Ripoti hiyo ya pamoja iliyotolewa leo na mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la afya ulimwenguni WHO, la nishati IEA, Benki ya Dunia, Idara ya Masuala ya Uchumi na Kijamii ya Umoja wa Mataifa (UNDESA), na shirika la Umoja wa Mataifa la Nishati endelevu IRENA imesema inalenga kuipa jumuiya ya kimataifa taswira ya kimataifa ili kuwa na picha kamili ya maendeleo katika upatikanaji wa nishati, ufanisi wa nishati, nishati mbadala na ushirikiano wa kimataifa ili kuendeleza SDG 7.

Hali ya Afrika

Zaidi ya watu milioni 560 walioko Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara hawana huduma ya umeme, huku milioni 970 wakikosa nishati safi ya kupikia. 

Licha ya maendeleo yaliyopatikana katika baadhi ya maeneo ya dunia, kasi ya upatikanaji wa umeme katika eneo hilo imepungua.

Ripoti inaeleza kuwa kiwango cha upatikanaji wa umeme duniani kilibaki asilimia 92 mwaka 2024. Ili kufikia upatikanaji wa umeme kwa wote ifikapo mwaka 2030, kasi ya maendeleo inapaswa kuongezeka mara tatu, hasa katika maeneo ya vijijini ambako mamilioni ya watu bado wameachwa nyuma.

Makamu wa rais wa Miondombinu kutoka Benki ya dunia Valerie Levkov usalama wa nishati na uwezo wa kumudu gharama zake vimekuwa vipaumbele vya kimataifa, na hii itabaki kuwa changamoto kubwa kwa miaka ijayo.

“ Mahitaji ya umeme yanaongezeka kwa kasi, lakini mamilioni ya watu bado wanaishi bila upatikanaji wa umeme, huku Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ikibeba mzigo mkubwa zaidi na kukosa fursa za ukuaji wa uchumi, ajira, na maendeleo. Tuna suluhisho za kuharakisha maendeleo teknolojia zilizothibitishwa, mifumo bora ya ufadhili, na ushirikiano imara lakini bajeti finyu za umma zinamaanisha kwamba lazima pia tuhamasishe uwekezaji mkubwa zaidi wa sekta binafsi. Tukifanya kazi pamoja, tunaweza kutoa nishati ya kuaminika na nafuu kwa watu wanaoihitaji zaidi.”

Changamoto kiafya

Takribani robo ya watu duniani bado wanategemea kuni, mkaa, mafuta ya taa na makaa ya mawe kwa ajili ya kupikia. Hali hiyo inakadiriwa kusababisha vifo vya watu milioni tatu kila mwaka kutokana na uchafuzi wa hewa majumbani, huku Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiendelea kubeba mzigo mkubwa zaidi.

Mkurugenzi Mtendaji wa WHO Dkt. Tedrso Adhanom Ghebreyesus amesema upatikanaji wa nishati safi na endelevu kwa wote si changamoto ya nishati tu; ni muhimu sana kiafya.

“Uchafuzi wa hewa majumbani kutokana na nishati ya kupikia hugharimu mamilioni ya maisha, husababisha magonjwa na ulemavu wa muda mrefu, na hudhuru mazingira yetu. Huwalemea watu waliokimbia makazi yao kwa kiasi kikubwa na wanawake na wasichana ambao hutumia saa nyingi kukusanya nishati, na kuzidisha ukosefu wa usawa kwa walio hatarini zaidi.”

Dkt. Tedros amesema usalama wa nishati, kupika vyakula safi ni muhimu ili kukuza afya, usawa wa kijinsia, kupunguza mabadiliko ya tabianchi na kupunguza gharama kwa kaya na serikali.

Maendeleo ya nishati jadidifu

Ripoti hiyo inaonesha kuwa nishati jadidifu sasa inachangia zaidi ya asilimia 30 ya umeme unaotumika duniani. Hata hivyo, tofauti kubwa bado ipo kati ya nchi tajiri na maskini, ambapo nchi zenye kipato cha chini zina uwezo mdogo wa kuzalisha nishati hiyo ikilinganishwa na nchi zenye kipato cha juu.

Mkurugenzi Mkuu wa IREA Francesco La Camera mtikisiko uliotokea duniani hivi karibuni kutokana na nishati  umeweka wazi  jambo moja “nchi zenye uwezo mkubwa wa nishati mbadala ziko katika nafasi nzuri ya kuhimili usumbufu wa kiuchumi na usambazaji.”

Amesema kuharakisha upelekaji wa nishati mbadala za ndani zenye ushindani wa gharama sasa lazima iwe muhimu katika kuimarisha usalama wa nishati na ustahimilivu wa kiuchumi, huku ikifuatilia SDG 7. “Ili kufikia hili, jumuiya ya kimataifa lazima itoe kipaumbele kwenye usaidizi wa kifedha unaoweza kugharamiwa na kubinafsishwa, hasa kwa nchi zenye maendeleo duni zinazokabiliwa na vikwazo vikubwa vya upatikanaji.” 

Ufadhili bado hautoshi

Ingawa ufadhili wa kimataifa kwa miradi ya nishati safi katika nchi zinazoendelea uliongezeka kidogo kufikia dola bilioni 24.6 mwaka 2024, kiwango hicho hakitoshi kukidhi mahitaji yaliyopo. 

Nchi maskini zaidi zilipata upungufu wa asilimia 11 wa ufadhili huo ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.

Ripoti hiyo inasisitiza kuwa kuongeza uwekezaji katika nishati jadidifu, mifumo ya umeme ya nje ya gridi, majiko safi na mbinu bunifu za ufadhili kutakuwa muhimu ili kuhakikisha hakuna jamii inayobaki nyuma katika safari ya kufikia nishati nafuu, salama na endelevu kwa wote ifikapo mwaka 2030.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *