
Taarifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, (WHO) Kanda ya Afrika iliyotolewa Kigali, Rwanda na Nairobi Kenya inasema mafanikio hayo, yaliyopatikana kupitia Mfumo wa Kimataifa wa Ufuatiliaji wa Usugu wa Vimelea dhidi ya Dawa na Matumizi ya Dawa (GLASS) wa WHO, yanaashiria hatua muhimu katika kuboresha matibabu yanayotegemea ushahidi, usimamizi bora wa matumizi ya dawa za kuua vijidudu na utoaji wa maamuzi ya afya ya umma.
Usugu wa vimelea dhidi ya dawa ni nini?
Usugu wa vimelea dhidi ya dawa hutokea pale bakteria, virusi, fangasi na vimelea vingine vinapobadilika na kuwa sugu kwa dawa zinazokusudiwa kuviangamiza, hali inayofanya maambukizi kuwa magumu kutibika na kuongeza hatari ya magonjwa makali, vifo pamoja na gharama za huduma za afya.
Kenya imefanya nini?
Kenya imejenga moja ya mifumo mikubwa zaidi barani Afrika ya ufuatiliaji wa usugu wa vimelea dhidi ya dawa kupitia uwekezaji endelevu uliodumu kwa karibu muongo mmoja.
Mafanikio makuu
- Imepanua vituo vya ufuatiliaji kutoka vituo viwili vya majaribio mwaka 2017 hadi kufikia vituo 32 vya ufuatiliaji katika kaunti 27, vikihusisha sekta mbalimbali za mfumo wa One Health.
- Imeanzisha mtandao wa kitaifa unaounganisha maabara, hospitali na taasisi za afya ya umma.
- Imeimarisha miundombinu ya maabara na uwezo wa uchunguzi wa magonjwa.
- Imeboresha mifumo ya usimamizi wa takwimu na kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya kuhusu ufuatiliaji wa AMR.
- Imeanzisha zana sanifu za ukusanyaji wa takwimu pamoja na mifumo ya taarifa za maabara.
- Imeweka utaratibu wa ukaguzi wa ubora wa takwimu pamoja na ushirikiano wa wataalamu wa maabara, wataalamu wa magonjwa ya mlipuko na wataalamu wa mifumo ya taarifa.
- Mwaka 2025 ilihama kutoka kuripoti takwimu za jumla kwenda kuripoti taarifa za kila mgonjwa mmoja mmoja kupitia mfumo wa WHO GLASS, jambo lililoruhusu uchambuzi wa kina zaidi wa mwenendo wa usugu wa vimelea.
- Imeunganisha takwimu za ufuatiliaji wa AMR, matumizi ya dawa za kuua vijidudu na matumizi halisi ya dawa kupitia Kituo Kikuu cha Kitaifa cha Takwimu (Central Data Warehouse).
- Imekusanya zaidi ya rekodi 100,000 za ufuatiliaji wa AMR kati ya mwaka 2021 na 2025.
- Imewasilisha rekodi 9,039 za wagonjwa mmoja mmoja kwenye mfumo wa WHO GLASS mwaka 2025.
Rwanda imefanya nini?
Rwanda imeimarisha mfumo wake wa ufuatiliaji kupitia ushirikiano madhubuti wa taasisi mbalimbali na kuboresha hatua kwa hatua uwezo wa kuripoti taarifa.
Mafanikio makuu
- Ilijiunga na mfumo wa WHO GLASS mwaka 2022.
- Iliwasilisha taarifa zake za kwanza za ufuatiliaji wa AMR mwaka 2023.
- Ilianza kuripoti kwa pamoja takwimu za jumla na taarifa za kila mgonjwa mmoja mmoja katika mzunguko wa taarifa wa mwaka 2025.
- Imeimarisha ufuatiliaji kwa kutumia taarifa kutoka hospitali nne kuu za rufaa:
- Hospitali ya Kufundishia ya Chuo Kikuu Kigali
- Hospitali ya Kufundishia ya Chuo Kikuu Butare
- Hospitali ya King Faisal
- Hospitali ya Jeshi la Rwanda
Kwa nini taarifa za kila mgonjwa mmoja mmoja ni muhimu?
Hapo awali, nchi nyingi zilikuwa zinawasilisha takwimu za jumla za kitaifa pekee.
Kuripoti taarifa za kila mgonjwa mmoja mmoja kunatoa taarifa za kina zaidi zinazowezesha mamlaka za afya:
- Kubaini maeneo yanakoibuka maambukizi sugu kwa dawa.
- Kugundua milipuko ya magonjwa kwa haraka zaidi.
- Kufuatilia mwenendo wa usugu kulingana na mgonjwa, hospitali na eneo husika.
- Kuboresha miongozo ya matibabu.
- Kusaidia matumizi sahihi ya dawa za antibiotiki.
- Kuimarisha programu za usimamizi wa matumizi bora ya dawa za kuua vijidudu.
- Kuzalisha ushahidi imara wa kutunga sera za afya.
Fursa za baadaye
Maboresho haya yanaweka msingi kwa Kenya na Rwanda kuimarisha zaidi mapambano dhidi ya AMR katika miaka ijayo.
Changamoto
Licha ya mafanikio hayo, nchi zote mbili zilikumbana na changamoto wakati wa utekelezaji.
Kenya
- Kutokuwepo kwa muunganiko mzuri kati ya mifumo mbalimbali ya taarifa za maabara.
- Kukosekana kwa baadhi ya taarifa za wagonjwa katika baadhi ya rekodi.
- Uhitaji wa wataalamu zaidi wa kuhakiki na kuthibitisha ubora wa takwimu.
- Wasiwasi wa awali kuhusu faragha na usiri wa taarifa za wagonjwa.
Rwanda
- Uhaba wa rasilimali watu kwa ajili ya usimamizi wa takwimu.
- Kutokuwepo kwa muunganiko mzuri kati ya mifumo ya taarifa ya hospitali mbalimbali.
Mapendekezo
Ili kuendeleza mafanikio yaliyopatikana, wataalamu wanashauri mambo kadhaa ikiwemo kupanua mfumo wa ufuatiliaji hadi hospitali, kaunti na vituo zaidi vya afya ngazi ya jamii na Kuboresha muunganiko kati ya mifumo ya taarifa za maabara na hospitali.