OFISA Habari wa Simba, Ahmed Ally, amefichua kuwa basi lao jipya la kisasa aina ya Iriza lililozinduliwa rasmi leo wakati wa paredi ya ubingwa wa Kombe la CRDB, limegharimu Sh1.5 bilioni, akisema ni sehemu ya uwekezaji unaoendelea kuifanya klabu hiyo kuwa ya kisasa zaidi.

Ally amesema hayo katika kilele cha paredi kilichofanyika Coco Beach ambapo maelfu ya mashabiki wa Simba walijitokeza kusherehekea ubingwa huo uliopatikana baada ya kuifunga Azam bao 1-0 kwenye fainali iliyochezwa Uwanja wa Gombani, Pemba.

Akizungumza mbele ya mashabiki hao, Ally amesema basi hilo ndilo litakalokuwa usafiri rasmi wa kikosi cha Simba, likiwa limegharamiwa na Kampuni ya JAYRUTTY, ambayo ni mzabuni wa jezi za klabu hiyo.

“Hili ni basi letu rasmi. Walisema basi letu ni bovu, wakasema mambo mengi lakini leo tumewajibu kwa vitendo. Basi hili limegharimu Sh1.5 bilioni,” amesema.

Ally amesema basi hilo lina vifaa vya kisasa vinavyolenga kuwapa wachezaji mazingira bora ya usafiri, akitaja kuwa lina sehemu ya masaji, mashine ya kutengeneza kahawa, friji na huduma nyingine zinazopatikana kwenye mabasi ya kisasa duniani.

Ally pia amewatupia vijembe wapinzani wao wa jadi, Yanga akisema uzinduzi wa basi hilo umeonyesha dhamira ya klabu kuendelea kufanya uwekezaji mkubwa badala ya kujibu maneno kwa maneno.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Jayrutty Investment, Joseph Rwegasira, amewapongeza mashabiki wa Simba kwa namna walivyoendelea kuiunga mkono timu hiyo katika kipindi chote cha msimu.

“Kwanza nawapongeza Wanasimba kwa moyo mkubwa wa kuisapoti timu yenu. Watu wameongea mengi, lakini Simba imerudi kwenye kiwango chake,” amesema.

Rwegasira amesema kampuni yake itaendelea kushirikiana na Simba katika safari ya maendeleo ya klabu hiyo, akiahidi msimu ujao kutakuwa na maandalizi makubwa zaidi ya kusherehekea mafanikio.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *