
Baada ya miongo kadhaa hatimaye hii leo Umoja wa Mataifa umeondoa kanuni ya kifedha iliyokuwa ikiulazimisha kurejesha kwa nchi wanachama fedha ambazo hazikutumika hata kama fedha hizo hazikuwa zimewasilishwa kabisa.
Uamuzi huo uliofanywa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa siku ya Jumanne unafuatia mapendekezo ya Kamati ya Tano, ya Baraza hilo ambayo inashughulikia masuala ya utawala na bajeti.
Hatua hiyo imekuja wakati Umoja wa Mataifa ukiendelea kukabiliwa na ukata kutokana na baadhi ya nchi wanachama kuchelewesha kulipa michango yao ya lazima ya kifedha. Hali hiyo imelazimisha kupunguzwa kwa matumizi katika mfumo mzima wa Umoja wa Mataifa, jambo linaloathiri vibaya ajira, operesheni za kulinda amani na utoaji wa misaada ya kibinadamu.
Guterres apongeza mageuzi muhimu
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, kupitia taarifa yake iliyotolewa baada ya upigaji kura kupitisha azimio hilo, amekaribisha uamuzi huo akisema kuwa kanuni za zamani za kifedha zilikuwa zinahatarisha “uthabiti wa Umoja wa Mataifa.”
“Kwa kura yake, Baraza Kuu limekubali kuanzisha, kwa kipindi cha majaribio cha miaka minne, mbinu mpya itakayohakikisha kuwa fedha ambazo hazijatumika zinarejeshwa kwa nchi wanachama pale tu zinapokuwa zimewasilishwa taslimu na kupokelewa” amesema Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa.
“Uamuzi huu utatuwezesha kusimamia rasilimali, hasa kwa bajeti ya kawaida na bajeti ya operesheni za kulinda amani, kwa njia iliyo thabiti zaidi na yenye uwajibikaji, na kutekeleza kwa ufanisi zaidi mamlaka tuliyopewa na Nchi Wanachama.”
Muhimu kwa mustakabali wa karibu wa Umoja wa Mataifa
Guterres ameeleza mabadiliko hayo kuwa ni “muhimu sana kwa mwendelezo wa shughuli zetu za haraka, hasa operesheni za kulinda amani,” na akasema yatakuwa maboresho makubwa kwa Katibu Mkuu ajaye atakayechukua madaraka mwezi Januari mwaka ujao baada ya yeye kutamatisha kipindi chake Desemba 31 mwaka huu.
Afisa huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa hatalazimika tena kurejesha fedha ambazo, kama illivyokuwa kwamba, “mara nyingi hazikuwahi hata kupokelewa.”
Kiwango cha juu zaidi cha madeni ya michango
Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya Katibu Mkuu kuhusu hali ya kifedha ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa mwezi uliopita, Umoja wa Mataifa ulimaliza mwaka 2025 ukiwa na kiwango cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa cha dola bilioni 1.6 za Marekani za michango ambayo haikulipwa.
Kwa ujumla, madeni ya michango katika bajeti ya kawaida, operesheni za kulinda amani na mahakama mbili za kimataifa yanazidi dola bilioni 6.5 za Marekani.
Mwanzoni mwa mwaka huu, Umoja wa Mataifa ulianza kutekeleza hatua kali za kuhifadhi fedha taslimu ili kupunguza na kudhibiti kasi ya matumizi.
“Katibu Mkuu amezitaka nchi wanachama kutekeleza wajibu wao wa kulipa michango yao kwa ukamilifu na kwa wakati, au kufanya mageuzi makubwa ya kanuni za kifedha za Umoja wa Mataifa ili kuzuia mfumo huo usikabiliwe na hatari ya kuporomoka,” ripoti hiyo ilisema.
Kanuni zilizokuwa zinazuia utendaji
Hadi Jumanne usiku, kanuni za kifedha zilizowekwa miaka 80 iliyopita zilikuwa zinahitaji Umoja wa Mataifa kurejesha kwa nchi wanachama fedha zote ambazo hazikutumika kama salio litakalokatwa kwenye michango yao ya baadaye.
Kanuni hiyo ilitumika hata pale ambapo fedha hazikutumika kwa sababu michango ilichelewa kufika au haikuwahi kupokelewa kabisa.
Rais wa UNGA80 aliwasilisha hoja hii mbele ya bunge la EU
Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Annalena Baerbock, alizungumzia suala hilo katika hotuba yake kwa Bunge la Ulaya mwezi Februari.
Akizungumzia “mgogoro mkubwa unaotishia uwepo wa Umoja wa Mataifa kutokana na uhaba wa ukwasi,” aliwahimiza mataifa ya Ulaya “kuwasilisha mapendekezo ya kufanyia mageuzi kanuni hii ya kifedha ya Kafkia inayolazimisha kurejesha fedha ambazo hazikuwahi kupokelewa.”
Kauli ya Baerbock baada ya azimio kupitishwa
Kupitia taarifa yake ya leo baada ya kupitishwa kwa azimio, Baerbock amesema, “kwa azimio hili la kihistoria, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limezuia hatari ya kuporomoka kwa kifedha iliyokuwa ikilikabili Umoja wa Mataifa na kufanya mageuzi ya kanuni ya kifedha iliyopitwa na wakati ya takriban miaka 75, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikidhoofisha uthabiti wa kifedha wa Shirika hilo.”
Amesema uamuzi huo pia unatuma ujumbe mpana kwamba, hata katika nyakati za mgawanyiko, nchi wanachama wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa zinaweza kuungana na kuchukua hatua madhubuti.