
HAKUNA ushindi usiokuwa na kilio. Hiyo ndiyo hali ya mashabiki wa Yanga wakishangilia ubingwa wao wa ligi lakini wakikumbuka tukio la kuumia kwa kiungo wao Pacome Zouzoua wanabadilika ghafla, sasa kiungo huyo ameshafanyiwa upasuaji wa eneo aliloumia.
Akizungumza na Mwanaspoti Meneja wa Habari wa Yanga, Ally Kamwe alisema Pacome baada ya kufikishwa hospitali ya Aga Khan jana, akatakiwa kufanyiwa upasuaji wa haraka kutokana na ushauri wa madaktari.
Kamwe alisema Pacome alifanyiwa upasuaji huo uliokamilika saa nane usiku, ukifanyika kwa mafanikio ambapo sasa atakuwa nje kwa wiki sita.
“Pacome baada ya kuumia jana (juzi) alipelekwa moja kwa moja hospitali ya Aga Khan, kwa sababu ya jeraha lake kuwa baya kama ambavyo mliliona, akapekwa moja kwa moja chumba cha dharura,jopo la madaktari wa pale Aga Khan wakiahirikiana na madaktari wa klabu wakakubaliana jeraha lile halitakiwi kucheleweshwa kupatiwa matibabu,”alisema Kamwe.
“Baada ya majadiliano na uongozi ukatoa baraka zake,tukakubaliana afanyiwe upasuaji huo ambao ukifanyika jana (juzi), tunamshukuru Mungu usiku huo wa saa nane upasuaji huo ukawa umekamilika kwa mafanikio ya asilimia mia moja.
“Kwa mujibu wa ripoti ya madaktari kitakuwa na wiki sita za kumuangalia baada ya upasuaji huo ukiwa ni uangalizi wa awali na baada ya hapo tutakuja kuwapa taarifa sasa kwamba Pacome atakuwa nje kwa muda gani.”
ALIYEMUUMIZA HUYU HAPA
Jana kiungo wa JKT Tanzania, Hassan Wahabi alimtembelea Pacome hospitalini nakwenda kumjulia hali baada ya tukio hilo la dakika 45 kwenye mchezo huo ambao wa juzi ambao Yanga ilishinda kwa mabao 3-0.
Wahabi ambaye aliongozana na Msemaji wa JKT, Masau Bwire alisema, hakuweza kuwa sawa usiku mzima baada ya tukio hilo ambapo aliwaomba viongozi wa klabu yake kuhakikisha anafika hospitali na kumjulia hali Pacome kufuatia tukio hilo
Wahabi alisema hakudhamiria kumuumiza Pacome kwenye tukio hilo ambapo alikwenda kwa nia ya kutaka kuondooa mpira kwenye umiliki wake lakini bahati mbaya ikatokea tukio hilo baya.
“Mimi sijawahi kukusudia kumuumiza mchezaji mwenzangu, inatokea tunapata maumivu kwenye mchezo wa soka, lakini hili linakuwa tukio kubwa na baya kwenye maisha yangu, najutia hata kwanini niliamua kutaka kumpokonya mpira kwa njia ile, nikikumbuka naumia moyoni,”alisema Wahabi.
“Niliwaomba viongozi wanipeleke kwake nikamuone na nimuombe radhi, nitamuombea sana apone haraka, nitafurahi na moyo wangu utakuwa wenye amani nikimuona anarudi kuendelea na kazi yake, nawaomba radhi viongozi wa klabu yake, mashabiki wote kwa tukio hili.
IBENGE AMFUATA
Mbali na Wahabi makocha wa Azam Florent Ibenge na wasaidizi wake wakiungana na kiungo wa Yanga, Maxi Nzengeli nao wakifika hospitalini hapo kwa ajili ya kumpa pole kiungo huyo.