BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC), mdhamini mkuu wa Ligi ya NBC kwa vijana chini ya miaka 20 (NBC U20 Youth League), imekabidhi kombe la ubingwa wa msimu wa 2025-2026 kwa Azam U-20 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Yanga U-20 katika mchezo wa fainali uliochezwa jana Jumatano kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Kabla ya mchezo huo wa fainali, Mbeya City U-20 ilitwaa nafasi ya tatu baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-2 kwa mikwaju ya penalti dhidi ya JKT Tanzania U-20, kufuatia timu hizo kutoka sare katika muda wa kawaida.
Hafla ya kukabidhi kombe hilo iliongozwa na Mkuu wa Kitengo cha Wajasiriamali, Vijana na Wanawake wa Benki ya NBC, Gaudence Shawa, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Theobald Sabi.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa soka nchini akiwemo Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Nassor Idrissa, Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Oscar Milambo, Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Lameck Nyambaya, viongozi wengine wa TFF na Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa, Taifa Stars, Miguel Gamondi.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Shawa aliwapongeza mabingwa Azam U-20, walioshika nafasi ya pili, Yanga U-20, waliomaliza nafasi ya tatu, Mbeya City U-20, klabu zote zilizoshiriki na TFF kwa kufanikisha msimu ulioonyesha kiwango cha juu cha ushindani na maendeleo makubwa ya kiufundi.
Amesema ubora wa michezo ulioshuhudiwa msimu huu unaonesha wazi kuwa uwekezaji katika maendeleo ya soka la vijana unaanza kuzaa matokeo yanayotarajiwa, huku ukitoa matumaini makubwa ya kuimarika zaidi kwa ligi za ndani na timu za taifa katika miaka ijayo.
“NBC tunaamini kwamba mafanikio ya soka la kulipwa huanzia kwenye uwekezaji madhubuti katika maendeleo ya vijana. Ndiyo sababu tuliamua kuwa sehemu ya safari hii ya kujenga kizazi kipya cha wachezaji wenye uwezo wa kuleta ushindani mkubwa katika Ligi Kuu ya NBC, NBC Championship na hatimaye kuiwezesha Tanzania kuwa na timu za taifa zenye ushindani wa kimataifa.
“Tunafurahishwa kuona kiwango cha ushindani na ubora wa soka katika ligi hii vinaendelea kuimarika kila msimu, jambo linalotupa imani kuwa uwekezaji huu unaendelea kuleta matokeo chanya,” amesema Shawa.
Ameongeza kuwa, kupitia udhamini wake wa Ligi Kuu ya NBC, NBC Championship na NBC U20 Youth League, benki hiyo itaendelea kushirikiana na TFF na wadau wengine wa mchezo huo katika kuimarisha mfumo wa ukuzaji vipaji, kuongeza ushindani wa ligi, kuinua hadhi ya soka la Tanzania na kuchochea ukuaji wa uchumi wa sekta ya michezo kupitia ajira na fursa mbalimbali zinazotokana na mchezo huo.
“Soka limekuwa sekta muhimu ya kiuchumi inayogusa maelfu ya Watanzania. Ndiyo maana tunaendelea kuwekeza si tu katika mashindano, bali pia katika kujenga mfumo endelevu wa kuzalisha vipaji na kuongeza thamani ya mchezo huu kwa manufaa ya wachezaji, makocha, klabu, mashabiki na taifa kwa ujumla,” ameongeza.
Mwenyekiti wa DRFA, Lameck Nyambaya, aliipongeza NBC kwa kuendelea kuwa mshirika muhimu wa maendeleo ya soka nchini kupitia uwekezaji wake katika ligi za vijana.
Amesema mashindano ya msimu huu yameonesha mabadiliko makubwa katika ubora wa kiufundi, nidhamu ya mchezo na ushindani miongoni mwa timu zilizoshiriki.