Akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya mtandao kutoka Nairobi, Kenya, msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu, Seif Magango, alianza kwa kutoa takwimu za matukio yaliyothibitishwa.

“Kulikuwa na angalau matukio 546 ya unyanyasaji wa kijinsia unaohusiana na migogoro nchini Sudan kati ya Aprili 15, 2023 hadi katikati ya Aprili mwaka huu, ambayo yamewaathiri angalau watu 838. Hii ni kulingana na uthibitisho tuliofanya sisi wenyewe. Lakini takwimu hizi zinawakilisha sehemu ndogo, kwani matukio mengi hayajaripotiwa.”

© UNOCHA/Giles Clarke Mwathirika wa ukatili wa kijinsia anafunika uso wake kwa mikono yake ndani ya hema yake katika kambi ya wakimbizi huko Tawila, Kaskazini mwa Darfur.

Magango alieleza pia ukubwa wa ukatili huo.

“Karibu robo ya matukio yaliyorekodiwa yalihusisha ubakaji wa magenge. Katika tukio moja, msichana alibakwa na genge la takriban wanaume 10.”

Akizungumzia wahusika wa matukio hayo, Magango alisema:

“Matukio mengi tuliyothibitisha yaliwahusisha wanaume waliovaa sare za Kikosi cha Usaidizi wa Haraka, RSF, washirika wao na wanamgambo wa Kiarabu. Baadhi ya matukio pia yamehusishwa na Jeshi la Sudan, washirika wake na wanamgambo wanaohusiana nalo.”

Ofisi ya Haki za binadamu wakakumbusha jumuiya ya kimataifa kuhakikisha suala la haki halisahauliki.

“Jumuiya ya kimataifa inapaswa kuhakikisha kwamba haki na uwajibikaji vinabaki kuwa sehemu muhimu katika kuunga mkono juhudi za kusitisha mapigano na utatuzi wa mgogoro.”

Hatari kwa siku za usoni

Ripoti hii inaonya kuwa iwapo mifumo na athari hizi za unyanyasaji wa kijinsia zinazohusiana na migogoro zisiposhughulikiwa kupitia haki, majibu na juhudi zinazolenga waathiriwa za kukabiliana na unyanyapaa na ubaguzi, amani na mshikamano wa kijamii nchini Sudan upo hatarini kudhoofishwa kwa miaka ijayo. 

OHCHR wametoa wito kwa wahalifu wote, ikiwa ni pamoja na wale wanaotekeleza jukumu la hilo kwa amri, kuwajibika kikamilifu, na kwa waathiriwa kuhakikishiwa upatikanaji wa suluhisho bora, ikiwa ni pamoja na fidia. 

Pia wamezisihi pande zote katika mgogoro nchini Sudan miongoni mwa mambo mengine, kuchukua hatua madhubuti na zinazoweza kuthibitishwa ili kuzuia unyanyasaji wa kijinsia kwani baadhi ya matukio waliyothibitisha ni uhalifu wa kibinadamu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *