WAO si walipanda fuso? Ndilo lilikuwa swali lililotawala midomoni mwa maelfu ya mashabiki wa Simba waliojitokeza kuipokea timu hiyo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, baada ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la CRDB.

Mashabiki hao walikuwa wakirejea tukio la jana Jumamosi ambapo watani wao Yanga walifanya paredi ya ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC huku safari hii wakitumia nafasi hiyo kurusha vijembe baada ya Simba kuwasili na msafara ulioongozwa na mabasi mawili ya kisasa aina ya Iriza, yaliyobeba wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa klabu hiyo.

Simba ilifuta majonzi ya  msimu huu kwa kutwaa taji la CRDB jana Jumamosi, kisiwani Pemba baada ya kuichapa Azam bao 1-0 katika fainali iliyochezwa Uwanja wa Gombani, hivyo kujihakikishia kumaliza msimu ikiwa na mataji mawili, ikianza na la Muungano.

ir 02

Asubuhi ya leo Jumapili Julai 5, 2026, kikosi hicho kilirejea Dar es Salaam kikitokea Pemba na kupokewa na umati mkubwa wa mashabiki waliokuwa wamefurika mapema kabisa uwanjani hapo wakisubiri kwa hamu kuwaona mabingwa wao.

Mara baada ya mabasi hayo kuanza safari ya paredi, nyimbo, nderemo na vifijo vilitawala huku mashabiki wakipaza sauti za kejeli kuelekea kwa watani wao. 

Mbali na vijembe hivyo, mashabiki wa Simba walionekana kuwa na furaha kubwa baada ya miaka minne mfululizo kukosa taji kubwa la ndani. 

ir 02

Wengi walivaa jezi nyekundu, waliinua bendera za klabu hiyo na kuwashangilia mastaa wao waliokuwa wakipunga mikono.

Msafara huo uliondoka JNIA ukiwa chini ya ulinzi wa vyombo vya usalama, ukipita barabara ya Nyerere kuelekea Tazara, kisha kuifuata barabara ya Nelson Mandela hadi Buguruni na kukatiza barabara ya Uhuru, huku mamia ya wananchi wakiendelea kujiunga njiani kuisindikiza timu hiyo kuelekea katikati ya jiji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *