RAIS wa Shirikisho la Mchezo wa Kabaddi Zanzibar, Abdalla Juma ametangaza majina ya wachezaji 18 watakaounda Timu ya Taifa ya wanaume kwa mwaka 2026, itakayoiwakilisha Zanzibar katika Mashindano ya Afrika yatakayofanyika visiwani humo Agosti 1 hadi 14 mwaka huu.

Akizungumza wakati wa kutangaza kikosi hicho, Juma amesema timu hiyo imeundwa na wachezaji kutoka klabu mbalimbali za Kabaddi nchini ikiwemo Nyuki, JKU, Fighter, VTA na KMKM na kulezea matumaini ya timu kufanya vizuri katika mashindano hayo.

Wachezaji waliotajwa ni Ali Bakari Ali, Mbarouk Mikidadi Sanganya, Rashid Ali Abdallah, Yakoub Talib Salum na Samir Mbaraka Sururu kutoka Nyuki. Wengine ni Saleh Khamis Ramadhan na Juma Said Jafar kutoka JKU, Muhidini Khamis, Mundhir Salum Mohammed na Othman Khalid Bakar kutoka Fighter.

Pia kuna Paul Khamis Ishari na Maganga Khamis Lunda kutoka VTA, sambamba na Ibrahimu Yunuss Juma, Hafidh Ali Hamad, Dau Daula Shehe, Ashrafu Nassor Mohammed, Khatib Hajji Mussa na Abdul Rahman Hamad Said kutoka KMKM.

Mashindano hayo ya Afrika yanatarajiwa kuwa muhimu kwa timu shiriki kwani yatatumika kutafuta timu zitakazofuzu Kombe la Dunia la Kabaddi  litakalofanyika hapa nchini, Desemba mwaka huu.

Rais huyo amewataka wachezaji waliochaguliwa kuanza maandalizi mapema na kuzingatia nidhamu, ushirikiano na kujituma ili kuhakikisha Zanzibar inapata matokeo mazuri katika mashindano hayo ya kimataifa.

Timu hiyo itakuwa ikifanya mazoezi katika viwanja vitatu tofauti ambavyo shirikisho imevichagua ambavyo ni Magogoni, Lumumba na Migombani wakati wa asubuhi na jioni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *