Video iliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) inaanzia katika mji wa Galaxidi nchini Ugiriki, ambako picha za angani zinaonesha vizimbavya kufugia samaki viliyotanda baharini huku wafanyakazi wakishughulika na uchakataji wa mazao ya samaki kwa ustadi na ufanisi.

Maelfu ya kilomita kutoka hapo, katika mkoa wa Quang Ninh nchini Vietnam, mfugaji wa kamba anaonekana akisimamia bwawa lake la ufugaji, akifuatilia kwa karibu ukuaji na afya ya mazao yake. Watu hawa ambao hapo awali walitegemea zaidi uvuvi wa asili, sasa wamegeukia ufugaji wa kisasa wa viumbe wa majini unaotumia mbinu za kisayansi na teknolojia za kisasa.

© FAO/Veejay Villafranca Boti za uvuvi zatia nanga katika Jengo la Bandari la Jiji la General Santos nchini Ufilipino.

Kupitia mwongozo wa FAO na ushirikiano wa karibu na serikali zao, wafugaji hawa wameimarisha ujuzi na uwezo wao wa kuzalisha mazao bora ya majini, yanayokidhi viwango vya ubora na mahitaji ya soko la ndani na la kimataifa.

“Ufugaji wa samaki unaendelea kuwa mfumo wa haraka zaidi wa kukua wa uzalishaji wa chakula duniani. Kuanzia mwanzo wa karne hadi sasa, umekuwa ukikua kwa karibu asilimia tano kwa mwaka bila kukoma. Na mwelekeo huu unaendelea. Pia tunaweza kuona kwamba uvuvi wa kawaida unabaki imara. Umekuwa imara kwa miaka arubaini iliyopita, na hii ni jambo zuri, kwa sababu ufugaji wa samaki unaongeza nguvu katika sekta iliyokuwa muhimu tayari kwa uhakika wa chakula na lishe.”

Video ya FAO inatuleta eneo jingine  viwanda vya usindikaji ambapo wafanyakazi wanachakata samaki waliovunwa kutoka mabwawa na baharini, mazao hayo yakiwa tayari kwa masoko ya nje ya nchi.

Kwa mujibu wa ripoti ya Hali ya Uvuvi na Ufugaji wa Samaki Duniani ya mwaka 2026, uzalishaji wa ufugaji wa samaki umefikia rekodi ya tani milioni 103 mwaka 2024, huku uvuvi wa kawaida ukizalisha tani milioni 92. Asilimia 89 ya uzalishaji wote unaelekezwa kwa matumizi ya binadamu.

Hata hivyo, sekta hiyo inakabiliwa na tatizo kubwa la mgawanyo usio sawa wa uzalishaji duniani.

Msaidizi Mkurugenzi Mkuu wa FAO na Mkurugenzi wa Kitengo cha Uvuvi na Ufugaji wa Samaki, Manuel Barange, anaeleza changamoto hiyo.

“Mgawanyo wa kijiografia wa uzalishaji wa ufugaji wa samaki unaelemea upande mmoja sana. Karibu asilimia 90 ya uzalishaji unafanyika Asia. Katika mabara mengine, uzalishaji ni mdogo sana. Kwa mfano, Afrika ina chini ya asilimia 2.5 ya uzalishaji wa dunia. Hii inaonesha fursa zilizopo kwa siku zijazo, kama tutaweza kuiga mafanikio ya baadhi ya maeneo na kuyaleta katika maeneo mengine ili kuboresha uhakika wa chakula na lishe ya watu wanaohitaji chakula na protini zaidi.”

UN News/ Devotha Songorwa. Mvuvi akiwa na samaki baada ya uvuvi ziwa Tanganyika.

Katika Ziwa Tanganyika nchini Zambia, wavuvi wanaonekana wakivua samaki kwa mbinu za jadi. Hata hapa, mabadiliko ya tabianchi yanaanza kuathiri uzalishaji na maisha yao.

Ripoti ya SOFIA pia inatoa mwelekeo wa sekta hiyo kwa muongo ujao. FAO inatarajia uzalishaji wa jumla wa samaki, konokono na viumbe vingine vya majini kufikia tani milioni 214 ifikapo mwaka 2034, huku ufugaji wa samaki ukichukua nafasi ya msingi katika ukuaji huu.

“Ifikapo mwaka 2034, sekta ya uvuvi na ufugaji wa samaki itaendelea kukua. Karibu tani milioni 20 zitaongezwa katika uzalishaji, na asilimia 85 ya ongezeko hilo litatoka katika ufugaji wa samaki. Hii inamaanisha kwamba ifikapo mwisho wa mwaka 2034, matumizi yetu ya vyakula vya majini  samaki, kamba, konokono  yatakaribia kilo 22 kwa mtu kwa mwaka, zaidi ya leo, na hivyo kuendelea kuboresha uhakika wa chakula na lishe ya watu wetu duniani.”

Katika kisiwa cha Jeju nchini Korea ya Kusini, wapiga mbizi wanawake wa Haenyeo wanaonekana wakizama ndani ya bahari ili kuvuna makombora na viumbe vingine vya baharini. Ni mfano wa uvuvi endelevu uliodumu kwa vizazi vingi  lakini hata mfumo huu wa zamani unatishiwa na mabadiliko ya tabianchi.

Ripoti ya SOFIA imebaini kwamba zaidi ya theluthi moja ya rasilimali za uvuvi wa baharini bado hazitumiwi kwa njia endelevu  tatizo ambalo linahitaji hatua za haraka.

“Uendelevu wa rasilimali za baharini ni tatizo zito hasa. Asilimia 62 ya uvuvi duniani ni endelevu, na hiyo inamaanisha zaidi ya theluthi moja ya rasilimali hazitumiwi kwa njia endelevu na hali hiyo lazima ibadilishwe.”

© Unsplash/Ed Wingate Nyavu za uvuvi zinahifadhiwa baharini huko Berufjörður nchini Iceland.

Zaidi ya hayo, mabadiliko ya tabianchi yanazidi kuathiri sekta nzima kwa njia mbili kuu: kubadilisha tija ya aina mbalimbali za samaki na kubadilisha maeneo wanayoishi, hali inayoleta msukosuko mkubwa kwa wavuvi, wasimamizi wa uvuvi na masoko.

“Katika uvuvi wa baharini, mabadiliko ya tabianchi yana athari kuu mbili. Ya kwanza ni kwamba baadhi ya viumbe vinakuwa na tija ndogo, na vingine zaidi. Ya pili ni kwamba usambazaji wa viumbe hivyo unabadilika. Hii ni msukosuko mkubwa kwa kila kitu kinachohusiana na uvuvi mahali tunapovua, tunachokivua, jinsi tunavyosimamia uvuvi, na tunachotoa masokoni na kwa walaji. Kwa hivyo, kukabiliana na mabadiliko hayo ni jambo la lazima katika ngazi zote. Tunahitaji kubadilisha taasisi. Tunahitaji kubadilisha mifumo ya usimamizi, tunahitaji kubadilisha uendeshaji wa uvuvi, na tunahitaji kutoa njia mbadala za maisha kwa wale watakaokuwa na athari kubwa zaidi.”

FAO inafanya kazi na nchi wanachama kupitia Ramani yake ya Mwelekeo wa Mabadiliko ya Buluu (Blue Transformation Roadmap) ili kuimarisha uendelevu, tija na ushirikishwaji katika sekta ya uvuvi na ufugaji wa samaki. Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2021, mpango huu umechochea hatua muhimu duniani, zikiwemo miongozo ya ufugaji endelevu wa samaki na mifumo rafiki kwa mazingira

Pamoja na changamoto zilizopo, kuna matumaini makubwa kwamba sekta hii, inayotegemewa na zaidi ya watu milioni 600 duniani, itaendelea kuchangia uhakika wa chakula na lishe bora kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *