha huduma ya umeme shuleni huku akimwagiza meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kusimamia suala hilo.
Meneja wa TANESCO wilaya ya Mbogwe, Mhandisi Fabian Rukiko alisema shule zote katika vijiji na vitongoji vilivyonufaika na mradi wa REA zimeingizwa katika mpango wa kuunganishiwa umeme.
Mhandisi Rukiko alisema usanifu unafanyika na bajeti inaandaliwa ili kukamilisha mpango huo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Bunigonzi, George Mwanilyela alisema wamefanikisha ujenzi na ukamilishaji wa miundombinu kwa sh milioni 267 lakini bado kuna uhitaji wa nishati ya umeme.
Mkuu wa shule ya sekondari Lugunga, Mwita Mgosi alisema serikali pia imekamilisha ujenzi wa shule mpya ya Elimu ya Awali na Msingi ya Mkondo mmoja kwa thamani ya sh milioni 330.
Naye Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Mapinduzi, William Msangi aliongeza kuwa serikali imetoa Sh milioni 133 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa sita na matundu 12 ya vyoo katika shule hiyo.