A

Chanzo cha picha, NHC

Iliyochapishwa

Muda wa kusoma: Dakika 6

Vanessa Stafford alipoona taarifa kuhusu miradi mipya ya nyumba inayoendelea Tanzania hakuzungumzia ukubwa wa majengo wala usanifu wake. Badala yake, aliuliza swali lililogusa kiini cha mjadala wa makazi nchini.

“Hivi kweli mwananchi wa kipato cha chini hapo umewasaidiaje? NHC leteni miradi ya nyumba za kawaida za milioni 30 au 50. Mikopo ya nyumba iwe miaka 25 au 30,” aliandika kwenye ukurasa wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Swali lake linakuja wakati Tanzania inaendelea kukua kwa kasi. Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 yanaonyesha nchi ina zaidi ya watu milioni 61, huku Mkoa wa Dar es Salaam ukiwa na wakazi zaidi ya milioni 5.3, idadi kubwa kuliko mkoa mwingine wowote nchini.

Kadiri miji inavyopanuka, ndivyo mahitaji ya makazi yanavyoongezeka. Ripoti ya Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-Habitat), inaonyesha asilimia 44.6 ya Watanzania wanaishi mijini, kiwango kilicho juu ya wastani wa Afrika. Wakati huo huo, tafiti za mtandao wa kimataifa wa serikali za mitaa unaojihusisha na maendeleo endelevu (ICLEI) na Taasisi ya Kimataifa ya Mazingira na Maendeleo (IIED) zinaonyesha kati ya asilimia 70 na 80 ya wakazi wa mijini wanaishi katika makazi yasiyo rasmi.

Katika mazingira hayo, Serikali imeongeza kasi ya uwekezaji katika sekta ya makazi kupitia miradi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), ikiahidi kuongeza upatikanaji wa nyumba bora katika mikoa mbalimbali nchini. Lakini pamoja na maghorofa mapya yanayoibuka na miradi mikubwa inayotangazwa, swali la Vanessa bado linasalia: Je, makazi hayo yanajengwa kwa ajili ya nani?

Ni swali linalohitaji kuangaliwa zaidi ya bei ya nyumba. Linahitaji kutazama ukuaji wa miji, uwezo wa wananchi kumudu makazi, mipango ya Serikali na nafasi ya sekta binafsi katika kuhakikisha ndoto ya nyumba bora haibaki kuwa ya wachache.

Miji inakua, changamoto za makazi nazo zinaongezeka

S

Chanzo cha picha, NHC

Ukuaji wa miji unaonekana wazi kwenye takwimu za kitaifa. Sensa ya Majengo ya mwaka 2022 inaonyesha Tanzania ina majengo zaidi ya milioni 14.3, ambapo asilimia 91.4 yanatumika kwa makazi. Hata hivyo, zaidi ya theluthi mbili ya majengo hayo, sawa na asilimia 67.1, yamejengwa kwenye ardhi ambayo haijapimwa, huku asilimia 33.3 hayana nyaraka rasmi za umiliki wa ardhi.

Changamoto haipo kwenye umiliki pekee. Takwimu hizo zinaonyesha ni asilimia 24.3 tu ya majengo yenye huduma ya maji, asilimia 22.8 yanapata umeme kutoka gridi ya taifa na asilimia 72.6 ndiyo yanafikika kwa barabara. Hii inaonyesha kuwa makazi bora hayamaanishi kuwa na paa la kuishi pekee, bali pia upatikanaji wa huduma muhimu zinazowezesha maisha yenye heshima na usalama.

Kwa mujibu wa ICLEI, kasi ya ukuaji wa miji nchini Tanzania imezidi uwezo wa upangaji wa matumizi ya ardhi na utoaji wa huduma, hali inayochangia kuongezeka kwa makazi yasiyo rasmi. Nayo IIED inaeleza kuwa makazi hayo sasa ni sehemu ya uhalisia wa miji ya Tanzania na yanahitaji sera zinazoyaboresha badala ya kuyaona kama tatizo la kuondoa pekee.

Mtazamo huo unaungwa mkono na Benki ya Dunia kupitia ripoti yake Stocktaking of the Housing Sector in Sub-Saharan Africa, inayosema kuwa Afrika inaweza kuwa na wakazi wa mijini bilioni 1.2 ifikapo mwaka 2050, huku watu wapya milioni 4.5 wakiongezeka kila mwaka kwenye makazi yasiyo rasmi. Ripoti hiyo inaonya kuwa bila sera zinazowezesha upatikanaji wa ardhi, nyumba na mikopo ya makazi, ongezeko hilo litaendelea kuzalisha miji isiyo na huduma za kutosha.

Kwa mkazi wa Tandale, Gasper Lema, changamoto hiyo si takwimu bali maisha ya kila siku. “Kasi ya ujenzi inafurahisha Tanzania, lakini sisi Tandale tunaumia kuishi kwenye nyumba holela. Natamani kila eneo lingekuwa na makazi bora na nafuu,” anasema.

Serikali inajibuje mahitaji hayo?

a

Chanzo cha picha, Fullshan/John

Kutokana na shinikizo hilo, Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya makazi na biashara kupitia Shirika la Nyumba la Taifa (NHC). Lengo si kujenga nyumba pekee, bali kuandaa miji inayoweza kuhimili ongezeko la watu na kuchochea ukuaji wa uchumi wa maeneo ya mijini.

Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2026/27, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo, alisema NHC linaendelea kutekeleza Samia Housing Scheme, mradi wa kimkakati wenye thamani ya Shilingi bilioni 466 unaolenga kujenga nyumba 5,000 katika mikoa mbalimbali nchini. Takribani asilimia 30 ya nyumba hizo zitajengwa Dodoma, huku asilimia 20 zikielekezwa kwenye mikoa mingine, sambamba na miradi inayotarajiwa kutekelezwa Dar es Salaam, Mwanza na Arusha.

Mbali na mpango huo, Serikali inaendelea na ujenzi wa nyumba 422 katika mradi wa Kawe 711 jijini Dar es Salaam wenye thamani ya Shilingi bilioni 169, ambao umefikia asilimia 85 ya utekelezaji. Pia kuna mradi wa Golden Premier Residence wenye nyumba 196 unaoendelea Kawe, huku maandalizi yakikamilika kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 800 za gharama nafuu katika maeneo ya Salama Creek (Kigamboni), Sabasaba (Morogoro), Iyumbu (Dodoma) na Buswelu (Mwanza).

Kwa mujibu wa Dkt. Akwilapo, miradi hiyo inaenda sambamba na utekelezaji wa mpango wa muda mrefu wa kuendeleza maeneo mbalimbali ya mijini. Mfano wake ni mpango wa miaka 20 wa kuendeleza Sinza (2026–2046) unaolenga kubadilisha eneo hilo kuwa kitovu cha kisasa cha makazi, biashara na huduma. Serikali inaamini kuwa upangaji huo utasaidia kuondoa makazi holela, kutumia ardhi kwa tija na kuongeza ubora wa maisha ya wakazi wa miji.

Hata hivyo, wataalamu wanaonya kuwa mafanikio ya miradi hiyo hayatategemea ukubwa wa uwekezaji pekee, bali ushirikishwaji wananchi na unafuu.

Je, makazi bora yanamfikia nani?

.

Chanzo cha picha, NHC

Licha ya uwekezaji mkubwa unaoendelea, mjadala kuhusu uwezo wa Watanzania kumudu nyumba hizo bado haujaisha. Kwa mfano, katika awamu ya kwanza ya Mpango wa Samia wa Makazi (Samia Housing Scheme), bei za nyumba zinaanzia Shilingi milioni 38 (sawa na takriban dola za Marekani 14,600) hadi Shilingi milioni 160 (sawa na takriban dola za Marekani 61,500), kutegemeana na ukubwa na eneo.

Kwa baadhi ya wananchi, bei hizo zinaonekana kuwa nafuu ukilinganisha na thamani ya maeneo husika.

“Utapata wapi Kawe, nyumba ya chini ya milioni 40? umewaza kiwanja?muda?ubora?mazingra? na huduma? kwanug hii ni rahisi sana”, anasema mmoja wa wanunuzi wa nyumba Kawe, ambaye hakupenda kutambuliwa.

Hata hivyo, Serikali inaiona changamoto ya wale wanaoshindw akabiusa kumudu na imeanza kutafuta suluhisho. Januari 2026, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo, aliagiza Shirika la Nyumba la Taifa kufanya tafiti kuhusu teknolojia mpya zitakazowezesha ujenzi wa nyumba bora kwa gharama nafuu zaidi.

“Mfanye tafiti za jinsi ya kujenga makazi bora kwa gharama nafuu na muelewe unafuu huo unamlenga nani, kwa kuwa kuna makundi mbalimbali ya Watanzania,” amesema Dkt. Akwilapo.

Kwa upande wake, Serikali pia inazitumia taasisi za fedha kupunguza mzigo wa malipo ya mkupuo kwa wanunuzi. “Lengo letu ni kuhakikisha kila Mtanzania mwenye ndoto ya kumiliki nyumba anapata suluhisho rafiki la kifedha ili aweze kufikia ndoto hiyo kwa uhakika,” anasema Meneja wa Mikopo ya Nyumba wa Stanbic Bank, Emmanuel Kimaryo.

Hata hivyo, wataalamu wa sekta ya makazi wanaamini kuwa mikopo peke yake haitoshi. Kwa mujibu wa mchambuzi wa masuala ya makazi Afrika kutoka Africa Innovation Network, Kairu Karega, mafanikio ya makazi nafuu yanahitaji mchanganyiko wa sera bora, teknolojia na ushirikishwaji wa wananchi.

“Kutatua tatizo la makazi nafuu Afrika kunahitaji zaidi ya kujenga nyumba. Kunahitaji ubunifu wa usanifu, matumizi ya vifaa vinavyopunguza gharama, sera rafiki na ushiriki wa jamii. Mafanikio ya Rwanda na Mali yanaonyesha kuwa hilo linawezekana,” anasema Karega.

Rwanda anayoitaja imeanza kutumia nyumba zinazojengwa kwa teknolojia ya kisasa zenye gharama ndogo na matumizi madogo ya nishati, huku Mali ikitumia matofali maalumu ya udongo (Hydraulically Compressed Earth Blocks) kupunguza gharama za ujenzi wa nyumba za kijamii. Miradi hiyo imekuwa ikitajwa na wachambuzi kama njia mbadala ya kuongeza upatikanaji wa makazi kwa wananchi wa kipato cha chini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na makazi nafuu barani Afrika (CAHF), Kecia Rust, anasema makazi ya kutosha na yanayomudu gharama ni kichocheo muhimu cha ukuaji wa miji na uchumi.

Anasema makazi yanapopangwa vizuri na kuunganishwa na miundombinu ya miji, huathiri moja kwa moja namna watu wanavyoishi, kufanya kazi na kupata huduma muhimu, huku yakichochea maendeleo endelevu ya miji.

Kwa mtazamo huo, Rust anasisitiza kuwa sera na miradi ya makazi inapaswa kuzingatia mahitaji ya wananchi wa vipato vyote cha chini, cha kati na cha juu kwa kujenga aina mbalimbali za nyumba, kuanzia nyumba za chumba kimoja, au viwili, hadi maghorofa ya makazi na nyumba za kifahari.

Hili linafanywa na NHC na je linaweza pia kuwa jibu la swali la Vanessa Stafford, lenye muelekeo wa kutaka kujua Tanzania inajenga makazi bora kwa ajili ya nani?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *