PWANI: Mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma wenye urefu wa kilometa 345 umefikia asilimia 89 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika ifikapo Agosti 21, 2026.
Kukamilika kwa mradi huo kutaimarisha uwezo wa kusafirisha umeme, kuongeza uthabiti wa Gridi ya Taifa na kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini.
Akikagua maendeleo ya mradi huo Julai 1, 2026, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi amesema mradi huo ni sehemu ya uwekezaji mkubwa wa kimkakati wa Serikali unaolenga kuimarisha miundombinu ya usafirishaji wa umeme ili kukidhi ongezeko la mahitaji ya nishati nchini na kuifanya Gridi ya Taifa kuwa imara zaidi.
Ndejembi amesema njia hiyo ya umeme ina umuhimu wa kipekee kwa kuwa itawezesha usafirishaji wa umeme unaozalishwa na Kituo cha Kufua Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP) chenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 kwenda katika maeneo mbalimbali ya nchi, hivyo kuongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme kwa wananchi na sekta za uzalishaji.

“Serikali imeona mahitaji ya umeme nchini yanaendelea kuongezeka kutokana na ukuaji wa uchumi na ongezeko la wateja. Ujenzi wa njia hii ni muhimu kwa sababu utaongeza uwezo wa kusafirisha umeme na kuimarisha uthabiti wa Gridi ya Taifa,” amesema Ndejembi.
Aidha, amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika miradi ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme ili kuhakikisha Watanzania wanaendelea kupata huduma ya umeme wa uhakika inayochochea maendeleo ya viwanda, biashara na uchumi kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Razalo Twange, amesema uwekezaji unaoendelea katika miundombinu ya umeme umewezesha Shirika kuongeza kwa kiasi kikubwa huduma kwa wananchi. Amesema katika mwaka wa fedha 2025/26, TANESCO imeandika historia kwa kuwaunganishia umeme zaidi ya wateja 800,000, idadi ambayo haijawahi kufikiwa tangu Tanzania ipate uhuru.
“Historia hii inaonesha wazi kuwa mahitaji ya umeme yanaongezeka kwa kasi, ndiyo maana tunaendelea kuwekeza katika miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme ili kuendana na ukuaji huo,” amesema Bw. Twange.