Dar es Salaam. Viongozi wa nchi saba zenye uchumi mkubwa duniani (G7) wamehitimisha mkutano wao wa siku tatu nchini Ufaransa kwa kuahidi kuendelea kuiunga mkono Ukraine, kuhimiza amani Mashariki ya Kati na kuweka msisitizo katika matumizi salama ya teknolojia ya Akili Unde (AI).
Mkutano huo wa 52 uliofanyika katika mji wa Évian-les-Bains nchini Ufaransa kuanzia Juni 15 na kuhitimishwa jana Jumatano, Juni 17, 2026, umeyakutanisha mataifa ya Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, Canada, Uingereza na Marekani, yakiwa ni mataifa yanayounda G7.
Katika mkutano huo, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kupitia tovuti ya habari ya Umoja wa Ulaya, Euronews, msaada kwa taifa la Ukraine ni moja ya mambo yaliyojadiliwa zaidi.
Ukraine iliibuka miongoni mwa wanufaika wakubwa wa mkutano huo baada ya viongozi wa G7 kuthibitisha kuendelea kuiunga mkono katika vita vinavyoendelea dhidi ya Russia.
Katika taarifa ya pamoja, viongozi hao waliahidi kuharakisha utoaji wa mifumo ya ulinzi wa anga, kusaidia miundombinu ya nishati ya Ukraine na kuimarisha vikwazo dhidi ya Russia.
Pia, viongozi hao wameeleza utayari wa kuzingatia kutoa leseni za uzalishaji wa vifaa vya kijeshi kwa Ukraine, hatua inayolenga kuimarisha uwezo wa nchi hiyo kujilinda dhidi ya mashambulizi ya Russia.
Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema Washington itarejesha vikwazo dhidi ya sekta ya mafuta na gesi ya Russia baada ya kusitishwa kwa muda ili kupunguza athari za upungufu wa nishati duniani.
Kwa mara ya kwanza, Trump ameleza wazi kuwa ni Urusi inayopaswa kufikia makubaliano ya kumaliza vita hivyo.
Pia, katika mkutano huo, mjadala kuhusu Mashariki ya Kati ulitawala kutokana na tangazo la Marekani na Iran kuhusu mfumo wa makubaliano ya kuelekea mkataba wa amani.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Iran haitaruhusiwa kumiliki silaha za nyuklia, huku ikitarajiwa kufunguliwa vikwazo vya kiuchumi na kurejeshewa mali zake zilizozuiwa.
Viongozi wa nchi za Magharibi walikaribisha hatua hiyo wakiamini inasaidia kufunguliwa tena kwa Mlango wa Bahari wa Strait of Hormuz, ambao ni njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani.
Trump pia ametoa kauli iliyozua mjadala baada ya kusema kuwa Israel itafanya vizuri zaidi katika kukabiliana na kundi la Hezbollah, huku akihimiza tahadhari zaidi ili kupunguza madhara kwa raia.
G7 yaelekeza macho China
Ingawa China haikuwa sehemu ya mkutano huo, sera zake za kiuchumi zilijadiliwa kwa kina na viongozi wa mataifa hayo saba tajiri duniani.
Kupitia taarifa yao, viongozi hao walionya kuhusu athari za kutokuwepo kwa uwiano katika uchumi wa dunia na kuzitaka nchi zenye ziada kubwa ya biashara ya nje kuimarisha matumizi ya ndani na kuepuka sera zinazoweza kuathiri uchumi wa mataifa mengine.
Kauli hiyo ilionekana kuelekezwa kwa China, ambayo kwa miaka ya karibuni imekuwa ikikosolewa kwa mfumo wake wa uchumi unaotegemea ruzuku za Serikali.
AI yapewa kipaumbele
Teknolojia ya Akili Unde (AI) ilikuwa miongoni mwa ajenda kuu za mkutano huo. Viongozi wa G7 wamekutana na wakuu wa kampuni kubwa za teknolojia kujadili namna ya kuendeleza matumizi ya AI bila kuongeza hatari kwa jamii.
Majadiliano hayo yalihusisha viongozi kutoka OpenAI na Anthropic pamoja na kampuni nyingine za teknolojia.
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron wakati akisalimiana na Rais wa Marekani, Donald Trump walipokutana katika Mkutano wa G7 nchini Ufaransa. Picha na Mtandao
Viongozi hao walikubaliana kuhusu umuhimu wa kulinda watoto katika mazingira ya kidijitali, wakieleza hofu ya matumizi mabaya ya chatbots na maudhui yanayotengenezwa kwa kutumia AI.
Matukio yaliyovuta hisia
Mbali na mijadala rasmi, mkutano huo pia ulizua gumzo kutokana na mazungumzo ya viongozi kunaswa na vipaza sauti vilivyoachwa wazi.
Miongoni mwa matukio yaliyovuta hisia ni mazungumzo ambapo Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni, alinukuliwa akisema ameacha kuvuta sigara mwezi mmoja uliopita, kauli iliyopokelewa kwa pongezi kutoka kwa viongozi wenzake na wadau wa afya duniani.
Ugonjwa wa Ebola na Saratani
Pia, mjadala wa viongozi hao ulijikita katika kutokomeza saratani, ambapo G7 imejitolea kuharakisha juhudi za kutokomeza saratani ya shingo ya uzazi na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika utafiti, hasa kwa saratani za watoto na vijana.
Aidha, wameazimia kuweka malengo makubwa ya upimaji wa mapema ili kupunguza vifo vitokanavyo na saratani ya mapafu ndani ya muongo mmoja ujao.
Jambo lingine ni mlipuko wa aina nadra ya kirusi cha Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Uganda, ambapo G7 imepongeza juhudi za Marekani kukabiliana na ugonjwa huo.
Marekani ilitenga zaidi ya Dola milioni 500 kwa ajili ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo, huku Umoja wa Ulaya ukitoa msaada wa Euro milioni 493 kwa ajili ya usalama wa afya katika ukanda wa Maziwa Makuu.
Viongozi wa G7 wakiongozwa na Marekani, Ujerumani, Uingereza, Ufaransa na Japan wakutana Evian-les-Bains kujadili masuala ya usalama wa dunia na uchumi, huku mgogoro wa Ukraine na ushindani wa kimataifa ukitawala mjadala.
Viongozi hao wamesisitiza umuhimu wa kuzuia virusi hivyo kusambaa mipakani, hususan kuelekea kipindi cha Kombe la Dunia, wakihimiza kuimarishwa kwa mifumo ya karantini na usafiri wa kimataifa.
Suala la madini
Katika nyanja ya uchumi, viongozi wa G7 wamezindua azimio la kulinda mnyororo wa usambazaji wa madini muhimu, ambayo ni uti wa mgongo wa sekta za nishati na kidijitali.
Ili kupunguza utegemezi wa mtoa huduma mmoja nje ya kundi la G7, wameweka lengo la kupunguza utegemezi wa madini adimu (rare earths) hadi chini ya asilimia 60 ifikapo mwaka 2030.
Fahamu kidogo
Kundi la Mataifa Saba Tajiri Duniani (G7) lilianzishwa mwaka 1975 kutokana na mgogoro wa mafuta uliotikisa uchumi wa dunia.
Kundi hilo linaundwa na Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, Uingereza na Marekani. Umoja wa Ulaya (EU) hushiriki katika shughuli za G7 kama mwangalizi, lakini hauhusiki katika mfumo wa uongozi wa kupokezana wa kundi hilo.
Mwaka 1998, Urusi ilijiunga na kundi hilo na kulifanya lijulikane kama G8. Hata hivyo, mwaka 2014 ushiriki wa Urusi ulisitishwa na kundi likarejea kutumia jina la G7.
Mwanzoni, G7 lilijikita kujadili masuala yanayohusu maendeleo ya uchumi wa dunia. Kadri miaka ilivyopita, ajenda zake zilipanuka na sasa zinahusisha masuala mbalimbali ya kimataifa, ikiwemo sera za mambo ya nje, usalama wa dunia, biashara, mabadiliko ya tabianchi na maendeleo.
G7 ni jukwaa lisilo rasmi la wakuu wa nchi na serikali za mataifa wanachama. Kutokana na hali hiyo, halina sekretarieti ya kudumu, kanuni rasmi za uendeshaji wala muundo wa kiutawala ulioanzishwa kisheria.
Wakati wa kuanzishwa kwake, nchi wanachama zilikuwa mataifa saba yenye nguvu kubwa zaidi za viwanda katika ulimwengu wa Magharibi.
Uongozi wa G7 hubadilishana kila mwaka kati ya nchi wanachama, ambapo nchi husika huwa mwenyeji wa mkutano wa viongozi na kuongoza ajenda za kundi hilo kwa kipindi cha mwaka mmoja. Mwaka 2026, taifa la Ufaransa ndilo limekuwa mwenyeji.