
“Janga la tabianchi linaongezeka kwa kasi na sasa tunaelekea kuvuka kiwango cha nyuzi joto 1.5 katika miaka michache ijayo,” amesema hayo katika hafla kuhusu vichafuzi hatari vya mazingira wakati wa Wiki ya Tabianchi iliyofanyika London.
Katibu Mkuu amesisitiza kuwa kupunguza ukubwa na muda wa kuvuka kiwango hicho kutahitaji kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa kwa haraka na kuharakisha mpito kutoka matumizi ya nishati ya mafuta ya kisukuku. Amesema hatua dhidi ya vichafuzi hatari ni muhimu kwa kuwa vinachangia karibu nusu ya ongezeko la joto duniani lililoshuhudiwa hadi sasa. “Methane ni kichafuzi kikubwa zaidi miongoni mwa vichafuzi hatari,” amesema, akiongeza kuwa ni “hatua ya haraka zaidi tunayoweza kuchukua ili kupunguza kasi ya ongezeko la joto duniani.”
Guterres ametangaza mwito mpya wa kimataifa wa kuchukua hatua dhidi ya methane, ukilenga uzalishaji unaotokana na sekta za kilimo, taka na mafuta na gesi. Ameeleza kuwa sehemu kubwa ya uzalishaji wa methane katika sekta ya mafuta na gesi inaweza kupunguzwa kwa kutumia teknolojia zilizopo tayari. Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Nishati, takribani asilimia 70 ya uzalishaji wa methane kutoka sekta hiyo unaweza kuondolewa kwa gharama ndogo au bila gharama ya ziada.
Akiwataka serikali na sekta binafsi kuchukua hatua, Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amezitaka nchi kubaini na kuziba uvujaji wa gesi, kukomesha uchomaji na utoaji wa gesi bila matumizi, na kuweka viwango vya kupima, kuripoti na kuthibitisha uzalishaji wa methane. “Enzi ya hatua za hiari imekwisha,” amesema. “Huu ni wakati wa kuwa na kanuni na viwango vya wazi vinavyowekwa na serikali na kutekelezwa na sekta ya viwanda.” Ameongeza kuwa iwapo wazalishaji wote wa mafuta na gesi wangetumia viwango vya Norway, uzalishaji wa methane katika sekta hiyo ungepungua kwa asilimia 90.
Katibu Mkuu amesema kupunguza methane pia ni mtihani wa mshikamano wa kimataifa, hasa kwa nchi zinazoendelea ambazo zinahitaji fedha, teknolojia na uwezo wa kiufundi ili kuchukua hatua. Ametangaza kuwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Mazingira (UNEP) litasaidia kusukuma mbele mwito huo mpya wa kimataifa. “Dunia inaweza na lazima ichukue hatua dhidi ya uchafuzi wa methane,” amesema, akihitimisha kwa wito wa hatua za haraka: “Tuwe kizazi kitakachovuta breki ya dharura ya mabadiliko ya tabianchi kabla ya kuchelewa.”
Tags: , , SDGs