
Kwa mujibu wa WHO, ongezeko hilo la joto tayari linaweka maisha ya watu hatarini na kuongeza shinikizo katika mifumo ya afya barani Ulaya.
Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Ulaya, Hans Kluge, amesema, “Kanda yetu inashuhudia ongezeko la joto kwa kasi zaidi kuliko maeneo mengine duniani.”
WHO inaeleza kuwa msongo wa joto ni miongoni mwa sababu kuu za vifo vinavyohusishwa na hali mbaya ya hewa, huku ukichochea magonjwa kama moyo, kisukari, pumu na matatizo ya afya ya akili.
“Tunaelewa namna ya kulinda maisha ya watu kwa kutoa tahadhari mapema, kuhakikisha upatikanaji wa maji na kivuli, pamoja na kuandaa mifumo ya afya kabla joto halijafikia kilele,” amesema Dkt. Kluge.
WHO inasisitiza kuwa vifo vinavyotokana na joto vinaweza kuzuilika kwa maandalizi sahihi.
Shirika hilo limewashauri wananchi kunywa maji mara kwa mara, kuepuka kukaa juani kwa muda mrefu hasa nyakati za mchana, kutafuta maeneo yenye kivuli au baridi, na kuwafuatilia watu walio katika hatari zaidi wakiwemo wazee, watoto na wenye magonjwa sugu.
WHO inasema hatua rahisi za tahadhari zinaweza kuokoa maisha wakati wa vipindi vya joto kali.