
Katika taarifa iliyotolewa Jumanne, Katibu Mkuu wa IMO, Arsenio Dominguez, amesema shirika hilo litaanza kutekeleza operesheni kubwa ya uokoaji kwa ushirikiano na nchi za eneo hilo, Marekani pamoja na sekta ya usafiri wa majini.
Operesheni hiyo ya uokoaji inafuatia miezi kadhaa ya mvutano na mashambulizi dhidi ya meli za kiraia yaliyotikisa mojawapo ya njia muhimu zaidi za usafiri wa baharini duniani na kuwaacha maelfu ya mabaharia wakikwama katika eneo hilo.
Dominguez ameyakaribisha makubaliano yaliyofikiwa kati ya Iran na Marekani, akiyataja kuwa hatua muhimu ya kurejesha usalama wa baharini na kukomesha mashambulizi dhidi ya meli za biashara.
“Baada ya miezi kadhaa ya mateso na hali ngumu kwa maelfu ya mabaharia wasio na hatia, pamoja na athari hasi kwa dunia nzima, ninapokea kwa furaha kubwa makubaliano ya amani yaliyofikiwa kati ya Marekani na Iran,” amesema.
Heshima kwa waliopoteza maisha
Mkuu huyo wa IMO pia ametoa heshima kwa mabaharia 14 waliopoteza maisha wakati wa mzozo huo.
“Huduma na kujitolea kwao katika kuwezesha biashara ya dunia havitasahaulika,” amesema.
Kwa mujibu wa IMO, operesheni ya kuwaondoa mabaharia hao itafanyika kwa ushirikiano wa karibu na Iran, Oman, mataifa mengine ya ukanda huo, Marekani pamoja na sekta ya usafiri wa baharini.
Shirika hilo limesema limepata dhamana za usalama na kuthibitisha kuwepo kwa mazingira salama ya urambazaji ili kuwezesha operesheni hiyo.
Kuhakikisha usalama wa usafiri wa baharini
Katibu Mkuu huyo amesisitiza dhamira ya IMO ya kuwalinda mabaharia na kuhakikisha biashara ya dunia inaendelea kupitia mojawapo ya njia muhimu zaidi za usafiri wa baharini duniani.
“Tunabaki kujitolea kikamilifu kuhakikisha usalama wa mabaharia na mwendelezo wa biashara ya dunia,” amesema.
Mlango wa Hormuz ni njia muhimu ya usafiri wa baharini ambapo sehemu kubwa ya mafuta na bidhaa za biashara duniani hupita, hivyo utulivu katika eneo hilo ni muhimu kwa biashara ya kimataifa na masoko ya nishati duniani.