DAR ES SALAAM: TANZANIA imeendelea na maandalizi muhimu kuelekea kuanza matumizi ya nishati ya nyuklia kwa ajili ya uzalishaji wa umeme, kwa kufuata hatua mbalimbali zilizoainishwa na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA). Kwa mujibu wa mwongozo wa IAEA, nchi inapaswa kutekeleza vipengele 19 katika awamu tatu kabla ya kuanza rasmi kuzalisha umeme wa nyuklia.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 5, 2026, katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC), Prof. Najat Kassim Mohammed, amesema mchakato huo unazingatia viwango vyote vya kimataifa vya usalama. Amesisitiza kuwa hatua zote zinazochukuliwa zinalenga kuhakikisha matumizi ya teknolojia ya nyuklia yanakuwa salama kwa wananchi na mazingira.
Prof. Najat amesema Tanzania bado haijaanza rasmi awamu ya kwanza ya utekelezaji, lakini tayari imekamilisha maandalizi ya awali. Ameeleza kuwa serikali imewaalika wataalamu wa IAEA kufanya tathmini ya utayari wa nchi ili kubaini kama imefikia vigezo vinavyoruhusu kuanza awamu hiyo. Amefafanua kuwa hatua ya kwanza inahusisha kuweka mfumo madhubuti wa kisheria na kiudhibiti pamoja na kuimarisha taasisi ya udhibiti wa usalama wa matumizi ya nishati ya nyuklia.

Ameongeza kuwa endapo tathmini ya IAEA itatoa matokeo chanya, Tanzania itaruhusiwa kuendelea na hatua zinazofuata za utekelezaji. Lengo la serikali ni kuhakikisha ndani ya takribani miaka saba nchi inafikia uwezo wa kuanza kuzalisha umeme wa nyuklia kwa matumizi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Kuhusu upatikanaji wa malighafi, Prof. Najat amesema Tanzania ina akiba kubwa ya madini ya urani, ambayo ndiyo malighafi muhimu katika uzalishaji wa umeme wa nyuklia. Hata hivyo, ameeleza kuwa urani inayochimbwa haiwezi kutumika moja kwa moja kuzalisha umeme, bali hulazimika kupitia mchakato maalumu wa kitaalamu na gharama kubwa ili kuandaliwa kuwa mafuta ya nyuklia. Katika hatua za mwanzo, urani itachimbwa nchini na kusafirishwa nje kwa ajili ya kuchakatwa, ambapo kwa sasa Tanzania inashirikiana na Urusi katika mchakato huo kabla ya kurejeshwa kwa matumizi ya uzalishaji wa umeme.
Aidha, Prof. Najat amesema mradi mkubwa wa uchimbaji wa urani unatarajiwa kuanza katika eneo la Mkuju, mkoani Ruvuma, huku tafiti zikiendelea katika maeneo mengine ya nchi kubaini uwepo wa akiba yenye tija ya madini hayo. Amewahakikishia wananchi kuwa hakuna sababu ya kuwa na hofu kuhusu matumizi ya nishati ya nyuklia, akisisitiza kuwa usalama unabaki kuwa kipaumbele kikuu katika kila hatua ya utekelezaji wa mpango huo.