Kwa Zinab, mwenye umri wa miaka 20 kutoka Adwa, jimbo la Tigray nchini Ethiopia, jina hilo sasa lina maana ya binafsi zaidi.

Kuibiwa jangwani, kumwagiwa petroli baharini

Simulizi yake inaanza Siku ya jumatano tarehe 25 Machi, 2026, boti aliyokuwa akisafiria ilizama karibu na pwani ya Djibouti. Watu wasiopungua tisa walifariki dunia, huku 45 wakitoweka na kuaminika kufariki. Zinab ni miongoni mwa manusura wachache.

Akiwa ametoka katika eneo lililoathiriwa kwa miaka mingi na migogoro, Zinab aliondoka nyumbani kwao akiwa na ndoto moja, kuisaidia familia yake na kutafuta maisha bora nje ya mazingira ya changamoto.

Nilitaka kujitegemea na kubadilisha maisha ya familia yangu. Ndiyo sababu niliondoka,” anasema.

Safari yake ilianza kwa maumivu. Aliporwa fedha na simu, akavuka maeneo ya jangwani kwa siku kadhaa bila chakula wala maji ya kutosha.“Tulikaa ufukweni kwa siku tatu. Hakukuwa na chakula wala maji, ni jangwa tu,” anakumbuka.

Kisha safari ya baharini ikaanza, na hofu ikaongezeka. Dhoruba ilipoanza, wasafirishaji walimimina mafuta ya petroli juu ya abiria ili kuwazuia wasisonge ndani ya boti iliyokuwa imejaa kupita kiasi.

Baadaye taharuki ilitanda. Hofu ilizidi baada ya taarifa kuwa mwanamke mmoja alikuwa amepoteza maisha kwa kukosa hewa.

Ndipo boti ikazama.

Watu wengi walikufa mbele ya macho yetu. Marafiki. Ndugu. Miili yao haikupatikana tena, Zinab anasema kwa sauti ya chini iliyojaa huzuni.

Maumivu yasiyo elezeka

Kinachoumiza zaidi kwa manusura wengi kama Zinab si tu kupona kimwili, bali kubeba maumivu ya kupoteza wapendwa wao na mzigo wa kurudi nyumbani mikono mitupu. Kwa wengi, safari hizi hubeba sio ndoto zao binafsi pekee, bali pia matumaini ya familia nzima iliyobaki nyumbani.

Zinab aliokolewa baadaye na walinzi wa pwani wa Djibouti kwa ushirikiano na mamlaka za nchi hiyo pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, IOM, lililotoa msaada wa haraka wa kitabibu na kisaikolojia.

Sasa anapatiwa hifadhi na usaidizi katika kituo cha uhamiaji cha Obock, Djibouti.

Sasa natakiwa kurudi nyumbani… lakini bila sababu yoyote,” anasema.

IOM na msaada kwa manusura

Afisa ulinzi wa IOM, Hawa Moussa, anasema siku za mwanzo baada ya ajali zilikuwa ngumu sana. Walikuwa katika hali mbaya sana. Zinab alikuwa hasemi kabisa na alikuwa akisumbuliwa na ndoto mbaya mara kwa mara, anasema.

Kupitia ushauri nasaha na msaada wa karibu, Zinab ameanza kurejea taratibu kwenye hali ya kawaida. Moja ya nyakati zilizompa faraja zaidi ilikuwa kuwasiliana tena na familia yake.

Alipoongea na kaka yake, alionekana mwenye furaha sana,” anasema Hawa.

Ingawa kumbukumbu za ajali hiyo bado zinamuumiza, polepole Zinab ameanza kutazama mbele. Kwa msaada wa IOM, sasa anajiandaa kurejea nyumbani kwao Ethiopia kuanza ukurasa mpya wa maisha.

Kila mwaka, maelfu ya wahamiaji huendelea kuhatarisha maisha yao kupitia njia hii wakikimbia migogoro, umaskini na ukosefu wa fursa. Wengine hutafuta usalama, wengine kazi, na wengi wanatafuta nafasi ya maisha bora kwa ajili yao na familia zao.

Lakini kwa wengi, safari huishia baharini.

Kwa Zinab, nyuma yake kuna maji yaliyochukua maisha ya wengi. Mbele yake kuna maisha yasiyo na uhakika lakini angalau bado yuko hai kuyakabili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *