Akifungua Mkutano wa Ngazi ya Juu kuhusu UKIMWI kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York hii leo , Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina Mohammed, aliyemwakilisha Kaatibu Mkuu amesema “dunia imefanikiwa kubadili janga hilo kutoka kuwa tishio kubwa la afya kuwa hadithi ya matumaini,” akibainisha kuwa vifo vinavyohusiana na UKIMWI vimepungua kwa asilimia 70 tangu kiwango chake cha juu zaidi mwaka 2004, huku zaidi ya watu milioni 32 wakipata dawa za kuokoa maisha.

© UNAIDS/Cynthia R Matonhodze Mama anayeishi na virusi vya Ukimwi akipokea dawa za kupunguza makali ya VVU kwenye hospitali moja nchini Zimbabwe

Janga la ukimwi halijaisha

Hata hivyo, Bi. Mohammed amesisitiza kuwa janga hilo bado halijaisha. “Tuwe wazi, UKIMWI haujaisha,” amewaambia wajumbe wa mkutano huo. Kufikia mwisho wa mwaka 2024, takribani watu milioni 9.2 waliokuwa wanahitaji matibabu ya VVU walikuwa bado hawajayapata, watu milioni 1.3 walipata maambukizi mapya ya VVU, na watu 630,000 walifariki kutokana na magonjwa yanayohusiana na UKIMWI.

“Kupunguzwa kwa ufadhili kunaathiri moja kwa moja juhudi za kinga na mifumo ya kijamii ambayo ni muhimu katika mapambano haya,” alionya.

Mohammed ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka kupitia vipaumbele vitano muhimu, ikiwemo kuongeza upatikanaji wa huduma za kinga na matibabu, kuimarisha uongozi wa jamii, kulinda haki za binadamu, kuongeza uwekezaji wa kifedha na kufufua mshikamano wa kimataifa.

Amesema ubaguzi na kutengwa kwa makundi mbalimbali bado unachochea maambukizi, hasa kwa watu walio katika mazingira hatarishi.

“Sheria, sera na mifumo ya kijamii inayowasukuma watu pembezoni si tu kwamba inakiuka haki za binadamu, bali pia inadhoofisha juhudi za afya ya umma na kuweka maisha ya watu katika hatari kubwa,” amesema.

Amewataka viongozi wa dunia kuimarisha dhamira yao ya kutokomeza UKIMWI ifikapo mwaka 2030, Bi. Mohammed amesema hakuna nchi inayoweza kufanikisha lengo hilo peke yake.

“Wajibu wa kumaliza UKIMWI kama tishio la afya ya umma ifikapo mwaka 2030 ni wa kila mmoja wetu,” amesema. “Tusonge mbele pamoja kwa dharura, mshikamano na azma ya kweli.”

© WHO/Asad Zaidi Mtaalamu wa maabara anafanya kipimo cha uchunguzi wa VVU katika kituo cha matibabu huko Hayatabad katika wilaya ya Peshawar nchini Pakistan.

UNAIDS: Virusi vinaendelea kusambaa

Akizungumza baada ya hotuba za ufunguzi, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa  linalohusika na masuala ya Ukimwi UNAIDS, Winnie Byanyima, ametoa tathmini ya hali ya sasa ya hatua dhidi ya VVU.

“Kwa mujibu wa shirika la ushirikiano wa kimataifa wa kiuchumi na maendeleo  OECD, ufadhili wa maendeleo ulipungua kwa asilimia 23 mwaka 2025, ikiwa ni kupungua kwa kiwango kikubwa zaidi kuwahi kurekodiwa,” amesema.

Ameonya kuwa programu za VVU katika nchi zenye mzigo mkubwa wa maambukizi na mapato ya chini zimeathirika kwa kiwango kikubwa.

“Takwimu zetu mpya zaidi za UNAIDS, zilizotolewa wiki iliyopita, zinaonesha hali ya kuyumba,” amesema. “Upimaji wa VVU umepungua kwa asilimia 22 katika maeneo yenye mzigo mkubwa wa maambukizi, jambo linalomaanisha kwamba watu wengi hawajui hali zao za maambukizi na virusi vinaendelea kusambaa.”

Hatua za kupambana na ukimwi ziko hatarini

Bi. Byanyima ameongeza kuwa kuwa ufadhili wa mipira ya kondomu umepunguzwa kwa zaidi ya asilimia 90 katika baadhi ya maeneo.

“Juhudi za kinga zinavunjwa wakati ambao tunapaswa kuwa tunaongeza matumizi ya ubunifu kama vile dawa mpya za muda mrefu zinazofanya kazi kwa kipindi kirefu.”

Licha ya changamoto hizo, Bi. Byanyima amesisitiza kuwa kumaliza UKIMWI bado kunawezekana.

“Utafiti bado unaweza kutupatia tiba. Kumaliza UKIMWI kunawezekana, hata hivyo tunakutana katika kipindi hatari,” amesema. “Ushirikiano wa kimataifa uko katika kiwango dhaifu zaidi katika kizazi hiki, huku vitisho vikijiandaa kufuta mafanikio yote tuliyoyapata.”

UNFPA/Junior Mayindu Nchini DRC, maelfu ya watoto bado wanaambukizwa VVU kila mwaka kutokana na ukosefu wa upimaji kwa wanawake wajawazito, fursa iliyopotea ya kuokoa maisha ya akina mama na kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Jamii ziwekwe katikati ya hatua

Akiwakilisha asasi za kiraia, Karen Dunaway, Afisa wa Programu za Kimataifa katika Jumuiya ya Kimataifa ya Wanawake wanaoishi na HIV (ICW), amewasihi wajumbe kukumbuka kwamba sera zinazojadiliwa katika vyumba vya mikutano zinaathiri maisha halisi ya watu.

“Mustakabali wa hatua hizi utategemea maamuzi tunayofanya katika chumba hiki,” amesema.

Ametoa wito wa kulindwa kwa uhuru wa mtu juu ya mwili wake, kuendelezwa kwa usawa wa kijinsia, na kuondolewa kwa sheria na sera zinazotenga, kuhalalisha unyanyasaji wa kisheria dhidi ya, au kuweka unyanyapaa kwa makundi muhimu ya watu.

Mapambano bado jayajakamilika

Akirejelea miongo kadhaa ya harakati na utetezi, amewakumbusha washiriki kwamba maendeleo hayakupatikana yenyewe.

“Kila mafanikio yalihitaji kupiganiwa. Kila kikwazo kilichoondolewa kilihitaji mtu wa kukihoji. Kila ahadi ni uchaguzi,” amesema.

“Hii ndiyo sababu wakati huu ni muhimu. Watu walioko katika chumba hiki wana uwezo wa kuunda hatua dhidi ya VVU ambazo zinaweza kuibadilisha dunia hii kuwa bora zaidi.”

Mkutano huo wa siku mbili unatarajiwa kuhitimishwa  kesho kwa kupitishwa kwa Azimio jipya la Kisiasa, ambalo linakusudiwa kuwa mfumo mkuu wa dunia wa uwajibikaji kwa ahadi za kitaifa kuhusu VVU hadi mwaka 2030.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *