Katika mahojiano na Leah Mushi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, Rashid amesimulia safari yake na kutuma ujumbe maalum kwa vijana wanaotamani kuomba fursa za mafunzo kwa vitendo ndani ya Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa.

Rashid anaanza kwa kueleza alijisikiaje alipopokea taarifa kuwa amefanikiwa kupata fursa hiyo.

Rashid: “Kwa kweli nilifurahi sana. Nilijua watu wengi duniani wanaomba nafasi kama hizi, hasa katika Umoja wa Mataifa. Mwanzoni sikuamini kama nitachaguliwa. Lakini nilipopata nafasi hii, nilijua ni fursa kubwa ya kujifunza kutoka kwa watu wenye uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano.”

UN News/Rashid Malekela Rashid Malekela wa UN News Kiswahili akizungumza na Mbaharia wa Kikundi cha Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) katika mwalo wa Luchelele, Funga Gavana (kulia) akizungumza kuhusu uhifadhi wa Ziwa Victoria huko Mwanza Tanzania.
Leah: Kabla na baada ya mafunzo kwa vitendo, tofauti unaionaje?

Rashid: “Tofauti ni kubwa sana. Chuoni tunajifunza nadharia na vitendo kwa kiwango fulani, lakini huku unakutana na uhalisia wa kazi.

Nimejifunza kuandika habari za aina mbalimbali kwa tovuti, redio na video. Leo naweza kuchukua habari moja na kuiandaa kwa majukwaa tofauti. Pia nimeelewa kwa undani namna Umoja wa Mataifa na mashirika yake yanavyofanya kazi kila siku.

Kwa kifupi, sipo tena pale nilipokuwa Januari.”

Leah: Ni jambo gani hutalisahau katika kipindi chote cha mafunzo?

Rashid: “Nimefanya kazi nyingi nzuri, lakini moja iliyonigusa sana ilikuwa habari kuhusu Siku ya Furaha Duniani. Tulizungumza na wananchi mbalimbali kuhusu nini kinawapa furaha.

Nilivutiwa na majibu yao. Wengine walisema furaha yao ni kumuona mama au watoto wao wakiwa wazima. Mvuvi mmoja alisema kurudi salama kutoka ziwani na kupata chakula kwa familia yake ndiyo furaha yake kubwa.

© UNESCO/Mariam Kungwi Rashid Malekela anaeleza Mwongozo wa Athari kwa Vijana Waelimishaji Rika kutoka UNESCO kwa ajili ya kukuza ujuzi wa vyombo vya habari na habari kwa nafasi salama za kidijitali mwaka 2025 katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Ilinikumbusha kuthamini hata vitu vidogo ambavyo mara nyingi tunavipuuzia.”

Leah: Kwa nini mafunzo kwa vitendo ni muhimu kwa vijana?

Rashid: “Mafunzo kwa vitendo ni muhimu sana kwa sababu yanakuandaa kwa mazingira halisi ya kazi. Unajifunza si tu kazi yenyewe, bali pia ushirikiano, mawasiliano, uvumilivu na namna ya kupokea marekebisho.

Waajiri wengi wanataka kuona siyo tu cheti, bali pia uzoefu na matokeo ya kazi zako. Mafunzo kwa vitendo yanakupa nafasi ya kujenga vitu vinavyoonekana, habari ulizoandika, makala, video au miradi uliyoshiriki.

Hivyo ni muhimu sana kwa vijana kwa sababu inakupa nguvu kubwa unapokwenda kuomba kazi.”

Leah: Kuna ofisi ambazo hazilipi wanaofanya mafunzo kwa vitendo. Hilo unalizungumziaje?

Rashid: “Ni kweli, si ofisi zote zinazotoa fursa ya mafunzo kwa vitendo zinalipa. Lakini wakati mwingine thamani ya uzoefu unaoupata ni kubwa kuliko fedha ya muda mfupi.

Kupitia mafunzo kwa vitendo haya niliyoshiriki, nimefanya kazi na mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa kama UNICEF na UNDP, nimesafiri ndani na nje ya nchi, nimekutana na wataalamu wa mawasiliano na nimejenga mtandao mkubwa wa kazi.

UN News/Rashid Malekela Rashid Malekela (kushoto akisimama) akiwa mmoja wa maafisa wa UNICEF katika mafunzo ya TACAIDS, UNICEF ya kuwajengea uwezo vijana kudhibiti UKIMWI nchini Tanzania

Hiyo ni thamani kubwa sana kwa mustakabali wa taaluma yangu.”

Leah: Unamwambia nini kijana mwenye hofu ya kuomba fursa hizi?

Rashid: “Kwanza kabisa, usiogope. Mafunzo kwa vitendo siyo kwa watu waliokwishakuwa wataalamu wakubwa. Ni kwa watu wanaotaka kujifunza.

Huhitaji kuwa na uzoefu wa miaka mingi. Kinachohitajika ni kutimiza sifa za msingi, kujiamini na kuthubutu kutuma maombi.

Watu wengi wana sifa lakini hawaombi kwa sababu ya hofu au kutojiamini. Mimi nasema: jiamini, unaweza. Tuma maombi yako.

Fursa kama hizi zinaweza kubadilisha maisha yako.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *