
Katika hatua za mwitikio wa kitaifa, Tume ya Kudhibiti UKIMWI nchini Tanzania, TACAIDS kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, nchini humo imeendesha warsha ya siku tano kuanzia Juni 15 hadi 19 mwaka huu kwa ajili ya kuwajengea uwezo viongozi wa asasi za vijana na wawakilishi wa vijana katika utetezi wa masuala ya VVU na Afya ya Uzazi.
Mafunzo hayo yamefanyika mjini Tunduma mkoani Songwe Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania jirani kabisa na nchi ya Zambia, ambapo vijana pamoja na wawakilishi wa Asasi za Kiraia kutoka mikoa ya Njombe, Iringa, Mbeya, na Songwe wamejifunza masuala ya uongozi na utetezi wa kimkakati ili kuendeleza mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI.
Kelvin Kisoma, Afisa Vijana wa TACAIDS, Idara ya Mwitikio wa Kitaifa, ameeleza mafunzo hayo ya siku tano yamelenga nini hasa.
“Mikoa hii ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa takwimu za hivi karibuni kwa ushamiri wa maambukizi ya VVU. Kwahiyo, tukaona kuna umuhimu wa kuihusisha hii mikoa katika warsha ili tuwajengee uwezo vijana wa kuweza kufanya utetezi wa masuala mbalimbali yanayohusu UKIMWI. Na kama tunavyojua, kwa takwimu za hivi karibuni, kundi la vijana la miaka 15 mpaka 24 ni kundi ambalo liko kwenye uhatarishi mkubwa sana, kundi ambalo linaongoza kwa kiasi kikubwa cha maambukizi ya VVU, tunaamini kupitia mafunzo haya, tumewajengea uwezo vijana hawa ili tuweze kufikia lengo la kupunguza kiasi cha maambukizi ya VVU kwa vijana,” ameeleza Kelvin Kisoma.
Bwana Kisoma ametoa wito kwa jamii ya Kimataifa kuendelea kutoa ushirikiano na ufadhili, “Kwa asasi za kimataifa, niwaombe tu tuendelee kushirikiana, hasa kwenye eneo la rasilimali ili tuweze kufikia Watanzania wengi zaidi, tuweze kufikia maeneo mengi zaidi. Tunajua tukibaki sisi pekee yetu, tunaweza tukafika kwa kuchelewa sana lakini tukishirikiana na asasi za kimataifa, tutafika kwa haraka zaidi.”
Naye, mwakilishi wa UNICEF, Alice Mwiru ambaye ni mtalaamu wa mabadiliko ya tabia za jamii amebainisha maeneo matatu wanayoshirikiana na TACAIDS.
“Eneo la kwanza ni kuwajengea uwezo wa kujitambua na kuwawezesha vijana kupata taarifa sahihi kuhusu afya, mambo mbalimbali yanayowahusu kama uongozi, ili waweze kuwa wawakilishi kwenye maeneo yao. Eneo lingine ni kutengeneza majukwaa ambayo yatawawezesha vijana kupata taarifa kupitia njia mbalimbali. Kama UNICEF ina jukwaa la kidijitali la U-Report lakini pia tuna apu ya simu ya kufuatilia mzunguko wa hedhi kwa mabinti ambayo ni OKY Tanzania. Hayo majukwaa yanawasaidia vijana kupata taarifa kuhusu afya, kujitambua miili yao, lakini pia kupata nafasi ya kutoa maoni yao katika mambo yanayowahusu,” ameeleza Alice Mwiru.
Bi. Alice Mwiru ameeleza kuwa eneo la mwisho ni kuyajumuisha na kuyashirikisha makundi maalumu, “Eneo la mwisho ni kuwafikia watu wa makundi maalum kama vijana, watoto na wanawake na hata wale wenye ulemavu ili kuweza kupata fursa sawa za kupata taarifa za kuelimika ili waweze kubadilisha tabia zao na kujenga jamii ambazo ni bora, ambazo ziko huru mbali na vihatarishi vya kupata maambukizi.”
Washiriki wameandaa mikakati ya utetezi ya pamoja kwa kila mkoa na kuahidi kwenda kuitekeleza ili kuleta mabadiliko katika jamii.
Gerald Muheto, Afisa Mwandamizi wa Ushirikishaji wa Jamii kutoka taasisi ya HUHESO Foundation mkoani Iringa amefunguka aliyojifunza.
“Kusema ukweli mafunzo ni mazuri toka siku ya kwanza, na ni vitu vingi sana ambavyo tumejifunza mpaka siku ya leo, ambapo tumejifunza masuala mbalimbali yanayohusu UKIMWI, pamoja na sheria ile ya mwaka 2008 ya VVU na UKIMWI. Kwa hiyo, ni mambo mazuri, hasa kwenye upande wa utetezi wa vijana, hususan kwenye masuala mbalimbali ya UKIMWI lakini na masuala mengine ya kimaendeleo,” ameeleza Gerald Muheto.
Balbina Safari, kijana na Afisa Miradi kutoka shirika lisilo la kiserikali la Empower Youth Prosperity la jijini Mbeya, ameeleza namna alivyovutiwa na majukwaa ya UNICEF kwa ajili ya vijana.
“Haya mafunzo yamekuwa ya muhimu sana, ikiwepo kujifunza zaidi kuhusu uchechemuzi na ni njia gani ambazo tutaweza kuzifanya kwenye uchechemuzi ili tukapate uchechemuzi ambao utakuwa na faida na matokeo makubwa. Kitu ambacho nimekipenda sana kwenye haya mafunzo ni apu ya OKY Tanzania, ambayo nilikuwa siijui kabisa. Kwahiyo nitaenda kuwa balozi mkubwa wa kuwafundisha wa kuwapa mabinti waweze kuitumia kwasababu inaweza ikamfundisha binti vizuri kuhusu hedhi,” amesema Balbina Safari.
Awamu hii ya mafunzo ni mwendelezo wa mafunzo ambayo yameshafanyika katika mkoa wa Shinyanga, Morogoro na Mbeya, baada ya mafunzo haya, TACAIDS itaendelea kutafuta rasilimali ili kufikia mikoa mingine, lengo likiwa kufikia mikoa yote ya Tanzania.