Taarifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP iliyotolewa leo huko Abuja, mji mkuu wa Nigeria inasema tathmini hiyo imewekwa bayana baada ya uchambuzi wa hali ya upatikanaji wa chakula na lishe uliofanywa na program iitwayo Cadre Harmonisé.

Uchambuzi huo umeonesha kuwa  zaidi ya watu milioni 17 katika majimbo 9  yaliyoathiriwa vibaya na migogoro wanakabiliwa na njaa ya kiwango cha kati, dharura au janga.

Katika jimbo la Borno pekee lililoko kaskazini-magharibi mwa Nigeria, zaidi ya watu milioni tatu wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, huku zaidi ya watu 10,000 wakikabiliwa na njaa ya kiwango cha janga, ambacho ni kiwango cha juu.

Kauli ya Mkuu wa WFP Afrika Magharibi na Sahel

Akizungumza kuhusu yaliyobainika, Mkurugenzi wa Kanda wa WFP kwa Afrika Magharibi na Kati, Kinday Samba, amesema, “Kinachotutia wasiwasi zaidi ni jinsi mgogoro huu unavyoendelea kusambaa. Migogoro sasa inaenea katika maeneo mengi zaidi, ikiwalazimu watu kuondoka mashambani na kuzuia upatikanaji wa misaada ya kibinadamu, hivyo njaa inaongezeka kwa haraka.”

WFP inaeleza kuwa changamoto za usalama na upungufu mkubwa wa fedha vimepunguza uwezo wa kuwafikia wahitaji. Hivi sasa, kati ya watu milioni 6.2 wanaokabiliwa na uhaba wa chakula katika majimbo matatu ya kaskazini mashariki, shirika hilo linaweza kuwasaidia watu 740,000 pekee, na kuwaacha zaidi ya watu milioni 5.5 bila msaada wa chakula na lishe.

WFP yaomba msaada wa haraka

Shirika hilo linaonya kuwa kusitishwa kwa misaada ya chakula kunachochea kuhama kwa wananchi, utumikishaji na ukatili wa kijinsia, huku baadhi ya watu wakijiunga na makundi yenye silaha ili kupata chakula au kipato. “Wakati watu wanapopoteza fursa ya kupata chakula, hatari za kuhama makazi, kunyonywa na kuongezeka kwa ukosefu wa utulivu huongezeka. Hata hivyo, rasilimali tulizonazo sasa ziko katika kiwango cha chini kabisa wakati ambapo zinahitajika zaidi,” amesema Samba.

WFP imeeleza kuwa inahitaji dola milioni 89 za Marekani katika kipindi cha miezi sita ijayo ili kuendelea kutoa msaada wa chakula, lishe na huduma muhimu za usafirishaji wa misaada kaskazini mwa Nigeria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *