
Taswira inaendelea kuonesha jinsi barabara hiyo ilivyoharibika kwa kiwango kikubwa baada ya vita na mahema yaliyosongamana pande zote mbili za njia, huku Saeed akijaribu kufika kwenye mabaki ya nyumba yake yenye kuta zilizomomonyoka.
Wakiwasili nyumbani hapo, Muayyad anapambana kuvuta kitimwendo ili kupita rundo la vifusi vilivyoziba njia, kisha Saeed anaegemea mabega ya mwanae ili kupanda ngazi zenye nyufa hatari kuelekea ghorofa ya pili. Akiwa ameketi kwenye kiti chake chakavu kilichoshika kutu, Saeed kwa masikitiko anasema.
“Kabla ya vita, niliishi mahali hapa kwa amani ya fikra na usalama. Niliweza kutembea kwenye kitimwendo hiki kwa urahisi na kwa utulivu kwa sababu kuta zilikuwa zikinilinda na kunisafirisha. Lakini baada ya vita, kama unavyoona, kuta zimeporomoka, na ugumu wa kutembea umejidhihirisha, hakika, naushuhudia ugumu huo kiukweli. Sikuwa na njia mbadala ya nyumba hii isipokuwa hema, na hema, kama unavyojua, si salama zaidi kuliko nyumba, na kukodisha nyumba nyingine ni gharama kubwa sana, ambayo iko nje ya uwezo wangu.”
Kamera inamwonesha Saeed akisoma Kitabu Kitukufu cha Qur’ani kilichoandikwa kwa maandishi ya nukta nundu ambayo ni maalum ya watu wasioona, huku kwa nje kupitia madirisha yaliyovunjika yakionekana mahema na nyumba zilizobomolewa zilizozunguka makazi yake.
Hali ya Saeed inaonesha upande usioonekana kwa urahisi wa janga la kibinadamu huko Gaza, unaohusu maisha ya watu wenye ulemavu wa kuona, viziwi, au ulemavu zaidi ya mmoja wakati huu wa uharibifu mkubwa na kuporomoka kwa huduma za afya. Mashirika ya Umoja wa Mataifa yameeleza kuwa vita vimeongeza hatari kwa kundi hili ambalo haliwezi kusikia amri za kuhama au kuona njia wakati hali ya hatari ikibadilika ghafla. Saeed anakumbuka kazi aliyokuwa nayo kabla ya vita vya sasa vilivyoanza Oktoba 7, 2023.
“Kabla ya vita, nilikuwa mtangazaji katika kituo cha redio cha hapa Gaza. Niliweza kwenda na kurudi kituoni kwa urahisi kwa sababu barabara ilikuwa inapitika. Lakini sasa, baada ya vita, barabara hazina lami, na nyumba, kama unavyoona, iko katika hatari ya kuporomoka.”
Mzee Saeed anaonekana akifungua kurasa za kitabu chenye maandishi ya nukta nundu. Kusoma, kwake sio mchezo wa kupitisha muda tu, bali ni nafasi ya kiroho ya kumsaidia kuhimili maisha, ingawa moto uliounguza nyumba yake umemwachia vitabu viwili pekee.
“Kitabu hiki mkononi mwangu, pamoja na kitabu kingine kilichochapishwa kwa njia ya kawaida inayotumiwa na watu wanaoona, ndivyo vitabu viwili pekee vilivyookoka kwenye moto ulioteketeza nyumba yangu wakati wa mashambulizi. Ndiyo maana sasa ninahisi upweke na uchovu mkubwa, baada ya kupoteza kitu kilichonipa furaha yangu muhimu na kitu nilichotumia muda wangu mwingi kukifanya; kusoma.”
Nats…
Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani, WHO, linakadiria kuwa hadi watu 43,000 kati ya 172,000 waliojeruhiwa Gaza tangu Oktoba 2023 wamepata majeraha yaliyobadili kabisa mfumo wa maisha yao, huku robo yao wakiwa ni watoto.
Licha ya mahitaji hayo makubwa, huduma za utengamao zimebaki kuwa duni sana, huku kukiwa hakuna kituo hata kimoja kinachofanya kazi kikamilifu, na zaidi ya wagonjwa 400 wapo kwenye orodha ya kusubiri vitanda vya matibabu hayo maalum.
Wakati huohuo, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Dharura, OCHA, inaeleza kuwa mashambulizi ya mabomu na risasi yanaendelea kuumiza raia katika Ukanda mzima wa Gaza, huku maeneo ya wakimbizi yakiwa katika hali mbaya sana kukiwa na ukosefu wa mwanga, nishati, na maji safi.
Kwa Saeed, changamoto kubwa zaidi ni usalama na jinsi ya kujiokoa dharura inapotokea.
“Wasiwasi pekee ni kupata mahali salama, kwa sababu mahali hapa pameporomoka. Kwa mfano, mashambulizi yanapotokea, mtu asiye na ulemavu anaweza kuondoka kwa urahisi na kuhama kutoka sehemu moja hadi nyingine. Lakini hali yangu ya afya hainiruhusu kufanya hivyo.”
Ikiwa ni siku chache baada ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Watu Wasioona na viziwi inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 27 Juni, hali ya Gaza inabaki kuwa mfano halisi wa changamoto wanazopitia walemavu.
Video za mwisho zinaonesha taswira ya jumla ya mtaa anaoshi Saeed ukiwa umejaa vifusi na mahema, huku mzee huyu akionekana kwa mbali ndani ya mabaki ya nyumba yake akiendelea kushika kitabu chake cha maandishi ya nukta nundu, kilichonusurika kwenye moto, akitafuta hifadhi salama na huduma za msingi zitakazomwezesha japo kuishi.