
Kwa mujibu wa UNICEF kwenye taarifa iliyotolewa leo Juni 30 jijini New York, Marekani kuelekea Mdahalo wa Kwanza wa Kimataifa kuhusu Utawala wa Akili Mnemba, AI imekuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya watoto duniani, ikileta fursa katika kujifunza, ubunifu na maendeleo ya maarifa, lakini pia ikiambatana na hatari mpya zinazohitaji hatua za haraka za ulinzi na usimamizi.
Uchambuzi wa UNICEF uliotumia takwimu kutoka nchi 10 unaonesha kuwa angalau watoto milioni 20 tayari wametumia AI. Takribani watoto milioni mbili, sawa na mtoto mmoja kati ya 10, wamesema hutumia AI kupata ushauri kuhusu mambo yanayowatia wasiwasi, huku zaidi ya watoto milioni 13 wakitumia teknolojia hiyo kusaidia masomo na kazi za nyumbani.
Shirika hilo limeonya kuwa pamoja na kuongezeka kwa matumizi ya Akili Mnemba miongoni mwa watoto, mifumo ya sheria na utawala wa teknolojia hiyo haijaendana na kasi hiyo. Watoto wanakabiliwa zaidi na athari za namna mifumo ya AI inavyobuniwa, jinsi taarifa zao binafsi zinavyotumiwa na mifumo ya kibiashara inayoiendesha, ilhali wana uwezo mdogo wa kujilinda au kupinga matumizi hayo.
UNICEF pia imeeleza kuwa ushahidi kuhusu athari za Akili Mnemba katika maendeleo ya kiakili, ustawi wa kihisia na usalama wa watoto bado unaendelea kujitokeza, hali inayomaanisha kuwa kizazi cha sasa kinakulia katika mazingira ambayo athari zake za muda mrefu bado hazijafahamika kikamilifu.
Kwa mujibu wa utafiti huo, theluthi moja ya watoto waliohojiwa wameeleza kuwa wana hofu kuhusu matumizi ya akili mnemba katika utapeli, udanganyifu na usambazaji wa taarifa potofu. Aidha, robo ya watoto hao wana wasiwasi kuwa picha au video zao zinaweza kubadilishwa na kutumiwa kutengeneza maudhui ya kingono kwa kutumia teknolojia ya ‘deepfake’ ambapo sura ya mtu inaweza kupachikwa katika video ya umbo la mtu mwingine.
Kutokana na changamoto hizo, UNICEF imezitaka serikali kuwekeza katika tafiti kuhusu athari za akili mnemba kwa maendeleo na ustawi wa watoto, kuimarisha sheria na mifumo ya uwajibikaji ili kuzuia unyanyasaji na unyonyaji wa kingono unaowezeshwa na akili mnemba, pamoja na kuhakikisha mifumo ya akili mnemba inabuniwa kwa kuzingatia usalama wa juu na uwazi.
Shirika hilo pia limetoa wito wa kuongeza elimu kuhusu matumizi salama ya akili mnemba kwa watoto, wazazi na walezi, pamoja na kuwekeza katika miundombinu ya kidijitali na upatikanaji wa intaneti ili kupunguza pengo la matumizi ya akili mnemba kati ya nchi na ndani ya nchi.
UNICEF imesema uamuzi utakaofanywa sasa kuhusu usimamizi wa akili mnemba utaamua kwa kiwango kikubwa usalama, faragha, ustawi na fursa za watoto kwa miongo mingi ijayo.