Akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani, kutoka jimbo la La Guaira, moja ya maeneo yaliyoathiriwa vibaya zaidi na matetemeko hayo, Mkurugenzi wa WFP nchini Venezuela, Stephanie Hochstetter, ameeleza kuwa hali ya kibinadamu sasa inabadilika kutoka operesheni za uokoaji wa dharura kwenda katika juhudi za muda mrefu za kutoa misaada na kuwasaidia manusura kurejea katika maisha yao.

Ukubwa wa mateso ya kibinadamu unaendelea kujitokeza wazi.

Hochstetter amesimulia kukutana na baba mmoja aliyekuwa amewakumbatia watoto wake watatu wa kiume wenye umri wa miaka miwili, minne na mitano baada ya nyumba yao kuharibiwa. 

“Familia hiyo haikuwa na chakula, maji wala makazi. Wakati huo huo, mama wa watoto hao alikuwa amelazwa hospitalini Caracas, mji mkuu wa Venezuela, huku familia hiyo ikiwa imepoteza ndugu na majirani kutokana na janga hilo,” amesema Mkuu huyo wa WFP nchini Venezuela.

“Mahitaji ya chakula, maji safi, makazi na huduma muhimu ni ya haraka na ya dharura,” amesema afisa huyo akiwa katika kituo cha kwanza cha WFP cha usambazaji wa chakula kilichoanzishwa katika kituo cha muda cha huduma jumuishi kinachounga mkono juhudi za serikali.

Msaada uliotolewa na WFP hadi sasa

WFP tayari imetoa msaada wa chakula cha dharura kwa zaidi ya watu 1,200 ndani ya siku chache tangu kutokea kwa maafa hayo, na inalenga kuwafikia hadi watu 500,000 katika kipindi cha miezi mitatu ijayo. 

Shirika hilo lina zaidi ya tani za ujazo 3,000 za chakula nchini Venezuela—zinazotosha kulisha zaidi ya familia 10,000 kwa miezi miwili—na linaendelea kununua bidhaa nyingine za ziada. Pia, vifaa vya misaada vilivyohifadhiwa katika vituo vya kikanda vya kibinadamu viko tayari kusafirishwa endapo vitahitajika.

Bado kuna miundombinu inayofanya kazi

Licha ya kiwango kikubwa cha uharibifu, miundombinu muhimu ya usafirishaji bado inaendelea kufanya kazi. Bandari za Puerto Cabello na La Guaira zinaendelea kupokea mizigo, hivyo kuruhusu misaada ya kibinadamu kuingia nchini, huku safari za ndege za kibinadamu kwenda Caracas zikiendelea licha ya kusimamishwa kwa safari za kawaida za kibiashara.

Kwa mujibu wa Hochstetter, changamoto kubwa kwa sasa ni kuwafikia haraka wananchi walioathirika huku tathmini ikiendelea kubaini ukubwa halisi wa uharibifu na mahitaji yaliyopo. 

Ingawa rasilimali kwa sasa zinatosha mahitaji yataongezeka

Vituo vya huduma jumuishi vinatoa chakula, huduma za afya, msaada wa kisaikolojia, maji safi, umeme, mawasiliano na makazi ya muda, lakini mashirika ya kibinadamu yanaonya kuwa mahitaji yataendelea kuongezeka kadri tathmini zinavyoendelea katika maeneo zaidi.

WFP imeonya kuwa ingawa ina rasilimali za kutosha kuanza mwitikio wa haraka wa dharura, akiba iliyopo haitatosheleza mahitaji yote ya kibinadamu. 

Shirika hilo linaomba dola za Marekani milioni 50 kama msaada wa awali ili kutoa huduma za kuokoa maisha kwa hadi watu nusu milioni katika kipindi cha miezi mitatu ijayo, pamoja na kufadhili shughuli za usafirishaji wa misaada na huduma za mawasiliano ya dharura.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *