Msikilizaji, katika ishara ya mshikamano na mamilioni ya watu wanaokabiliwa na njaa duniani, Papa Leo wa Kumi na nne amezuru ofisi hizi za makao makuu ya Shirika la WFP, mjini Roma hapa nchini Italia.

Akiwa ameandamana na viongozi wa shirika hilo, Papa ametembelea ukuta wa kumbukumbu ya wafanyakazi waliopoteza maisha wakitekeleza majukumu yao, na kuweka shada la maua na kisha akasimama kwenye mimbari kuzungumza na bodi ya utendaji pamoja na wafanyakazi wa WFP kutoka maeneo mbalimbali duniani.

© WFP/Giulio d’Adamo Mtakatifu Papa Leo XIV akiwa katika ziara yake katika Makao Makuu ya WFP huko Roma, Italia.

Katika hotuba yake, Papa Leo amesema njaa siyo tu tatizo la kibinadamu bali pia ni tishio kwa amani na maendeleo ya dunia.

“Ni zaidi ya hofu ya masuala ya kibinadamu , njaa inamomonyoa mshikamano wa kijamii , inaongeza hatari za migogoro na kuchochea kuwalazimu watu kufunga virago na kuhama makazi yao.”

Kwa mujibu wa WFP, ziara hiyo imekuja wakati dunia ikishuhudia ongezeko kubwa la mahitaji ya msaada wa chakula kutokana na migogoro, majanga ya tabianchi na changamoto za kiuchumi zinazoathiri mamilioni ya watu hasa wakati huu ambapo ukata wa fedha umeongeza shinikizo.

Akizungumza na wafanyakazi wa WFP wanaohudumu katika maeneo yenye migogoro na majanga, Papa ametoa pongezi kwa juhudi zao za kuokoa maisha na kuwafikia walio katika mazingira magumu zaidi. Papa ameonya kuwa njaa

” Huendeleza mzunguko wa udhaifu katika jamii na hatimaye kuathiri jumuiya nzima ya kimataifa.”

Hivyo amesisitiza umuhimu wa mshikamano wa kimataifa katika kukabiliana na tatizo hilo.

Ziara hiyo ya Papa Leo wa Kumi na Nne katika makao makuu ya WFP inaonekana kama ujumbe wa matumaini na wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza juhudi za pamoja kuhakikisha hakuna mtu anayelala njaa katika dunia yenye uwezo wa kuzalisha chakula cha kutosha kwa kila mtu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *