Mshambuliaji nyota wa Namungo FC, Mkongomani Fabrice Ngoy akifunga Hat Trick ya tatu katika Ligi Kuu Bara msimu huu, baada ya kuifungia timu hiyo mabao matatu kwenye ushindi wa 3-2, dhidi ya KMC FC.

Mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex Dar es Salaam, ilishuhudiwa nyota huyo akifunga mabao hayo dakika ya 18, 24 na 52, ikiwa ni Hat-Trick ya tatu, baada ya Mossi Nduwumwe wa Singida Black Stars na Mathew Momanyi wa Pamba Jiji kufunga.

Ushindi huo unakuwa ni wa kwanza kwa Namungo FC baada ya timu kucheza mechi 17, mfululizo za Ligi Kuu Bara bila ya ushindi tangu mara ya mwisho kikosi hicho cha ‘Wauaji wa Kusini’, kilipoichapa pia KMC FC bao 1-0, Januari 31, 2026.

Matokeo hayo yanaifanya KMC iliyoshuka daraja kuendelea kuburuza mkiani na pointi tisa, ikishinda mechi mbili, sare tatu na kupoteza 23, huku kwa upande wa Namungo ikiwa nafasi ya 10 na pointi 30, kufuatia kushinda sita, sare 12 na kupoteza 10.

Kwenye Uwanja wa Airtel mjini Singida, wenyeji Singida Black Stars iliendeleza wimbi la ushindi baada ya kuifunga maafande wa Tanzania Prisons mabao 3-1, huku ikishuhudiwa nyota wa kikosi hicho, Mrundi Mossi Nduwumwe akifunga mawili kati ya matatu.

Mabao hayo mawili ya Mossi yanamfanya nyota huyo kufikisha jumla ya mabao 14, akimfikia kiungo nyota mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’, akizidisha presha katika vita ya ufungaji bora huku zikiwa zimebakia mechi mbili tu.

Bao lingine la Singida limefungwa na beki wa kati wa kikosi hicho, Kennedy Juma na kuihakikishia timu hiyo kumaliza nafasi ya nne na pointi 50, ambazo haziwezi kufikiwa na yoyote, baada ya kushinda mechi 15, sare tano na kupoteza nane.

Bao pekee la Prisons limefungwa na Kelvin Sengati dakika ya 49, ambapo kwa sasa kikosi hicho kinafikisha pointi 26, kikiwa nafasi ya 15 na kuendelea kubakia nafasi ya kushuka daraja, baada ya kushinda mechi saba, sare tano na kupoteza 16.

Kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha, TRA United ilishinda kutamba na kulazimishwa sare ya bao 1-1, dhidi ya Coastal Union, huku Pamba Jiji ikichapwa na Mbeya City mabao 2-0, yaliyofungwa yota na mshambuliaji, Eliud Ambokile.

Bao la TRA United ilifungwa kwa mkwaju wa penalti na nahodha wa kikosi hicho, Nasry Kombo dakika ya 54, kisha mshambuliaji wa Coastal Union, Maabad Maulid akachomoa kwa penalti dakika ya 68.

Fountain Gate ikiwa kwenye Uwanja wa Black Rhino jijini, Arusha, ilishindwa kutamba nyumbani, baada ya kuchapwa bao 1-0, na maafande wa Mashujaa FC, lililofungwa dakika ya 86 na nyota wa kikosi hicho, Hussein Mihambo.

Katika mechi pekee ambayo haijazalisha bao lolote ni ile iliyopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, ambapo wenyeji Dodoma Jiji ililazimishwa suluhu na JKT Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *