
Wakati wa uzinduzi wa muhtasari wa kwanza wa kina kuhusu historia ya misheni hizi, Rosemary DiCarlo, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Kisiasa na Ujenzi wa Amani, anaelezea rekodi yao imekuwa “wakati mwingine ya kawaida, wakati mwingine ya kihistoria,” lakini imebeba ukweli mmoja usiobadilika, “Diplomasia inafanya kazi.” Anasisitiza kuwa funzo hilo lina umuhimu mkubwa hasa katika nyakati za sasa.
Kwa mujibu wa chapisho hilo, lililoandaliwa na Idara ya Masuala ya Kisiasa na Ujenzi wa Amani ya Umoja wa Mataifa, linaangazia kipindi cha kuanzia mwaka 1948 hadi 2025, likifafanua namna jukumu la kisiasa la Umoja wa Mataifa lilivyobadilika sambamba na mabadiliko ya mazingira ya kimataifa.
Kuanzia Palestina hadi leo
Misheni ya kwanza maalum ya kisiasa ilianzishwa muda mfupi baada ya kuundwa kwa Umoja wa Mataifa. Mwezi Mei 1948, Baraza Kuu lilimteua mwanadiplomasia wa Sweden, Count Folke Bernadotte, kuwa mpatanishi wa Umoja wa Mataifa nchini Palestina. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Umoja wa Mataifa kumtuma mjumbe maalum kusaidia kutatua mgogoro wa kivita.
Leo, misheni maalum za kisiasa hutekeleza majukumu mbalimbali ya kiraia yenye lengo la kuzuia migogoro, kusaidia michakato ya amani na kujenga amani endelevu. Baadhi huwezesha mazungumzo ya amani, nyingine hufuatilia utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano, kusaidia uwekaji wa mipaka, kuchunguza ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu au kuunga mkono mageuzi ya kisiasa.
Kwa mujibu wa DiCarlo, sifa kuu ya misheni hizi ni unyumbufu wake. Anasema historia yake “inaakisi historia ya Umoja wa Mataifa wenyewe,” kwa kuwa imekuwa ikibadilika kulingana na changamoto za kila enzi.
“Zimekuwa katika sura mbalimbali, ikiwemo wajumbe maalum wa Katibu Mkuu, misheni za uchunguzi na kutafuta ukweli, ofisi za kikanda, paneli za wataalamu zinazosaidia Baraza la Usalama kufuatilia utekelezaji wa vikwazo, na misheni zinazosaidia nchi kupitia mageuzi magumu ya kisiasa,” anaeleza DiCarlo.
Anaongeza kuwa misheni hizo zinaweza kuanzishwa na Baraza Kuu au Baraza la Usalama, huku zikiweza kufanya kazi katika ngazi ya kitaifa, kikanda au kimataifa, “unyumbufu ndiyo nguvu yake kubwa. Nyenzo iliyotumika kusimamia usitishaji wa mapigano inaweza pia kusaidia kuweka mipaka kati ya nchi au kusimamia uteketezaji wa silaha za kemikali. Ni zana chache za kimataifa zilizo na uwezo huo.”
Kusaidia nchi kuwa taifa
Miongoni mwa mafanikio ya awali ya misheni hizi ni mchango wake katika safari ya Libya kuelekea uhuru.
Mwishoni mwa miaka ya 1940, Libya, iliyokuwa koloni la Italia kati ya mwaka 1911 na 1942 na kabla yake sehemu ya Milki ya Ottoman, ilikuwa imegawanyika kisiasa na kiutawala, huku maeneo yake yakitumia sarafu tofauti.
Tume ya Umoja wa Mataifa ilisaidia kuleta mwafaka wa kisiasa, kuandaa katiba, kuunda serikali ya mpito, kuanzisha mfumo mmoja wa fedha na kuwajengea uwezo watumishi wa umma.
Miaka miwili baadaye, Libya ikawa taifa la kwanza kupata uhuru kupitia mchakato uliosimamiwa na Umoja wa Mataifa.
Misheni kama hizi pia zilisaidia mchakato wa kuondoa ukoloni katika maeneo mengine. Umoja wa Mataifa ulisimamia kura za maoni nchini Cameroon, Guinea ya Ikweta na Togoland, ulifanya mashauriano ya wananchi nchini Bahrain na kusaidia mataifa mapya kujenga taasisi zake za utawala.
Diplomasia wakati wa Vita Baridi
Katika kipindi cha Vita Baridi, ushindani kati ya mataifa makubwa mara nyingi ulifanya Baraza la Usalama kushindwa kufikia makubaliano. Hali hiyo ilifanya Umoja wa Mataifa kutegemea zaidi wajumbe maalum wa Katibu Mkuu.
Katika miaka ya 1980, Mwakilishi Binafsi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliongoza mazungumzo ya miaka kadhaa kuhusu Afghanistan yaliyohitimishwa kwa kutiwa saini kwa Mikataba ya Geneva mwaka 1988.
Wakati huohuo, Mwakilishi Maalum mwingine alisaidia kuendeleza mazungumzo kati ya Iran na Iraq wakati wa mojawapo ya vita vya muda mrefu na vya umwagaji damu zaidi katika karne ya ishirini.
Kwa mujibu wa DiCarlo, historia hiyo inaonesha kwamba tofauti za kisiasa za kimataifa si sababu ya kuacha juhudi za diplomasia.
“Mgawanyiko wa kijiografia na kisiasa si kisingizio cha kutokuchukua hatua,” anasema na kuongeza kuwa, “Misheni maalum za kisiasa zilifanya kazi katika kipindi chote cha Vita Baridi na zilipata mafanikio makubwa.”
Changamoto mpya baada ya Vita Baridi
Baada ya kumalizika kwa Vita Baridi, migogoro mingi iliyokuwa imezuiwa ilizuka upya, na hivyo kuongeza mahitaji ya misheni maalum za kisiasa.
Kuanzia miaka ya 1990, misheni hizi zilianza kusaidia nchi kuandaa uchaguzi, kuandika katiba mpya, kufanya mageuzi ya taasisi za serikali na kujenga upya imani baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Mafanikio makubwa yalishuhudiwa Tajikistan, ambako misheni ya Umoja wa Mataifa ilisaidia kutekeleza Mkataba wa Amani wa mwaka 1997 na kuwezesha mpito kutoka vita vya wenyewe kwa wenyewe hadi amani.
Misheni kama hizo pia zilifanya kazi nchini El Salvador, Guatemala, Burundi, Somalia, Nepal, Angola, Haiti na mataifa mengine mengi. Wakati huohuo, paneli za wataalamu zilianzishwa kufuatilia utekelezaji wa vikwazo vya Baraza la Usalama.
Kadiri miaka ilivyopita, mamlaka ya misheni hizi yaliendelea kupanuka. Baada ya Mgogoro wa Suez wa mwaka 1956, Umoja wa Mataifa ulisimamia operesheni ya kusafisha Mfereji wa Suez. Mwaka 2002, uliisaidia Cameroon na Nigeria kutekeleza uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki kuhusu uwekaji wa mipaka. Mwaka 2013, Baraza la Usalama lilianzisha misheni ya pamoja ya Umoja wa Mataifa na OPCW kusimamia uteketezaji wa silaha za kemikali nchini Syria.
Haiti na changamoto za mpito wa kisiasa
Haiti ni mfano wa namna misheni maalum za kisiasa zinavyoendelea kujibadilisha kulingana na mazingira.
Badala ya kusimamia utekelezaji wa makubaliano ya amani, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuweka utulivu nchini Haiti (BINUH) inalenga kuhimiza mazungumzo jumuishi ya kisiasa, kusaidia maandalizi ya uchaguzi baada ya miaka mingi bila uchaguzi wa kitaifa na kuratibu msaada wa kimataifa wakati nchi ikikabiliwa na changamoto za usalama na udhaifu wa taasisi za serikali.
Carlos Ruiz Massieu, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Haiti na Mkuu wa BINUH, alisema msingi wa mafanikio ya misheni hiyo ni uaminifu.
“Kuna imani kubwa kwa Umoja wa Mataifa,” anasema, akibainisha kuwa pia kuna matarajio kwamba misheni maalum za kisiasa zina uwezo wa kuleta matokeo. Alisisitiza kuwa uaminifu huo unapaswa kulindwa, kuthaminiwa na kuendelezwa.
Kazi isiyoonekana lakini yenye athari chanya kubwa
Kufikia mwisho wa mwaka 2025, Umoja wa Mataifa ulikuwa na misheni maalum za kisiasa 40 duniani kote.
Leo, misheni hizo zimejikita zaidi katika kuzuia migogoro, upatanishi, diplomasia ya kikanda na kusaidia michakato ya amani inayozingatia mazingira mahsusi ya kila nchi.
Mara nyingi kazi yake hufanyika kimya kimya kupitia diplomasia ya faragha, mazungumzo ya siri na ushirikiano wa muda mrefu na serikali, pande zinazohusika katika migogoro, mashirika ya kikanda na asasi za kiraia.
Shamala Kandiah Thompson, Mkurugenzi Mtendaji wa Security Council Report, Shirika huru lisilo la kiserikali ambalo hutoa taarifa na uchambuzi kuhusu shughuli za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, anasema misheni hizi “kwa utulivu zimekuwa nyenzo muhimu ya kuzuia migogoro na kuimarisha ushirikiano wa kisiasa.”
Anaongeza kuwa ingawa hazionekani sana kama operesheni za walinda amani, umuhimu wake haupungui hata kidogo.
Akihitimisha, DiCarlo anasema chapisho hilo si kumbukumbu ya historia pekee, bali pia ni ukumbusho wa uwezo wa diplomasia katika kujenga amani, “hata katika mazingira magumu zaidi, mazungumzo yanaweza kufungua milango, subira inaweza kujenga uaminifu, na diplomasia inaweza kubadilisha mkondo wa historia.”
Huenda hiyo ndiyo sababu misheni maalum za kisiasa zimeendelea kuwa miongoni mwa nyenzo muhimu zaidi ingawa mara nyingi hazionekani za Umoja wa Mataifa katika kuzuia migogoro. Mafanikio yake makubwa hayapimwi kwa ushindi wa kijeshi wala vichwa vya habari, bali kwa migogoro iliyozuiliwa na vita ambavyo havikutokea kamwe.