Daktari Marie-Roseline Belizaire, ambaye ni Mkurugenzi wa Dharura wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO), akizungumza kutoka Bunia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), leo amewaeleza amesema kuwa mwezi mmoja baada ya mlipuko wa Ebola kutangazwa, hali bado ni mbaya na inaendelea kubadilika.

Amesema maambukizi yanaendelea kuripotiwa katika maeneo mbalimbali, jambo linaloonesha umuhimu wa kuendeleza na kuharakisha juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo. Hadi sasa, wagonjwa 896 waliothibitishwa na vifo 232 vimeripotiwa kutoka kanda 33 za afya katika majimbo matatu ya DRC.

Dkt. Belizaire amesema katika wiki za hivi karibuni ametembelea jamii zilizoathirika, vituo vya matibabu na vituo vya operesheni, ambapo ameshuhudia kujitolea kwa hali ya juu kwa wahudumu wa afya walio mstari wa mbele. Pia amekutana na manusura wa Ebola ambao wameunganishwa tena na familia zao.

WHO inaendelea kuunga mkono Serikali ya DRC na kushirikiana na wadau mbalimbali katika nyanja zote za mwitikio. Zaidi ya wataalamu 115 wa WHO wamepelekwa katika maeneo yaliyoathirika huku tani zaidi ya 110 za vifaa vya dharura zikisambazwa kusaidia shughuli za kukabiliana na ugonjwa huo.

© UNICEF/John James Timu ya wataalamu wa usafi inafanya kazi kuzuia kuenea kwa Ebola huko Bunia, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Shirika hilo limesema uwezo wa uchunguzi na matibabu unaendelea kuongezeka ili kuboresha upatikanaji wa huduma na kupunguza muda wa kuthibitisha kesi. Hata hivyo, changamoto za upatikanaji wa baadhi ya maeneo yenye hatari kubwa na ufuatiliaji wa watu waliokutana na wagonjwa bado zinaendelea kuathiri juhudi za kudhibiti maambukizi.

“Mlipuko huu bado ni tishio kubwa, lakini pia nimeona mwitikio unaozidi kuimarika kila siku. Tunajua nini kinafanya kazi katika kusitisha maambukizi ya Ebola,” amesema Dkt. Belizaire.

UNFPA: Ebola ni dharura pia kwa afya ya uzazi na ulinzi wa wanawake na wasichana

Noemi Dalmonte, Naibu Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) nchini DRC, amesema mlipuko huu wa Ebola siyo tu dharura ya afya ya umma bali pia ni dharura ya afya ya uzazi na ulinzi kwa wanawake na wasichana.

Akizungumza kutoka Kinshasa, amesema wanawake na wasichana walikuwa tayari wanakabiliwa na hatari nyingi kabla ya mlipuko huo, na sasa hali imekuwa mbaya zaidi. Wanawake wengi ndiyo walezi wakuu wa wagonjwa nyumbani, huku wahudumu wengi wa afya walioko mstari wa mbele, hasa wakunga na wauguzi, wakiwa wanawake.

UNFPA imesema kiwango cha vifo kwa wanawake wajawazito wanaoambukizwa Ebola kimewahi kufikia asilimia 90, huku vifo vya watoto wachanga kabla au baada ya kuzaliwa vikifikia asilimia 100 katika baadhi ya maeneo.

Shirika hilo linaendelea kusaidia kuzuia maambukizi katika vituo vya uzazi kwa kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya, kuimarisha mifumo ya usafi na usimamizi wa taka, pamoja na kusambaza vifaa vya kujikinga. Kwa sasa UNFPA ina wakunga 153 walioko mashariki mwa DRC kusaidia huduma salama za uzazi, huduma za dharura kwa wajawazito na huduma baada ya kujifungua.

Bi. Dalmonte amesisitiza kuwa wanawake na wasichana hawapaswi kusahaulika katika mwitikio huu wa Ebola. Ameongeza kuwa UNFPA inahitaji dola milioni 17.1 za Marekani ili kuendelea kutoa huduma za afya ya uzazi, kuzuia ukatili wa kijinsia na kuimarisha ushirikiano na jamii, huku ufadhili uliopatikana hadi sasa ukiwa asilimia 10 pekee ya mahitaji.

UNHCR: Wakimbizi zaidi ya milioni mbili wako katika maeneo yenye hatari ya Ebola

Daktari Allen Maina, Mkuu wa Afya ya Umma katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), amesema zaidi ya watu milioni mbili waliolazimika kuhama makazi yao, wakiwemo wakimbizi zaidi ya 320,000, wanaishi katika maeneo yaliyo katika hatari ya Ebola nchini DRC.

Amesema mapigano yanayoendelea sambamba na mlipuko huo yanachochea hofu kuhusu uhamaji wa watu ndani na nje ya maeneo yaliyoathirika, hali inayoweza kuongeza maambukizi.

Kwa mujibu wa UNHCR, kutokuaminiana kwa baadhi ya jamii dhidi ya timu za mwitikio, pamoja na taarifa potofu kuhusu Ebola, kunaendelea kuchelewesha watu kupata huduma zinazookoa maisha. Shirika hilo linaimarisha maandalizi katika nchi jirani za Uganda, Rwanda, Burundi, Tanzania na Sudan Kusini kwa kushirikiana na WHO na serikali husika.

© WHO/Josua Mulala Raymond Mwezi mmoja baada ya mlipuko wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, uwezo wa utambuzi umeongezeka sana. Maabara nne sasa zinafanya kazi katika maeneo ya afya yaliyoathiriwa, na mbili kati yao pekee zinaweza kusindika karibu sampuli 1,000 kwa mwaka.

Dkt. Maina amesema hatari ya Ebola si ya DRC pekee bali ni ya kikanda kutokana na uhusiano wa kibiashara, kifamilia na mienendo ya wakimbizi katika eneo lote la Maziwa Makuu.

IOM: Zaidi ya watu milioni moja wachunguzwa mipakani kuzuia kusambaa kwa Ebola

Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) limesema limevuka lengo la kufanya uchunguzi wa afya kwa zaidi ya watu milioni moja katika mipaka na njia kuu za usafiri katika nchi zilizoathirika na zile zilizo katika hatari ya Ebola.

Zoe Brennan wa IOM amesema mlipuko huo unatokea katika moja ya njia zenye shughuli nyingi zaidi za kuvuka mipaka barani Afrika, ambapo maelfu ya watu husafiri kila siku wakitafuta usalama, ajira, huduma za afya na kuungana na familia zao.

Katika Jimbo la Ituri pekee, zaidi ya watu 16,000 huvuka mipaka isiyo rasmi kila siku. IOM imekuwa ikitoa msaada katika vituo zaidi ya 110 vya kuingia na kutoka nchini, huku vituo 40 vikiwa katika njia kuu za usafiri.

Bi. Brennan amesema IOM sasa inaongeza shughuli zake nchini DRC na Uganda kwa kuimarisha ufuatiliaji wa afya katika maeneo ya mipakani na njia za usafiri. Ameeleza kuwa hatua hizo ni muhimu si tu kwa kudhibiti mlipuko wa sasa, bali pia kwa kuimarisha uwezo wa nchi kugundua, kuzuia na kukabiliana na milipuko ya magonjwa ya baadaye.

Mshauri Mwandamizi wa Afya ya Uhamiaji wa IOM, Kit Leung, amesema kujenga imani na jamii ni jambo la msingi katika mafanikio ya mwitikio huo, akisisitiza kuwa usafiri na uhamaji wa watu unapaswa kuwa salama na unaofuatiliwa kwa karibu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *