
CHAMA cha Gofu cha Wanawake Tanzania (TLGU), juzi kilizindua rasmi Dira ya Rais pamoja na Mpango Mkakati wa Miaka Mitano (2026-2030), huku kikitangaza mashindano ya The Lady President’s Golf Cup 2026 yatakayofanyika Julai 11, katika Viwanja vya Gofu vya Lugalo, Dar es Salaam.
Kupitia kaulimbiu ya “Piga kwa Ujasiri, Tengeneza Mustakabali” chama hicho kimeeleza kuwa kinaanza safari mpya ya kuimarisha maendeleo ya gofu ya wanawake nchini kwa kuongeza ushiriki wa wanawake na wasichana, kukuza vipaji, kuandaa viongozi na kuiweka Tanzania kwenye ramani ya gofu ya wanawake barani Afrika.
Rais wa TLGU, Timea Chogo, alisema dira hiyo inalenga kuweka msingi imara wa maendeleo ya mchezo huo kwa kizazi cha sasa na kijacho.
“Tunataka kuona kila msichana mwenye ndoto ya kucheza gofu akipata nafasi ya kuanza, kukua na kufikia kiwango cha kuiwakilisha Tanzania kimataifa. Dira yetu haiishii kuandaa mashindano pekee, bali ni kujenga mfumo endelevu wa kukuza vipaji, kuandaa viongozi na kutumia gofu kama chombo cha maendeleo ya wanawake katika nyanja mbalimbali za maisha,” alisema Chogo.
Mpango huo wa miaka mitano umejengwa katika nguzo kuu tatu ambazo ni ‘Victory Path’, unaolenga kuimarisha ushindani kupitia maendeleo ya timu ya taifa, ushiriki wa mashindano ya kimataifa, usajili wa wachezaji kwenye World Amateur Golf Ranking (WAGR) na kuanzisha mfumo wa viwango vya kitaifa.
Nguzo ya pili ni Eagle Initiative, itakayolenga kuongeza ushiriki wa watoto na vijana kupitia programu za gofu mashuleni, utekelezaji wa SNAG Golf na kuandaa njia ya kukuza vipaji kutoka shule hadi timu za taifa.
Nguzo ya tatu ni Beyond the Fairway, ambayo inalenga kutumia mchezo wa gofu kama jukwaa la kukuza uongozi wa wanawake kupitia mafunzo, maendeleo ya taaluma, ufadhili wa masomo na kujenga mitandao ya kitaaluma. Katika mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa mkakati huo, TLGU inalenga kuongeza wanachama hai kutoka 110 hadi zaidi ya 150, kuanzisha mashindano makuu matatu ya kila mwaka, kuzindua programu za vijana Dar es Salaam na Arusha, kusajili zaidi ya wasichana 20 kwenye programu za maendeleo ya gofu na kuipeleka timu ya taifa ya wanawake kushiriki mashindano ya kimataifa kwa mara ya kwanza.
Mashindano ya The Lady President’s Golf Cup 2026 yatakuwa hatua ya kwanza ya utekelezaji wa mkakati huo, yakitarajiwa kuwakutanisha wachezaji wa gofu wa ridhaa, viongozi wa serikali, sekta binafsi, wanadiplomasia na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Mbali na ushindani wa uwanjani, mashindano hayo yataambatana na programu za uongozi, mafunzo, mijadala ya kitaalamu, shughuli za kuwajengea uwezo wanawake na fursa za kujenga mitandao ya kikazi, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuyafanya kuwa miongoni mwa matukio makubwa ya gofu ya wanawake Afrika Mashariki.