Kabla ya mikutano muhimu ya Umoja wa Mataifa kuhusu Akili Mnemba AI, shirika la Umoja wa Mtaifa la Masuaka ya Wanawake UN Women limeonya kuwa upendeleo wa kijinsia, ukatili mtandaoni na athari za kiuchumi vinaingizwa ndani ya mapinduzi ya teknolojia ya akili mnemba

Shirika hilo limesema AI, inabadilisha kwa kasi namna dunia inavyowasiliana, kufanya kazi na kupata taarifa. Hata hivyo, bila hatua za haraka kuchukuliwa, teknolojia hii inaweza kuongeza pengo la usawa wa kijinsia duniani, kwa mujibu wa onyo kali lililotolewa na UN Women kabla ya mazungumzo muhimu ya kimataifa kuhusu usimamizi wa AI yatakayofanyika mwezi ujao.

Wakati serikali, kampuni za teknolojia na viongozi wa mashirika ya kiraia wakijiandaa kukutana katika Mdahalo wa Kimataifa wa Umoja wa Mataifa kuhusu Usimamizi wa Akili Mnemba AI na Mkutano wa AI for Good mjini Geneva, UN Women imesema kasi ya matumizi ya AI imezidi juhudi za kuhakikisha teknolojia hiyo inawahudumia wanawake na wasichana kwa usawa.

“AI tayari inabadilisha uhalisia wa maisha kwa mabilioni ya watu,” UN Women imesema. “Swali ni kama uhalisia huo utaakisi maisha na uzoefu wa wanawake, au utaendelea kuwafuta na kuwapotosha.”

© UN Women Deepfakes na Haki za Wanawake: Tishio la AI kwa Usawa wa Kijinsia.

Upendeleo wa kijinsia umejengeka ndani ya mfumo

Shirika hilo limeeleza kuwa ushahidi unaoongezeka unaonesha kuwa ubaguzi wa kijinsia umejikita katika mifumo mingi ya AI inayotumika sasa.

Utafiti uliochunguza mifumo 133 ya AI ulibaini kuwa asilimia 44 ilikuwa na upendeleo wa kijinsia, huku asilimia 26 ikionesha upendeleo wa kijinsia na wa rangi kwa wakati mmoja.

Licha ya kuongezeka kwa matumizi ya AI inayozalisha maudhui, ni asilimia 51 pekee ya wataalamu wa masoko wanaotumia usimamizi wa binadamu kukagua maudhui yanayotengenezwa na AI kabla ya kuchapishwa.

“Upendeleo si hitilafu ya AI,” shirika hilo limesema. “Ni mwenendo uliothibitishwa katika mifumo mingi kwa kiwango kikubwa.”

Tafiti zimeonesha kuwa mifumo mikubwa ya lugha (LLMs) mara nyingi huwahusisha wanawake na maneno kama nyumbani, familia na watoto, huku wanaume wakihusishwa na biashara, mtendaji, mshahara, na kazi.”

Jambo linalotia wasiwasi zaidi kwa mujibu wa UN Women ni kwamba takribani jibu moja kati ya matano yanayotolewa na baadhi ya mifumo ya AI limeonesha mitazamo ya kibaguzi au ya kudhalilisha wanawake, ikiwemo kuwaona wanawake kama vyombo vya starehe za kingono au mali ya waume zao.

“Haya ni matokeo yanayotarajiwa kutoka katika mifumo iliyofundishwa kwa kutumia miongo ya uwakilishi usio sawa wa wanawake na wanaume,” UN Women imesema.

Tatizo hilo halihusiani tu na ubunifu wa teknolojia. Kati ya nchi 138 zilizofanyiwa tathmini, ni nchi 24 pekee zilizotaja masuala ya kijinsia katika mikakati yao ya kitaifa ya AI, huku nchi 18 tu zikiwa na hatua madhubuti za kuhakikisha usawa wa kijinsia.

“Bila hatua za makusudi, ukosefu wa usawa una hatari ya kujengeka ndani ya mifumo ya AI ya baadaye,” shirika hilo limeonya.

AI Inachochea ukatili wa mtandaoni dhidi ya wanawake

UN Women pia imesema kuongezeka kwa maudhui yanayotengenezwa na AI kunaleta vitisho vipya kwa wanawake na wasichana katika mazingira ya kidijitali.

Kwa mujibu wa takwimu za shirika hilo, karibu mwanamke mmoja kati ya wanne waliotafitiwa ambao ni watetezi wa haki za binadamu, wanaharakati au wanahabari, walikumbana na ukatili wa mtandaoni uliosaidiwa na AI.

Asilimia 12 wameripoti kuwa picha zao binafsi au za faragha zilisambazwa bila ridhaa yao, huku asilimia 6 wakisema walilengwa kupitia deepfakes au video na picha zilizobadilishwa kwa njia ya kidijitali.

Zaidi ya robo ya washiriki walipokea jumbe zenye maudhui ya kingono ambazo hawakuzitaka.

“Deepfakes ni miongoni mwa mifano inayoonekana zaidi ya matumizi mabaya ya AI ambayo huwalenga wanawake na wasichana kwa kiwango kikubwa,” UN Women imesema. “Kadiri maudhui yanayotengenezwa na AI yanavyozidi kuwa ya kawaida, ndivyo zana za unyanyasaji, udanganyifu na matumizi mabaya ya picha zinavyoongezeka.”

© UNICEF/Aleksey Filippov Wanawake wanaripoti kuwa waathiriwa wa ukatili mtandaoni.

Wanawake wanaachwa nje ya maamuzi kuhusu AI

Shirika hilo pia limeangazia pengo kubwa la kijinsia ndani ya sekta ya AI yenyewe.

Ingawa AI inatarajiwa kuongeza ajira katika sekta za teknolojia, wanawake wanawakilisha asilimia 30 tu ya nguvu kazi ya AI duniani.

“Watu wanaobuni mifumo hii hawaakisi mabilioni ya watu ambao mifumo hiyo inapaswa kuwahudumia,” UN Women imesema. “Pengo hilo linaongeza ukubwa wa tatizo.”

Ukosefu wa wanawake katika maendeleo ya AI unaibua hofu kuwa bidhaa na sera nyingi zinatengenezwa bila kuzingatia kikamilifu uzoefu, mahitaji na usalama wa wanawake.

Athari za kiuchumi za AI zitawaathiri zaidi wanawake

UN Women imeonya kuwa mabadiliko ya kiuchumi yatakayosababishwa na AI yanaweza kuwaathiri wanawake zaidi kuliko wanaume.

Nje ya sekta ya teknolojia, wanawake wana uwezekano wa karibu mara mbili zaidi kuliko wanaume kuwa katika ajira zilizo katika hatari kubwa ya kubadilishwa na mifumo ya kiotomatiki.

Shirika hilo limesisitiza kuwa madhara ya AI hayaishii kwenye jinsia pekee.

“Ukosefu wa usawa huongezeka pia kutokana na tofauti za rangi, ulemavu, hali ya kiuchumi na eneo la kijiografia,” ripoti hiyo imeeleza. “Makundi ambayo tayari hayawakilishwi vya kutosha ndiyo yaliyo katika hatari kubwa zaidi ya kuachwa nyuma.”

Ujumuishaji ni faida kwa biashara

Licha ya kuonesha hatari zilizopo, UN Women imeeleza kuwa mifumo ya AI inayojumuisha watu wote inaweza kuleta manufaa makubwa kwa biashara.

Utafiti wa kimataifa wa Unstereotype Alliance umeonesha kuwa matangazo yasiyo na mitazamo ya kijinsia yanaongeza mauzo kwa asilimia 3.46 kwa muda mfupi na asilimia 16.26 kwa muda mrefu.

Aidha, chapa zinazokuza ujumuishaji zina uwezekano mkubwa zaidi wa kuwa chaguo la kwanza kwa watumiaji, zina uwezo mkubwa wa kupanga bei na hupata uaminifu mkubwa zaidi kutoka kwa wateja.

Kadiri AI inavyozidi kuwa sehemu muhimu ya upangaji na uzalishaji wa kampeni za matangazo, kampuni zinazoweka ujumuishaji katika mifumo yao zitafaidika zaidi,” UN Women imesema. “Zisizofanya hivyo zinakabiliwa na hatari kubwa za sifa na biashara.”

Wito wa hatua kabla ya kuchelewa

Wakati viongozi wa dunia wakijiandaa kujadili mustakabali wa usimamizi wa AI mjini Geneva, UN Women imetoa wito wa kuhakikisha usawa wa kijinsia unaingizwa katika kila hatua ya mzunguko wa maisha wa AI kuanzia ubunifu, maendeleo, matumizi hadi usimamizi wake.

Shirika hilo linaamini kuwa AI inaweza kusaidia kuongeza uwakilishi, kuboresha upatikanaji wa huduma na kupunguza mitazamo hasi ikiwa itabuniwa na kutumiwa kwa uwajibikaji.

“Uamuzi uko mikononi mwa wale wanaofanya maamuzi,” UN Women imesema. “Iwapo AI itakuza usawa au itaendeleza ubaguzi, itategemea ni sauti zipi zitajumuishwa katika kuamua mustakabali wake.”

Kadiri matumizi ya AI yanavyozidi kuenea duniani, ujumbe wa UN Women ni mmoja, muda wa kujenga mustakabali wa kidijitali wenye usawa wa kijinsia unaendelea kupungua kwa kasi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *