Dar es Salaam. Moja ya wanamuziki nguli walioacha alama kubwa katika historia ya muziki wa Tanzania ni Ramadhani Ongala maarufu kama ‘Remmy Ongala’.
Msanii huyo anakumbukwa kwa sauti yake ya kipekee. Nyimbo zenye ujumbe mzito wa kijamii na uwezo wake wa kuzungumza matatizo ya wananchi wa kawaida kupitia muziki.
Nguli huyo aliyepewa jina la ‘Sauti ya Mnyonge’. Alitamba kwa vibao vingi vilivyogusa maisha ya kila siku. Huku akijijengea heshima kubwa ndani na nje ya Tanzania.
Kwa miongo kadhaa, alikuwa miongoni mwa wanamuziki wakubwa zaidi waliowahi kutokea Tanzania, akijijengea heshima ndani na nje ya nchi kupitia muziki wa dansi na soukous.
Remmy aliwahi kukiri kuwa kabla ya kugeukia maisha ya kiroho, aliishi maisha ambayo hakuyaficha kuyataja kuwa ya dhambi na uasi dhidi ya Mungu.
Licha ya changamoto na misukosuko hiyo, kipaji chake cha muziki kiliendelea kung’ara. Huku nyimbo zake nyingi zikibeba ujumbe uliogusa maisha ya kawaida ya wananchi.
Nyimbo kama Muziki Asili Yake Wapi, Dunia na Kalola zilionyesha namna alivyojua kutumia muziki kuzungumzia masuala ya kijamii, maisha ya mwanadamu na wakati mwingine kugusia masuala ya kiroho.
Mashabiki wake walimfahamu kama msanii aliyekuwa na uwezo wa kuwasilisha ujumbe mzito kupitia muziki unaoburudisha.
Akiwa na umri wa miaka 60, Remmy Ongala alitangaza hadharani kuokoka na kuamua kuanza maisha mapya ya imani ya Kikristo.
Katika tukio lililovuta hisia za wengi, alibatizwa katika ufukwe wa Mbezi Beach. Chini ya kanisa la WAPO Mission na kufanya uamuzi mwingine mkubwa wa kunyoa rasta zake zilizokuwa sehemu ya utambulisho wake kwa zaidi ya miaka 40.
Hatua hiyo iliwashangaza mashabiki wengi waliomzoea katika sura yake ya zamani. Baada ya kuokoka, alitangaza kuwa hataki tena kuitwa “Dr. Remmy”. Jina lililompatia umaarufu mkubwa katika muziki. Badala yake alitaka afahamike kama “Mlokole Remmy Ongala”, akieleza kuwa maisha yake yalikuwa yamebadilika kabisa.
Baada ya hapo alijikita zaidi katika nyimbo za injili na kushiriki shughuli mbalimbali za kiroho. Miongoni mwa kazi zake za kipindi hicho ni albamu ya Kwa Yesu Kuna Furaha, iliyodhihirisha mabadiliko makubwa aliyokuwa ameyafanya katika maisha yake.
Hata hivyo, wakati akiendelea na safari hiyo mpya, afya yake ilianza kudhoofika. Nguli huyo wa muziki alifariki dunia usiku wa Desemba 13, 2010 katika Hospitali ya Regency jijini Dar es Salaam kutokana na matatizo ya figo na kisukari.
Remmy alizaliwa mwaka 1947 katika eneo la Kindu, Mkoa wa Kivu, iliyokuwa Zaire zamani na sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kabla ya kuhamia Tanzania ambako alijenga maisha na taaluma yake ya muziki.
Katika maisha yake aliacha familia pamoja na watoto wake. Huku baadhi ya vyanzo vikieleza kuwa alikuwa na watoto watatu miongoni mwao akiwa mwanamuziki na mwanasoka wa zamani Kali Ongala.
Zaidi ya miaka 15 tangu kifo chake, Remmy Ongala anaendelea kukumbukwa si tu kwa mchango wake mkubwa katika muziki wa Tanzania. Bali kwa simulizi ya maisha yake iliyojaa mafanikio, changamoto na mabadiliko makubwa yaliyokuja katika kipindi cha mwisho cha maisha yake.