
“Nilipowasili hapa kama mkimbizi, nilikumbana na changamoto nyingi,” alisema. “Niliona jinsi ilivyo rahisi kwa kijana mkimbizi kupoteza udhibiti wa mustakabali wake.”
Kwa baadhi yao, alisema, kuhamishiwa kuishi katika nchi nyingine kunaweza kuonekana kuwa tumaini pekee. Hata hivyo, mchakato huo unaweza kuchukua miaka mingi, wakati mwingine hata miongo kadhaa. Wakati huo, vijana wengi hubaki wakisubiri bila kupata elimu ya kutosha, shughuli za kuwajenga au ajira.Utambuzi huo ulimchochea Stephane na wenzake kuanzisha mabadiliko.
Kuwawezesha wakimbizi
Mwaka 2020, alianzisha Chuo cha Mpira wa Kikapu cha Wakimbizi au Refugee Basketball Academy (RBA), mpango unaowawezesha vijana wakimbizi na wale waliotengwa katika jamii kupata fursa ya kujiendeleza kupitia michezo, mafunzo ya uongozi na elimu.
18-06-2026_DRC-Refugee_Basketball-03
Alitumia mafunzo ya ujasiriamali aliyoyapata kupitia taasisi ya Cosmo au Cosmo Foundation kugeuza wazo dogo kuwa programu ambayo hadi sasa imewafundisha zaidi ya wachezaji 100.Chuo hicho huendesha mazoezi, mashindano na vikao vya ushauri na malezi. Pia hutengeneza video za wachezaji ili kuwasaidia kuunganishwa na shule na fursa nyingine mbalimbali.Stephane anasema kuwa hadi sasa vijana saba wamepata ufadhili wa masomo kupitia programu hiyo. Hata hivyo, kwake lengo si kuzalisha wanamichezo bora pekee. “Hatujengi wachezaji wa mpira wa kikapu tu, tunajenga viongozi,” anasema.
Maisha yaliyojaa majukumu
Stephane mwenyewe ana ratiba yenye shughuli nyingi. Huamka mapema kwa ajili ya mazoezi, huhudhuria masomo katika Chuo Kikuu cha Cavendish ambako anasomea usimamizi na ujasiriamali, kisha hurudi uwanjani baadaye kuwafundisha na kuwalea wachezaji wadogo.
Anasema uwanja wa mpira huwapa vijana mpangilio wa maisha, kujiamini na nafasi ya kuhisi kuwa sehemu ya jamii. Kwa watoto na vijana wengi wakimbizi waliopitia vita au kulazimika kuyahama makazi yao, mpira wa kikapu pia huwapa utulivu ambao ni nadra kuupata. “Tukiwa hapa tunahisi amani,” anasema.
Stephane anatarajia kupanua shughuli za akademia hiyo hadi katika jamii na kambi nyingine za wakimbizi nchini Uganda ili vijana wengi zaidi waweze kupata mafunzo, ushauri na msaada wa kuendelea na masomo.
Kubadili mtazamo kuhusu ukimbizi
Pia anataka vijana wakimbizi wajione kwa mtazamo tofauti, si kama watu wanaosubiri kusaidiwa tu, bali kama watu wenye uwezo, mawazo na mustakabali unaostahili kuwekewa uwekezaji. “Sisi tunaondoka kwenye nyumba zetu,” anasema akizungumzia wakimbizi wanaolazimika kukimbia makazi yao. “Lakini tunaondoka tukiwa tumebeba vipaji vyetu.” Akiwa na shauku kubwa ya kuendeleza uongozi wa vijana na maendeleo endelevu, Stephane ameazimia kuchangia utekelezaji wa Ajenda ya 2030 kupitia uwezeshaji wa vijana, michezo na elimu.
Ujumbe wake ni rahisi lakini wenye nguvu, “kuwa mkimbizi hakupaswi kuonekana kama mwisho wa ndoto za mtu.” Kwa Stephane, uwanja wa mpira wa kikapu ni moja ya maeneo ambako ndoto hizo zinaweza kuanza tena.