
MMILIKI wa kituo cha Cambiasso Sport Academy kilichopo Tuangoma Kigamboni, Kambi Zuberi Seif(40) na wenzake watano wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka manane yakiwemo ya kuongoza genge la uhalifu, kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine zenye uzito wa kilo 34.89 pamoja na kutakatisha fedha.
Mbali na Zuberi, washtakiwa wengine ni aliyekuwa kocha wa makipa wa timu ya Simba Sport Club, Muharami Sultani(40) maarufu kama Shilton; Maulid Mzungu(54) maarufu kama Mbonde na mkazi wa Kisemvule ambaye ni dalali wa viwanja na muuza nazi.
Wengine ni Said Matwiko(41), ambaye ni fundi seremala na mkazi Magole; John Andrew(40), maarufu kama Chipanda na mkazi wa Kitunda ambaye kazi yake ilikuwa ni kutafuta vijana wenye vipaji na kuwapeleka Cambiasso Sport Academy pamoja na mshtakiwa wa sita ni Sarah Joseph, ambaye ni mke wa Matwiko.
Hii ni mara ya pili kwa washtakiwa hao kufikishwa katika Mahakama ya Kisutu na kusomea mashtaka kama awali, kwa mara ya kwanza ilikuwa ni Novemba 21, 2022, ambapo walisomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 71 ya mwaka 2022 yenye mashtaka manane.
Desemba 5, 2024, washtakiwa hao walisomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo( Committal Proceedings), na kisha kesi hiyo kuhamishiwa Mahakama Kuu, Divisheni ya Rushwa na Makosa ya Uhujumu Uchumi, maarufu kama ‘Mahakama ya Mafisadi’ kwa ajili ya usikilizwaji na ilikuwa mbele ya Jaji Jaji Sharmillah Sarwat.
Hata hivyo, jana Alhamisi Juni 18, 2026 Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) aliwafutia kesi hiyo washtakiwa hao chini ya kifungu cha 92(3) Cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ( CPA) na kisha washtakiwa hao kukamatwa.
Leo Ijumaa Juni 19, 2026 washtakiwa hao wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 13825 ya mwaka 2026.
Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka yao na wakili wa Serikali, Erick Mabagala, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki.
Kabla ya kusomewa mashtaka yao, hakimu Magutu aliwaeleza washtakiwa hao kuwa hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali maalumu.
Pia shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili washtakiwa wote, halina dhamana kwa mujibu wa sheria, hivyo wataendelea kusalia rumande hadi upelelezi utakapokamilika.
Hakimu Nyaki baada ya kutoa maelezo hayo, washtakiwa hao walisomewa mashtaka yao.
Wakili Mabagala alidai shtaka la kwanza ni kuongoza genge la uhalifu shtaka linalowakabiliwa washtakiwa wote ambapo Inadaiwa katika tarehe tofauti kati ya mwaka 2016 na Novemba 4, 2022 maeneo tofauti na ndani ya mkoa wa Dar es Salaam na Pwani washtakiwa hao waliongoza genge la uhalifu kwa lengo la kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin Hydrochloride.
Shtaka la pili ni kusafirisha dawa za kulevya, tukio wanalodaiwa kulitenda Oktoba 27,2022 katika eneo la Kivule wilaya ya Ilala washtakiwa kwa pamoja walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin zenye uzito wa kilo 27.10.
Shtaka la tatu pia ni kusafirisha dawa za kulevya, ambapo Novemba 4, 2023 eneo la Kamegele Wilaya ya Mkuranga, washtakiwa wote walikutwa wakimiliki dawa za kulevya aina ya Heroin zenye uzito wa Kilo 7.79.
Katika shtaka la nne, tano, sita, saba na nane ni ya utakatishaji fedha yanayomkabili mshtakiwa Kambi pekee yake.
Kambi anadaiwa kati ya Aprili 15, 2021 na Aprili 25, 2021 katika Wilaya ya Ilala, alijipatia magari matano aina ya TATA yenye jina la Safia Group of Companies LTD huku akijua mali hizo zilipatikana kwa kosa la kuongoza genge la uhalifu.
Washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yao, upande wa mashtaka ulidai upelelezi haujakamilika na kwamba wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Wakili Mabagala baada ya kutoa taarifa hiyo, wakili wa washtakiwa hao, Josephat Mabula alidai wateja wake wamefutiwa kesi na kwa mujibu wa sheria kesi inapokuwa imefutwa, Jamhuri inapowafungulia kesi nyingine, inapaswa upelelezi uwe umekamilika, hivyo aliomba upande wa Jamhuri unielezee Mahakama umefikia wapi katika suala la upelelezi.
Akijibu hoja hizo, wakili Mabagala alidai kuwa upelelezi bado na ukikamilka wataieleza Mahakama.
Hakimu Nyaki baada ya kusikiliza hoja hiyo aliahirisha hadi Juni 2, 2026 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana kiasi cha dawa wanachodaiwa kusafirisha ni kikubwa na halina dhamana kwa mujibu wa sheria.