
KOCHA Mkuu wa Simba Queens, Mussa Hassan ‘Mgosi’ amesema amebaini kuna maeneo yanayohitaji kuimarishwa kabla ya timu hiyo kuanza safari ya kuwania tiketi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kupitia michuano ya kufuzu ya ukanda wa CECAFA.
Michuano hiyo ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika ukanda wa CECAFA kwa mwaka huu imepangwa kufanyika Rwanda kuanzia Agosti 22 hadi Septemba 6, huku Simba Queens ikiiwakilisha Tanzania baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mgosi amesema kwa sasa wachezaji wako kwenye mapumziko ya mwezi mmoja na timu itarejea kambini Julai 19 kujiandaa na michuano hiyo.
“Wachezaji bado wapo likizo, tuliwapa mapumziko ya mwezi mmoja kuanzia Juni 12 hadi Julai 19, kisha tutaanza maandalizi rasmi kwa ajili ya mashindano ya CECAFA,” amesema Mgosi.
Ameongeza, tathmini ya kiufundi iliyofanyika baada ya msimu kumalizika inaonyesha kuna nafasi zinazohitaji kuongezewa nguvu ili kuongeza ushindani wa kikosi hicho.
“Tumeona yapo maeneo ya kufanyia kazi upande wa kiufundi. Tunahitaji kuongeza mabeki wawili, kiungo mmoja na eneo la ushambuliaji. Kwa sasa hatuwezi kuweka wazi majina, lakini baadhi ya wachezaji tumeshakamilisha mazungumzo nao,” amesema.
Hii ni mara ya tatu Simba inacheza michuano hiyo, awali ilikuwa mwaka 2022 ilipobeba taji hilo. Mwaka 2024 ikashiriki tena na kuishia hatua ya makundi huku C.B.E ya Ethiopia ikiibuka na taji hilo.
Mbali na Simba, JKT Queens imewahi kucheza mashindano hayo ikibeba ubingwa mara mbili, mwaka 2023 na mwaka 2025.
Bingwa wa michuano ya CECAFA atakata tiketi ya kuuwakilisha ukanda huo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake.