Dodoma. Chama cha ACT -Wazalendo kimewaasa vijana kufanya siasa za mapambano ya kutafuta haki, lakini wajiepushe na siasa za matusi.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumapili, Julai 4, 2025 na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu, wakati alipozungumza na vijana wanafunzi wa vyuo vikuu, wakiwemo 130 waliojiunga na chama hicho kwa mara ya kwanza, na wamefanya mkutano wa ndani kwa uratibu wa ngome ya vijana wa chama hicho.

Ado, ambaye ni mbunge wa Tunduru Kaskazini, amesema chama hicho hakiamini katika matusi bali kinaamini katika ujenzi wa demokrasia na mapambano ya kutafuta haki.

Amesema vijana wasomi lazima watambue wajibu wao kuwa elimu wanayoipata itumike kuleta mabadiliko kwa kuusema ukweli na kudai demokrasia bila kurudi nyuma, ikiwemo Katiba mpya na elimu bila ada kuanzia shule za awali hadi vyuo vikuu.

“Vuguvugu la vijana katika kuleta mapinduzi lazima mlifanye kwa haki, msitoe matusi, badala yake semeni ukweli. Tutawapa mbinu kupitia madarasa ya itikadi katika vyuo vyenu,” amesema Ado.

Amesema pia vijana wanapaswa kusoma kwa bidii ili watambue na kuufahamu ukweli, siyo kukurupuka bila kujua wanachokisema.

Ameagiza viongozi wa ngome ya vijana kupaza sauti kwa kuusema ukweli na waanzie kutetea vijana 436 waliodaiwa kujenga Ikulu ya Chamwino, ambao kwa mujibu wake walipewa ahadi ya ajira na aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli, lakini wameachwa.

Katibu huyo amesema kizazi kisichohoji hakifai, bali wasomi wanapaswa kuhoji na kupambana kutafuta ukweli bila kuupindisha kwa maslahi ya wananchi wa Tanzania.

Katika hatua nyingine amesema matamko yanayotolewa na baadhi ya viongozi, ikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama, hayafuati misingi ya Katiba bali kuna ukiukwaji wa haki.

Naibu Katibu wa ngome ya vijana kwa vyuo vikuu, Japheth Mkuya, amesema huu si wakati wa kusinzia bali ni wa mapambano ya kweli bila kukata tamaa.

Amesema hakuna aliyefanikiwa kwa kulala na kuamka akajikuta amefanikiwa, bali lazima apitie magumu na misukosuko mingi kama ilivyo kwa baadhi ya watu maarufu Tanzania na duniani.

Katika kusanyiko hilo walikuwepo vijana kutoka vyuo vikuu vya Dodoma (UDOM), Mipango, St John’s, Veta na Chuo cha Biashara (CBE), vyote vya jijini Dodoma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *