NYOTA wa Yanga, Allan Okello, Pacome Zouzoua na wenzao wataoga mamilioni baada ya uongozi wa klabu hiyo kutoa bonasi ya Sh700 milioni kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu NBC.
Siku moja tu baada ya Yanga kuchukua ubingwa wa ligi, mabosi wa klabu hiyo wamefanya uamuzi wa kuwahisha kutoa bonasi ya ubingwa huo kwa wachezaji.
Wakati wowote kuanzia leo unaposoma habari hii basi wachezaji wa Yanga watapokea bonasi ya Sh700 milioni ya ubingwa wa ligi waliyoahidiwa na mdhamini wa klabu hiyo, Ghalib Said Mohammed ‘GSM’ ambayo katika mechi saba zilizopita ilikuwa kila ushindi una thamani ya Sh100 milioni.
Baada ya Yanga kupoteza mchezo dhidi ya Dodoma Jiji kwa mabao 3-2, kabla ya timu hiyo kucheza mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya JKT ikishinda kwa mabao 2-0, tajiri huyo aliwapa ahadi hiyo wachezaji ili kuwahamasisha wasiendelee kuangusha pointi.
Tangu alipotoka ahadi hiyo, Yanga imeshinda mechi zake saba za ligi, ikizifunga Singida Black Stars, Namungo, Mashujaa, Fountain Gate, Azam FC, TRA United na juzi wakamaliza na JKT ikijihakikishia ubingwa huo wa tano mfululizo. Yanga kwa kutwaa ubingwa imepata fedha za ubingwa Sh750 milioni kati ya hizo Sh650 milioni zinatoka AzamTV huku Sh100 milioni zikitoka kwa wadhamini wa ligi Benki ya NBC.
Mbali ya fedha hizo Yanga kwa kutwaa ubingwa huo wanapata bonasi ya Sh262.5 milioni kutoka kwa wadhamini wao Sportpesa ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya mkataba wa Sh21.7 bilioni.
PANGA LINAFUATA
Baada ya kutoka kwa bonasi hiyo kinachofuata kwa Yanga ni mchakato wa kukiboresha kikosi hicho kwa wachezaji wengi kwa kuachwa ili kupisha wengine wapya.
Yanga inataka kumalizana na wachezaji wake ambao msimu huu wamepoteza ubora wao na kuifanya timu hiyo kupitia kipindi kigumu.
Yanga inapiga hesabu za kuwaacha wachezaji 11 waliomaliza msimu na timu hiyo ambapo ndani ya hao kuna wakigeni wanne wakati wazawa saba huku wakigoma kuweka wazi majina yao kamili, ikitaka kwanza kumalizana nao.
“Tutaondoa wachezaji wengi tuseme ukweli, huu ni msimu ambao kila mmoja aliteseka kwa mawazo jambo ambalo tunashukuru ni tumemaliza salama kwa kuchukua baadhi ya mataji na mengine tukiangusha,” alisema bosi huyo.
“Tutamalizana na wachezaji wote haraka kuwalipa bonasi zao ili sasa tubaki na kazi ya kutengeneza timu kwa msimu ujao, tunaweza kuwaacha wachezaji mpaka 11 kwenye hiki kikosi ambacho tumemaliza nacho ligi jana (juzi).
Ukiacha wachezaji hao Yanga pia itaachana na wachezaji wote watano ambao wako nje kwa mkopo kutokana na viwango vyao kutoonyesha kubadilika huku hata klabu ambazo wamekwenda zikigoma kutaka kuendelea nao.
“Huko kwa wachezaji ambao wako nje kwa mkopo nadhani nyie wenyewe mnaweza kuona kuna anayestahili kurudi hapa tena? Hapana hakuna ambacho umekisikia au kuona kama kuna mmoja wao anafanya vizuri, hao nao watatupisha, tunakwenda kujenga timu kweli hakuna muda wa kupoteza.”