DAR ES SALAAM: SERIKALI imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuvutia wawekezaji zaidi kutoka Poland, huku sekta binafsi ikiendelea kuwa mhimili wa ukuaji wa uchumi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Poland jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Fredy Msemwa, amesema Serikali inaendelea kutekeleza mageuzi yatakayorahisisha mazingira ya biashara, kuimarisha uthabiti wa sera na kupanua miundombinu muhimu kwa ajili ya biashara na uwekezaji.
Amesema Tanzania inakamilisha mapitio ya mazingira ya biashara ili kuongeza ushindani wa nchi katika kuvutia uwekezaji, huku ikiendelea kuwekeza katika sekta za umeme, barabara, reli na usafiri wa anga.
Msemwa amesema uwezo wa uzalishaji wa umeme unatarajiwa kuongezeka kutoka megawati 4,000 hadi 8,000 katika kipindi cha miaka mitano ijayo ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kujenga uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050.
Aidha, amesema uwekezaji wa Poland nchini Tanzania kwa sasa unakadiriwa kufikia dola za Marekani milioni 21.7, huku akieleza matarajio ya kuongezeka kwa uwekezaji huo katika sekta za viwanda, kilimo, uchakataji wa mazao, teknolojia ya kidijitali, madini, usafirishaji na uongezaji thamani wa bidhaa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TISEZA, Balozi Aziz Mlima, amewataka wawekezaji wa Poland kutumia fursa zilizopo nchini, akisema Tanzania ina mazingira mazuri ya uwekezaji na nafasi ya kimkakati ya kuhudumia soko la Afrika Mashariki na Bara la Afrika.
