
Katika ujumbe wake kwa ajili ya Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Kauli za Chuki, ambayo huadhimishwa kila mwaka Juni 18, Guterres amesema chuki hutumiwa kama nyenzo ya mgawanyiko inayolenga makundi mbalimbali, yakiwemo wanawake, wahamiaji, wakimbizi, watu wa jamii ya LGBTQIA+, watu wenye ulemavu na makundi mengine ya wachache, na mara nyingi kwa manufaa ya kisiasa.
“Kauli za chuki ndiyo hatua ya kwanza katika njia ya kuwanyima watu utu wao, njia ambayo mara nyingi hupelekea vurugu, migogoro na uhalifu wa kutisha,” amesema Guterres.
Amesisitiza kuwa tatizo hilo limekuwa kubwa zaidi katika zama za kidijitali ambapo ujumbe wa chuki unaweza kusambaa kwa kasi isiyokuwa ya kawaida kupitia mitandao ya kijamii na majukwaa ya mtandaoni.
Algoriti za mitandao ya kijamii zakosolewa
Katibu Mkuu huyo amesema maendeleo ya teknolojia, hususan matumizi ya akili Mnemba (AI), yameongeza kasi ya kusambaa kwa taarifa za chuki na upotoshaji. Ameonya kuwa baadhi ya algoriti za majukwaa ya kidijitali zinachochea mgawanyiko kwa kuhamasisha maudhui yanayoibua hasira na migogoro kwa lengo la kuongeza ushiriki wa watumiaji.
Ameongeza kuwa “Algoriti nyingi sana zinasababisha hasira na mgawanyiko, zikihamasisha uongo ili kupendwa au ‘likes’ na kukuza vurugu ili kupata watazamaji zaidi,” amesema. Aidha, ameeleza kuwa kutokujulikana kwa watumiaji mtandaoni kunafanya iwe vigumu kuwawajibisha wanaosambaza kauli za chuki na ujumbe wa uchochezi.
Wito wa hatua madhubuti dhidi ya chuki
Pamoja na changamoto hizo, Guterres amesema kuna suluhu za vitendo zinazoweza kuvunja mzunguko huo hatari.
Ametaja elimu inayowawezesha watu kutambua na kukataa kauli za chuki, msaada kwa waathirika wa unyanyasaji au wa ukatili wa mtandaoni na hatua madhubuti zaidi kutoka kwa serikali na kampuni za teknolojia.
Amesisitiza kuwa nchi zina wajibu wa kisheria chini ya sheria za kimataifa kupambana na uchochezi wa chuki na kukuza ushirikishwaji, kuheshimu tofauti za watu na kuimarisha mshikamano.
Hata hivyo, ameonya kuwa uhuru wa kujieleza haupaswi kutumiwa kama kisingizio cha kusambaza ujumbe unaodhuru wengine.
UN yataka mazingira salama ya kidijitali
Katibu Mkuu amesema Mkakati na Mpango wa Utekelezaji wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Kauli za Chuki pamoja na Kanuni za Kimataifa za Uadilifu wa Taarifa zinatoa mwongozo muhimu wa kujenga mazingira ya kidijitali yaliyo salama na yenye maadili.
Katika maadhimisho haya ya tano ya Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Kali za Chuki, Guterres ametoa wito kwa watu, serikali na taasisi kote duniani kukataa ubaguzi wa aina zote na kushirikiana kujenga dunia inayozingatia haki za binadamu, utu na heshima kwa wote.
Amehitimisha ujumbe wake kwa kusisitiza kuwa “Tukatae chuki katika aina zake zote na tushirikiane kujenga dunia inayojengwa juu ya haki za binadamu, utu na heshima,”