
Siku sita baada ya matetemeko makubwa ya ardhi kugonga eneo la kati-kaskazini mwa Venezuela, Carlotta Wolf, msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) ameuambia mkutano wa waandishi wa habari mjini Geneva kwamba katika jimbo la La Guaira, ambalo ndilo lililoathirika zaidi, “upungufu wa chakula umeenea sana”.
UNHCR – watoto peke yao
“Huduma za msingi zimevurugika na mawasiliano yamekatika kwa kiasi kikubwa,” amesema, akiongeza kuwa mvutano wa kijamii unaongezeka huku upatikanaji wa msaada ukiendelea kuwa mdogo.
Bi. Wolf ameeleza kuwa baada ya janga kubwa kama hili, “kuna hofu… watu wanataka kupata msaada haraka iwezekanavyo”.
Tathmini ya haraka ya mahitaji iliyofanywa na UNHCR mwishoni mwa wiki iliyopita katika majimbo ya La Guaira, Eneo la Mji Mkuu, Miranda, Aragua na Carabobo ilionesha kuwa nusu ya waliohojiwa wanakaa kwa majirani au ndugu, wakati “asilimia 39 wanaishi mitaani na katika maeneo ya umma, na wengine kwenye makanisa, shule au vituo vya muda vilivyoboreshwa kwa dharura,” alisema Bi. Wolf.
“Makazi haya ya muda hayakidhi viwango vya chini vya ulinzi… kuhusu faragha, maeneo salama na viwango vya msingi vya usafi na staha,” alisisitiza.
Msemaji wa UNHCR pia ameonesha wasiwasi kuhusu ukweli kwamba “asilimia 17 ya waliohojiwa waliripoti kuwepo kwa watoto wasio na uangalizi au waliotengana na familia zao katika jamii zao.”
Kufikia Jumatatu Juni 29, mamlaka za Venezuela zilithibitisha vifo 1,719, takribani watu 5,034 waliojeruhiwa na 15,866 walioathirika au kupoteza makazi, UNHCR imesema.
“Huduma za afya ziko chini ya shinikizo kubwa sasa,” amesema Christian Lindmeier, msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO), akibainisha ongezeko la wagonjwa wa majeraha ambalo limezidi uwezo wa vituo vya afya.
WHO – Hali tete ya afya
Takwimu za WHO zilizothibitishwa Jumamosi kuhusu vituo 21 vya afya katika Caracas, La Guaira, Miranda na Falcón zinaonesha kuwa vitatu viko “katika hali mbaya sana,” sita vina uharibifu wa miundombinu au vinafanya kazi kwa sehemu, “na vingine vyote vinaendelea kutoa huduma chini ya mzigo mkubwa,” alisema.
Bwana Lindmeier ameonya kuhusu “utoaji huduma wenye mkanganyiko na mtiririko wa wagonjwa, uliojaa msongamano, kuchelewa kwa upasuaji… kuvunjika kwa hatua za usalama wa kibayolojia, na wafanyakazi waliochoka sana.”
Pia amebainisha “mapengo makubwa” ikiwemo kuporomoka kwa huduma za uchunguzi wa maiti na hifadhi za maiti, pamoja na usajili usiotosha wa majeruhi na ufuatiliaji wa watu waliopotea.
“Kuna hatari kubwa sasa ya milipuko ya magonjwa yanayoweza kuzuilika kwa chanjo, kama surua, diphtheria, kifaduro, pamoja na homa ya manjano na magonjwa mengine yanayoenezwa na wadudu na maji, ikiwa ni pamoja na dengue, chikungunya, Zika, oropouche na malaria,” ameonya.
Msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani, WHO pia ameeleza “hatari kubwa ya kiafya” kwa watu waliopoteza makazi, kutokana na kiwango cha chini cha chanjo kabla ya tetemeko, na upatikanaji mdogo wa chanjo kwa sasa.
Bwana Lindmeier alieleza zaidi kuwa baadhi ya wahudumu wa afya katika La Guaira bado hawajulikani walipo, wakiwemo wanaohusika “na mnyororo mzima wa huduma za afya ya uzazi katika eneo hilo” hali inayosababisha pengo kubwa katika huduma za uzazi.
UNDP na vifusi
Nalo Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo UNDP limetoa tathimini ya awali inayoonesha kuwa vifusi vilivyotokana na matetemeko hayo ni tani milioni 1.2.