Ni kwa mtazamo huo ndipo hatua mpya za kujikinga dhidi ya Ebola zimeimarishwa katika Gereza Kuu la Bunia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, ambako zaidi ya wafungwa 2,000 wanaishi katika mazingira ya msongamano mkubwa. 

Kituo gerezani

Ndani ya kuta za bluu za gereza hilo, kituo maalum cha muda cha kutenga na kuhudumia wagonjwa wa Ebola kimeanzishwa ili kusaidia kuzuia maambukizi na kulinda afya za wafungwa pamoja na wafanyakazi wa gereza.

Mratibu wa kiufundi wa WHO, Michele Di Marco, amesema ushirikiano wa jamii ulikuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya mradi huo. “Mradi huu umejengwa kwa ushirikiano mkubwa na jamii ya eneo hili. Cha kuvutia zaidi, sehemu kubwa ya kazi ilifanywa na wafungwa wenyewe waliotumia ujuzi na nguvu zao kusaidia. Hii inaonesha namna ushiriki wa jamii unavyoweza kuimarisha mwitikio wa afya ya umma.”

© WHO/Saida Swaleh WHO inaunga mkono ujenzi wa kitengo cha kutengwa katika Gereza la Bunia ili kupokea watu wenye uwezekano wa kuwa na ugonjwa wa Ebola miongoni mwa wafungwa.

Kituo hicho chenye uwezo wa kuhudumia wagonjwa wanne kimejengwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani WHO, kwa ushirikiano na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo MONUSCO. Hatua hiyo inakuja wakati mamlaka za afya nchini humo zikiendelea kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola unaoenezwa na virusi vya Bundibugyo, maambukizi yameripotiwa zaidi katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Katika mazingira ya gerezani, hatari ya maambukizi huwa kubwa zaidi kutokana na msongamano, mwingiliano wa karibu na mzunguko wa watu wanaoingia na kutoka. Wafungwa wa Bunia hukutana mara kwa mara na wageni, hushiriki shughuli za pamoja ikiwemo michezo ya mpira wa miguu, na hutumia maeneo ya pamoja kwa shughuli mbalimbali. Hali hii huongeza uwezekano wa ugonjwa kama Ebola kusambaa kwa kasi iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa mapema.

Kituo hicho kipya kimeundwa mahsusi kwa ajili ya kuwatenga watu wanaoonesha dalili za Ebola ili waweze kufuatiliwa kwa karibu, kupimwa na kupata huduma salama wakati wakisubiri majibu ya maabara. Hatua hii inasaidia kupunguza hatari ya maambukizi miongoni mwa wafungwa, walinzi wa gereza, wahudumu wa afya pamoja na jamii inayozunguka gereza.

Kwa mujibu wa WHO, kituo hicho kina sehemu zinazojitegemea zikiwemo vyoo na maeneo ya huduma kwa wagonjwa. Pia kinaongeza uwezo wa mfumo wa afya wa gereza hilo ambao tayari unahudumia changamoto nyingine za kiafya kama kifua kikuu.

Mafanikio 

Kwa uongozi wa gereza la Bunia, uwepo wa kituo hicho umeleta nafuu kubwa ya kiakili. Mkurugenzi wa Gereza Kuu la Bunia, Zonzi Mokonyo Camille, amesema walikuwa na hofu kubwa kuhusu uwezekano wa kupata mgonjwa wa Ebola gerezani.

“Tunashukuru sana kwa hatua hii ya kujikinga. Tulikuwa na hofu kubwa tukiwaza nini kingetokea kama tungepata mgonjwa aliyethibitishwa kuwa na Ebola hapa gerezani. Leo tunapata faraja kuona kwamba tumejiandaa,” 

© WHO/Nyka Alexander Wagonjwa, wanafamilia na watu walio karibu nao wanapokea usaidizi wa kisaikolojia kama sehemu ya kukabiliana na mlipuko wa Ebola Bundibugyo.

Hatua hii inaonesha ukweli mmoja muhimu katika afya ya umma: kuzuia ugonjwa kabla haujasambaa ndiyo kinga bora zaidi. Katika vita dhidi ya milipuko kama Ebola, maandalizi yanaweza kuwa tofauti kati ya udhibiti wa haraka au janga kubwa.

zaidi ya watoto 130 wapoteza wazazi

Wakati huo huo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF limesema watoto wanaathirika si tu kwa maambukizi ya Ebola, bali pia kwa kupoteza wazazi, unyanyapaa, msongo wa mawazo na kuvurugika kwa huduma muhimu kama afya, elimu, lishe, maji na huduma za ulinzi wa watoto. 

Mkoa wa Ituri umeendelea kuwa kitovu cha mlipuko huo, ambapo watoto 135 waliopoteza wazazi tayari wanapatiwa msaada wa kisaikolojia na huduma za kijamii.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Catherine Russell amesema, “Timu zetu huko Ituri zimekutana na watoto waliopoteza mama zao, na katika baadhi ya matukio wazazi wote wawili, wamefariki dunia kutokana na Ebola.” Ameongeza kuwa, “Watoto wako kwenye mazingira magumu zaidi kwa sababu wanawategemea walezi wao na hawawezi kujitenga kwa urahisi na mzazi au ndugu mgonjwa.”

UNICEF imeonya kuwa watoto na vijana karibu milioni 2.95 mashariki mwa DRC wanakabiliwa na hatari kubwa kutokana na mlipuko wa Ebola, huku idadi ya wagonjwa waliothibitishwa duniani ikifikia 1,000. 

Kwa mujibu wa UNICEF, watoto na vijana wenye umri wa miaka 18 na chini ya hapo wanawakilisha asilimia 54 ya watu wanaoishi katika maeneo 31 yaliyoathirika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *